Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

Mrina na Matokke hawakujali kuyapitia matokeo ya utafiti makini wa wanahistoria na mabingwa wa ilimu ya athari (archaeology) au hata Biblia yenye kumtaja Kush na watu wa kutoka ustaarabu wa Kikushi ambao wanaiunganisha Afrika Mashariki na Somalia, Ethiopia na Bara Arabu. Lakini hilo halikuwa lengo lao na ndio maana safari yao haikuwapeleka huko. Lengo lao lilikuwa kupiga siasa na kuziharibu akili za walimu na wanafunzi kutoka Zanzibar na Tanganyika.
 
Misafara ya masomo ya dhiki na dhuluma Hadithi dhidi ya Waswahili na Waarabu ambazo hazitegemei aina yoyote ile ya ushahidi zimekithiri kama uyoga kunako vichwa na nyoyo zenye kuipa jina baya Dola ya Zanzibar ili ipatikane sababu ya kuiangusha au kuizuwia isije juu. Yako mambo mtu akisema hapohapo hutakiwa ushahidi na hoja mpaka msikilizaji aridhike na kuna mambo hayahitajii hata chembe moja ya ushahidi midamu makapi ya hoja yanaonekana.
 
 
Kwa mfano, R. K. Mwanjisi kwenye kijitabu chake Abeid Amani Karume utakuta ameandika kuwa:

Kuna mambo mengi sana ambayo yalitendeka nchini Unguja na Pemba na ambayo hayana budi yathibitishwe kwa ushahidi kamili, na kuandikwa kwa makini. Kuna nyumba Unguja iitwayo “Mambo Msiige” ambayo baada ya kumalizika kujengwa wale Waafrika walioijenga waliuwawa wote ili wasiige maarifa ya ujenzi wa nyumba kama ile.

Yasemekana pia kuwa wake za Waarabu siku hiyo wakifurahi huwaambia mabwana zao “mie sijapata kuona mtoto anavyokaa tumboni mwa mwanamke, nataka kuona hivi leo.” Basi bwana wa Kiarabu hutuma watumwa wake wamlete mama wa Kiafrika mja mzito na akapasuliwa tumbo kumwonyesha bibi mkubwa jinsi mtoto anavyokaa tumboni! Kisha maiti ya yule mjakazi wa Kiafrika ikatupwa shimoni!
 
Yasemekana kuwa wakati huo Mwarabu akitaka kuhakikisha ikiwa gobori lake lina nguvu humwambia mmoja wa watumishi wake apande mnazi. Akiisha fika juu yule “Bwana” alifyatua gobori lake, kisha “Mtumwa” akalia “Yallah” akaanguka chini na kufa. Kiisha yule Mwarabu akaja na kuipiga teke ile maiti na kusema “Ama, hivi kafa huyu!” Inasemekana kuwa kuna Mwarabu mmoja alizaa mtoto na mtumwa wake Mwafrika. Jambo hili lilipojulikana yule Mwarabu akachukua kisu akamwua yule kijakazi wake na kumtumbukiza chooni!10
 
Hizo ni sumu kali ndani ya kijitabu ambacho lengo lake ni kuzielezeya habari za maisha ya Mzee Abeid Amani Karume kwa wasomaji ambao wanatakiwa wafahamu kuwa: Unguja na Pemba imepita katika tanuri la moto wa utumwa, udanganyifu wa wafanya biashara na washika misahafu, utawala wa kigeni, ubaguzi wa rangi, utetezi, juhudi za uhuru, mapinduzi na ujamaa.11
 
Cha Mwanjisi ni kijitabu kidogo kilichotungwa kwa ajili ya wasomaji wa kawaida. Mambo yalizidi kuwa hatari wakati kasumba kama za Mwanjisi zilipoingizwa ndani ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Zanzibar. Na hayo yalifanywa na Wazanzibari Waafrika Waislamu ambao walitekwa akili na hadithi za utumwa zisizokuwa na hata chembe moja ya uthibitisho. Angalau Mwanjisi alitahadharisha kuwa hadithi zake kuhusu ushenzi na mambo maovu kabisa ya Waarabu waliyowafanyiya Waafrika “hayana budi yathibitishwe kwa ushahidi kamili, na kuandikwa kwa makini.”
 
Akina Luteni Kanali Musa Maisara Kheri, mkuu wa uandishi na muandikaji wa utangulizi, Maalim Ubwa Mamboya Ismail, Mwenyekiti wa halmshauri ya uandishi wa kitabu cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania, 1964–1974, Zanzibar na ndugu zao wengine wa Kiislamu walioshiriki kwenye uandishi wa kitabu hicho, hawakuiyona haja wala madhara ya kuitumiya sumu ya hadithi zisizo na uthi-bitisho wowote midam sumu hiyo iliwapa uhai wenye utukufu wa kidunia. Mafunzo ya dini ya Kiislamu na ule msemo wa Imam Ali usemao “Utukufu hupatikana kwa kumtumikia Muumba na mwenye kuutafuta kwa viumbe hatoupata” haukuwa na maana yoyote kwao
 
