Katika Uchaguzi mdogo huo, Tambwe Hiza alikuwa Mgombea wa CUF jimbo la Temeke, Hussein Mmasy alikuwa Mgombea wa CUF katika jimbo la Ubungo. Kampeni zilifana sana. Vijana walijitolea na kukodi malori (Fusso) kwenda kwenye mikutano ya hadhara iliyokuwa na hamasa kubwa. Marehemu Tambwe Hiza alikuwa na kipaji cha kuhutubia na kuchekesha.
Salama Masoud, wakati huo bado kijana mdogo - nadhani alikuwa bado anasoma - alikuwa mshehereshaji wa jukwaa katika kampeni za Temeke. CUF ilikuwa tishio kubwa. Kila siku ya kampeni, Wananchi – wafuasi wa CUF - walikamatwa na kuwekwa ndani. Naamini tulishinda chaguzi ndogo za Ubungo na Temeke, lakini kama kawaida CCM na dola walicheza rafu.
Nadhani hofu kubwa ya CCM ilikuwa kuitangaza CUF kuwa imeshinda uchaguzi wa majimbo mawili ya Dar es Salaam, wakati tunaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2000. Vyombo vya Dola vilitumiwa kuhakikisha Wagombea wetu hawatangazwi kuwa wameshinda.