Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

Kwahivyo, naweza kusema kuwa yeye kwangu mimi ni zaidi ya mzee, ni zaidi ya kiongozi, ni zaidi ya Maalim katika shughuli zangu. Hivyo ndivyo ninavyomkumbuka Maalim Seif katika safari ya kisiasa.

Maalim Seif huwezi kumtia ila hata kwa nukta ndogo katika maswala ya ufisadi licha ya kuwa katika madaraka na nafasi za juu kwa muda mrefu sana.
 
Kuna jambo ambalo Maalim Seif mwenyewe alilitaja katika kitabu chake alichokiandika kinachokusanya kumbukumbu za maisha yake, pamoja na maisha ya Comrade Ali Sultan. Alitaja kadhia ambayo hata mimi binafsi nakumbuka kuwa aliwahi kunieleza, na hata akikaa na jamaa wengine alikuwa anaizungumzia ambayo iliwashangaza wengi.
 
ZAWADI BINAFSI KUTOKA KWA MFALME WA BRUNEI:
Mwaka 1987 alikuwa waziri kiongozi, alifanya ziara katika nchi za mashariki ya mbali akiitafutia Zanzibar mahusiano makubwa ya kiuchumi, na ndio safari yake ya mwanzo kufika Singapore, hata baadae tukaja tukatafuta idea ya kuja kusema Zanzibar inaweza kuja kuwa Singapore ya Afrika Mashariki.
 
Lakini safari ile pia ilimpeleka katika nchi (Kisiwa) ya Brunei. Baada ya kukutana na mfalme wa Brunei katika Hijja Makkah, Saudi Arabia. Katika ziara ile, kama tunavyojua Mfalme wa Brunei alitajwa kuwa ni mtu tajiri zaidi kuliko watu wote duniani kwa miaka ile, alimtunuku Maalim zawadi binafsi ya dola milioni tatu ($3,000,000), na alimwambia kuwa hii ni zawadi yako binafsi. Lakini aliporudi fedha zile Maalim Seif aliziingiza katika akaunti ya serikali katika hazina ya Zanzibar.
 
Alisema kuwa Mfalme wa Brunei hanijui mimi, bali ananitambua mimi kama Waziri Kiongozi wa Zanzibar. Kwahivyo fedha hizi haziwezi kuwa ni zawadi yangu binafsi na siwezi kuzikubali. Na zikaingizwa katika hazina ya Zanzibar. Hakujitajirisha. Alikuwa ni kiongozi kwa zaidi ya miaka arubaini. Hata nyumba za kuishi hana, amebakia kuishi katika nyumba za kukodi. Lakini nyumba yake moja ya Pemba ilibidi ijengwe na kumalizwa na marafiki zake kwasababu ilikuwa inamshinda kujenga.
 
Hakuwahi hata kujishughulisha kumiliki gari isipokuwa gari ambazo alipewa na chama kutumia kwa ajili ya kazi zake, na mambo mengi kama hayo.

Lakini alipoondoka katika nafasi ya uwaziri kiongozi, mwenyewe akisema kulikuwa na jaribio kubwa la kutaka kumchafua, na kuliundwa tume ya kwenda kukagua nyaraka zote katika ofisi za waziri kiongozi kutafuta wapi labda kulikuwa na marupurupu au masurufu aliyoshindwa kurejesha matumizi yake,

wakati alikuwa Maalim Seif hata posho za safari alizokuwa akipewa, akirudi hurejesha stakbadhi za matumizi na fedha zilizobakia huzirudisha katika akaunti ya serikali.
 
KUREJESHA BEGI LENYE FEDHA:
Na la mwisho katika hilo ambalo nataka kulitoa mfano vile vile, wengi hawajalijua kwasababu sijui kama aliwahi kumhadithia mwengine. Katika safari binafsi mara moja alikuwa anakwenda Dubai na alipofika pale alikuwa amechukua briefcase yake, lakini akatokezea mfanyabiashara mmoja mwenye asili ya kiasia ambaye alikuwa ana briefcase iliyofanana mno na yake.
 
Wakati wa kupitisha katika security checkpoint (scan machine) kila mmoja akachukua la mwenzake bila ya kujua. Maalim alinihadithia, alipofiki katika nyumba aliyofikia akalifungua na kukuta limejaa pesa za dola, akajua kwamba sio lake. Jambo hili likamfadhaisha sana. Jambo hili kwa mtu mwengine angelipiga vigeregere kwamba ameokota lulu siku ile.
 
Lakini yeye alichokifanya katika begi lile ni kutafuta contact za yule mwenye begi. Alipozipata akampigia simu na kumwambia nadhani wewe umechukua begi langu, na yule mtu kwa mshituko akamwambia ni kweli. Alishangaa kuwa mtu alichukua begi lenye fedha na anataka kumrejeshea mwenyewe. Na hakumwambia njoo pahala fulani uje unifuate bali alimwambia kuwa atasogea na vijana wake nusu njia na yeye aende nusu njia ili warudishiane mabegi yao. Huyo ndie Maalim Seif ambaye wengi walishindwa kumfahamu.
 