Jambo la kupendeza lilikuwa kwamba mpaka mwaka 1974 kulikuwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Zanzibar. Zanzibar ikijilinda wenyewe. Mambo makubwa zaidi ni yale yenye kuwasononesha wale waliohusika katika kushiriki kuwauwa ndugu zao ambao leo wameshakuwa watu wazima na kesho kuna kukutana na Muumba wao. Kitabu hicho kiliandikwa chini ya uwenyekiti wa halmashauri ya uandishi wa kitabu chini ya uongozi wa Kanali Seif Bakari Omari, na Luteni Kanali Musa Maisara Kheri akiwa Mkuu wa Uandishi na muandikaji wa Utangulizi. Propaganda ya “misafara ya dhiki na dhuluma”
 
inasema:
Vikosi vya jeshi la wananchi wa Tanzania Zanzibar katika kazi yake ya siasa hufanya misafara kila mwaka mara mbili kwa kuvizuru vituo vyote ambamo wakiteswa Waafrika katika zama za utawala wa kifalme na vibaraka vyao ili kuelewa wanakotoka kwa makusudi ya kunyanyua juu nguvu za kimapigano na kuwa na chuki kwa matendo hayo waloyofanyiwa wafanyakazi na wakulima. Halmashauri ya siasa baada ya kukaa na kuzingatia ilitoa mpango maalumu kwa vikosi vyote kupita sehemu zote ambazo masalio ya baadhi ya vitu ambavyo Waafrika wakiteswa… Vituo hivyo ni:—
1. Mkunazini – U.M.C.A.
2. Tumekuja 3.
Maruhubi 4.
Kijichi 5.
Dunga jumba la mawe
 
BEIT – El AJAB
[Beit alajaib – jumba la maajabu] Hapo Forodhani Unguja lipo jumba kubwa la ghorofa tatu lililojengwa na mflame Baraghashi katika mwaka wa 1883 na mpaka hivi leo lipo bado. Ujenzi wa jumba hili ulipoteza roho chungu nzima za Waafrika wasio na hatia. Ilikuwa ni desturi kwa mujibu wa itikadi za kiarabu—kuchinja kinyama kama mbuzi, au ngombe ili awe kinga kwa kila baya. Watawala wa kiarabu badala ya kuchinja vinyama wao waliwachinja Binadamu badala yake! Dhulma ilioje!!!

Katika sehemu zote hizo zilizokwisha elezwa ndio sehemu muhimu kwa historia ya Waafrika walimoteswa na ndizo sehemu muhimu. Kwa hivi sasa zinazo pitiwa na wanajeshi na kufahamishwa hali ya tawala za kisultani na vibaraka vyao walivyo watesa kikatili Waafrika katika nchi hii. Ili kuwafanya wanajeshi wa kimapinduzi wawe na chuki kubwa mioyoni mwao kwa wapinga maendeleo ya kimapinduzi.
 
Mrengo wa Umoja wa Kiafrika—Pan-Africanism Kwa Zanzibar,
siasa ya Pan-Africanism au Pan-Arabism ni mfano wa globu za taa ambazo hazina budi kuzimika kwa sababu ni taa za siasa zenye kuumurika upande mmoja wa jamii na kuuwacha upande wa pili ndani ya giza. Zanzibar ni jamii ya mchanganyiko kwa hiyo mirengo ya kisiasa yenye kuiwacha nje nusu ya jamii na matokeo yake ni kuraruka kwa jamii ambayo ilitakiwa kwa pamoja ilikamate guo la kuwapamba na kuwasitiri.
 
Pan-Africanism kama alivyoichambuwa Dkt. Saleh Al-Miskry katika tasnifu yake ya shahada ya udaktari wa falsafa Pan-Africanism and Nyerere in Tanzania ni harakati yenye kuungwa mkono na kikundi cha watu na si na nguvu za umma. Sababu kubwa anayoitowa Al-Miskry ni ule ukaribu uliopo baina ya thakafa, dini, na mila baina ya viongozi wa Pan-Africanism na thakafa, dini, na mila za Ulaya. Anaendelea Al-Miskry, “…pan-Africanists na mabeberu kutoka Ulaya walifanya kazi kwa pamoja wakati wa ukombozi dhidi ya ukoloni.”
 
Hoja ya kibaguzi iliyotumika ni kuwa Waarabu kutoka kokote kule ni wageni Zanzibar na Mwambao wa Afrika Mashariki. Na si Waarabu peke yao, bali hata Washirazi pia. Ubaguzi huu unaonekana waziwazi katika barua ya Jumuiya ya Waafrika /African Association ya 1949 waliyomuwandikia Balozi wa Kiingereza Zanzibar na kwa Waziri wa Makoloni wa Uingereza isemayo:

Tunasikitika sana kuona kwamba Serikali imemteuwa Mshirazi, Mwasia kwa ajili ya kumtumiliya, badala ya Waafrika wa Zanzibar. Inaeleweka wazi kwamba Mshirazi ni Mwasia katika rekodi za Serikali ya Zanzibar. Tunaelewa kwamba tunanyimwa haki zetu za uraia na hii imewabakiza Waafrika katika hali ya kukata tamaa. Kwa jina la Demokrasi, Ukristo, na usawa wa Binadamu, tunapinga vikali hatua ya Serikali na tunaomba ufikirie na kutizama upya mwenendo huu wa ubaguzi, ukandamizaji, kunyimwa haki na kunyanyaswa katika nchi yetu
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…