Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

Mfanyabiashara katika Soko la Kitunda, Salama Hussein alisema yeye ni mmoja wa walioathirika na mkopo wa ‘kausha damu’ baada ya kukopa Sh200,000 ambayo riba yake ni Sh60,000 ndani ya mwezi mmoja.
 
Salama alisema kabla ya kupewa mkopo huo aliotakiwa kurejesha jumla ya Sh260,000, alinunua fomu ya kujiunga Sh10,000 na alitakiwa atoe Sh5,000 wakati alipotembelewa nyumbani kwake na maofisa wanaotoa mkopo ili waangalie vitu vya ndani vitakavyowekwa kama dhamana.
 
Alisema kutokana na shida aliyokuwa nayo alilazimika kuchukua Sh185,000 baada ya Sh15,000 kukatwa kwenye fomu na kutembelewa nyumbani.
 
Salama alisema kila siku alikuwa anarejesha Sh8,000, wakati mwingine alikuwa anakosa hela na kutakiwa kulipa faini ya Sh2,000 kwa siku ambayo hapeleki rejesho.
 
Kutokana na ugumu wa maisha, biashara yangu ilikufa kwa sababu mkopo niliochukua umerudi kwa walionikopesha, kila siku nilikuwa natoa Sh8,000 bado sijapigwa faini ya Sh2,000 nikikosa kurejesha,” alisema alisema Salama.
 
Kuna siku moja nilikuwa nalaza hadi siku tatu nalipa Sh6,000, kutokana na msingi wangu kuwa mdogo ulikufa, hela ya matumizi nayo nilikuwa nachukua kwenye biashara yangu.”
 
Mfanyabiashara wa Soko la Kigogo, Aisha Salehe alisema alikopa Sh50,000 kwenye taasisi moja ya kukopesha fedha kwa lengo la kuongezea mtaji katika biashara yake, lakini matokeo yake alichukuliwa godoro na sasa analala chini.
 
Aisha alisema aliambiwa atoe Sh5,000 kwa ajili ya fomu, Sh5,000 za kutembelewa na maofisa wanaotoa mkopo na amana ya mkopo alitoa Sh10,000.
 
Alisema riba aliyotakiwa kutoa ni Sh15,000, jumla ya fedha anazotakiwa kurejeshwa kwa mwezi Sh65,000 na kila siku alikuwa anatakiwa kutoa Sh2,200 kwa ajili ya rejesho.
 
“Ukichukua Sh200,000 lazima ulipe pamoja na riba, kila siku ‘kausha damu’ unatakiwa upeleke Sh4,300 na ukituma lazima utume na ya kutolea, usipotoa kwa siku moja faini yake ni Sh2,000 na hela yenyewe wanakupa Sh175,000 baada ya kukata fedha ya fomu, amana na wanapokutembelea nyumbani kwako
 
Aisha alisema kuna wengine wanachukua hadi Sh1 milioni, riba ya mkopo huo ni asilimia 30 nayo unalipa ndani ya mwezi mmoja, kila siku unatakiwa utoe Sh40,000 kama rejesho na usipotoa kwa siku faini yake ni Sh20,000.
 
Serikali ya mtaa yanena

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Pugu Bombani ambako baadhi ya wananchi wamelalamikia mikopo hiyo, Amanzi Bundala alisema ‘kausha damu’ katika mtaa wake vikundi vinavyokopesha vipo vingi na vimekuwa kero kwa wananchi wake.
 
“Mtu akichukua Sh50,000 kuna mambo mawili, la kwanza analipa kila siku Sh2,500 na ya pili wanatoka kwenye uhalisia wa biashara, kisha zinakuwa ngumu; hebu fikiria leo hii mtu akichukua Sh50,000 kwa ajili ya kujikwamua kibiashara haiendi kama alivyotarajia, matokeo yake vyote vinachukuliwa na huyo mkopeshaji,” alisema Bundala.
 
Hata hivyo, alisema amebaini wanaotoa mikopo hiyo baadhi yao hawana vibali, jambo ambalo ni tatizo kwa kuwa nchi inakosa mapato na Serikali ya mtaa huo hawapati chochote.
 
Machungu mengine ya mkopo huo yanasimuliwa na mkazi wa Tabata, Ibrahim Abdalla kwa kusema, “mimi nilikopa Sh500,000 kwa mtu binafsi na kila Sh100,000 riba ni Sh30,000 kwa mwezi, aise! Nilikuwa na shida, lakini maumivu yake ni makali sana.
 
Kutokana na riba kuwa kubwa, nilijikuta deni linafika zaidi ya Sh1 milioni, kuna nyakati nilishindwa kulipa mkopo na kubaki kulipa riba tu, kwa hiyo hii ni changamoto sana ya mikopo umiza,” alisema Abdalla.
 
Mkopaji, mkopeshaji nani tatizo?

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kutetea Haki za Wanawake (HDO), Prisca Ngaeshemi alisema wanaochukua mkopo wa ‘kausha damu’ ni wajasiriamali wa chini, wakiwamo mamalishe, wauza vitumbua na mbogamboga.
 
Prisca alisema wanawake hao wanapochukua mkopo urejeshaji wake ni shida, huku akitolea mfano anayechukua Sh200,000 kila siku anatakiwa atoe Sh8,000, “biashara gani inayomfanya apate faida ya kupata hela hiyo.”

Alisema matokeo yake mtaji unakufa kwa sababu hela hiyo hiyo inampasa atoe ya matumizi ya nyumbani na nyingine kwa jili ya marejesho ya kila siku.

Hata hivyo, Wakili John Seka alipoulizwa kuhusu utendaji wa kampuni hizo, alisema kuna faida ya kila mkopo, huku akieleza wanaokopa huko na kutatua shida zao, ndiyo wanajua umuhimu wake na huenda tatizo likawa ni wateja.
 
Alisema kabla ya kuangalia uvunjaji wa sheria ni vyema kuangalia hatari kiasi gani wanabeba watu hawa wanaokopesha mikopo hiyo.

“Licha ya mikopo yao kutoka ndani ya muda mfupi, lakini (mkopaji) hana uhakika kama wanatumia muda wa kutosha kufanya ufuatiliaji wa mtu wanayemkopesha kama inavyofanywa na benki,”alisema wakili huyo.

“Benki ukiomba mkopo watakufanyia ufuatiliaji wa vitu vingi ili kujiridhisha kuwa wanayekwenda kumpa mkopo wao atarudisha, lakini hawa wanaweza kukupatia mkopo kwa kutumia kadi ya gari, hawakagui gari ni nzima kiasi gani kama inaweza warudishia pesa zao ila wanakuamini.”
 
Madalali wafunguka

Potess Moshi kutoka Mem Auctionineer and General Broker Limited alisema kuna tatizo la watu wanaochukua mikopo kutojua wanaenda kufanya nini na kama walikuwa na wazo, tayari hubadilika baada ya kupata fedha.

“Mtu anachukua mkopo anafanya rejesho moja halafu haonekani, sasa hatujui kama ni kwa sababu ya riba kubwa au biashara kuanguka,” alisema Moshi.

Alisema wengine hadi wanapewa mkopo wanakuwa na hela pungufu tofauti na iliyopo kwenye fomu kwa sababu wanatoa rushwa ili waonekane wana vigezo
 
Back
Top Bottom