Kwanza niseme kwamba safari ile ilikuwa ni safari miongoni mwa safari alizokuwa akizifanya mwaka 1993 baada ya kuundwa vyama vingi na CUF kupata usajili wa kudumu. Aliamua yeye wakati ule alipokuwa makamo mwenyekiti akifuatana na wenzake wawili watatu kuwazungukia viongozi mbali mbali wa kitaifa; Jaji mkuu, Spika, na watu wengine mashuhuri akiwemo Mwalimu Nyerere; kwajili ya kwenda kuelezea dhamira ya kuunda chama cha CUF, na nini chama cha CUF kinasimamia. Na mote humo alikuwa akichukua nyaraka za msingi.
 
Kuna picha maarufu ile ambayo anaonekana akizungumza na Mwalimu. Kwa bahati mbaya ile picha imepigwa wakiwaonesha wawili wao tu kwasababu ndio waliokuwa focus ya mkutano ule. Lakini pia pale alikuwa amefuatana na wenzake. Alikuwa amefuatana na Hamad Rashid Mohammed, Marehemu Mzee Shaaban Khamis Mloo, na Marehemu Khatib Hassan.

Na lile linaloonekana katika meza pale, kaprasha nililifunga mimi nikiwa kama katibu wake, ndani yake kulikuwa na katiba ya CUF, muongozo wa sera za CUF, na baadhi za hotuba alizozitoa Maalim Seif zilokuwa zikielezea muelekeo wa kisiasa wa CUF akimchukulia zawadi Mwalimu Nyerere.
 
Lakini khasa alichokwenda kumwambia alimwambia kwamba tumekuja kwako kukuambia kuwa tumeunda chama, na wewe na wenzako (akimwmabia kwa utani) mmetufukuza CCM, lakini sasa tuna fakhari kuwa vyama vingi vimekaribishwa, na walimshukuru mwalimu kwa mchango wake katika kusukuma ule mjadala wa vyama vingi, na baadae wakawa na mazungumzo mengi walofanya.
 
Alimtaka mwalimu aingilie kati suala ambalo lilikuwa limeanza la uvunjwaji wa haki za kibinaadamu na kutoheshimu haki za vyama vipya vya kisiasa vilivyokuwa vimeanza. Akamwambia kwa vile wewe ndie ulikuwa kinara wa kusiamamia upande wa CCM kutaka ikubali mfumo wa vyama vingi, sasa ni jukumu lako la kuepuka madhara, ikumbukwe alikwenda kumuona wakati tayari kushatokea mauwaji ya kwanza ya kisiasa Zanzibar kisiwani Pemba Januari 31, 1993 wakati bendera za CUF zilipopandishwa na watu wakapigwa risasi Shumba Mjini.
 
MAJIBU YA NYERERE KWA MAALIM SEIF:
Jambo moja ambalo linaweza kuwavutia wasikilizaji ni kwamba katika kurejesha majibu Mwalimu alimwmabia kwamba atajitahidi, ingawa alijivua akasema yeye sie tena raisi wa Muungano, lakini angetumia ushawishi wake kulisukuma hilo. Lakini alimwambia kuwa ni kweli nilikufukuza wewe na wenzako, lakini lazima nikiri kuwa haukuwa uamuzi sahihi, na kwamba CCM imepata pigo na imeyumba na imevurugika Zanzibar baada ya kuwafukuza nyinyi lakini mwisho akacheka akamwambia ndio siasa.
 
Lakini madamu sasa muna chama chenu basi muna haki ya kufanya siasa zetu, na nawaomba mufanya siasa za amani na vile vile muhakikishe kwamba munaulinda muungano. Hiyo ndio iliyokuwa lugha ya mwalimu, na niseme maana labda watu wengi hawakusema hadharani, lakini ndani ya kamati kuu ya chama alikuja akatoa briefing (ufupisho) kamili ya mazungumzo yale, ambayo ndio haya ninayoyakariri mimi ambayo niliyasikia kama walivyoyasikia wengine katika kikao kile cha kamati kuu.
 
Lakini nataka niseme kwamba moja ya mambo ambayo Maalim atakumbukwa sana na imemjengea heshima sana, na pengine tunajiuliza kwanini mtu anagombea uraisi mara sita, hapewi kuongoza serikali pamoja na kushinda uchaguzi, na bado akirudi kwenye karatasi za kura Wazanzibari wanamiminika kwa wingi zaidi kuliko mara ya mwanzo kumuongezea kura?
 
Basi kama kuna kitu kinachompa heshima hiyo ni kuwa mkweli katika mambo ambayo aliyaamini, na misimamo yake ya kutoyumba katika anachokiamini. Na hichi tumekishuhudia mara nyingi sisi ambao tumefanya kazi naye, na yameshuhudiwa hadharani kwa vile mambo ya siasa yanakwenda hadharani, lakini pengine wengine walikuwa hawajui nini kilikuwa kinaendelea nyuma ya pazia.
 
MAZUNGUMZO YA MIAFAKA:
Kuna mambo nataka niyagusie machache. Moja, watu wengi hawajui kuwa masuala ya kuingia katika mazungunzo ya miafaka na maridhiano hayajapata kuwa mepesi ndani ya vyama ambavyo amekuwemo (alipokuwa CUF na hata ACT Wazalendo). Watu wengi wamelitaja hili la karibuni la mwaka jana kwasababu ya namna uchaguzi wenyewe ulivyokwenda, lakini mara zote haijapata kuwa rahisi.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…