Genius "Ginimbi" Kadungure na
Wicknell Chivhayo wanatajwa kwa pamoja kwa sababu ya historia yao kama matajiri vijana na maarufu zaidi nchini Zimbabwe.
Wawili hawa walikuwa na maisha ya kifahari yaliyovuta hisia za wengi, ushindani mkubwa wa hadharani, kesi za kisheria walizoshirikiana, na mwisho wa maisha yao uliogubikwa na
vifo vya ghafla na vya kusikitisha.
Leo kumekuwa na taarifa za kusikitisha kwamba Wicknell Chivhayo na mkewe wamepoteza maisha katika ajali ya helikopta huko Marondera, jambo ambalo limefanya umma ulinganishe kifo chake na kifo cha Ginimbi cha mwaka 2020 kilichotokana na ajali ya gari aina ya Rolls-Royce.
Sababu kubwa inayofanya majina haya mawili yafungamanishe ni
vifo vyao vya ghafla na vya kiwewe.
Ginimbi alifariki akiwa na umri wa miaka 36 mnamo Novemba 8, 2020, baada ya gari lake la kifahari kugongana uso kwa uso na gari jingine na kuwaka moto jijini Harare.
Kwa upande mwingine, kifo cha Wicknell Chivhayo pamoja na mkewe Lucy Muteke kwenye ajali ya helikopta kimeacha mshtuko mkubwa nchini Zimbabwe, kikiwakumbusha watu jinsi nchi hiyo ilivyopoteza matajiri wake wawili vijana na wenye ushawishi mkubwa katika matukio ya ajali.
Mbali na vifo vyao, wawili hawa walikuwa na
historia ya kisheria na kashfa za kifedha zilizowaweka pamoja.
Walishawahi kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa pamoja wakituhumiwa kushirikiana katika utapeli mkubwa wa zaidi ya dola milioni 1 uliotokea mwaka 2012, ambapo walidaiwa kutumia makampuni feki ya Afrika Kusini kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Wakati wa kesi hizo, uhusiano wao uliingia mivurugano mikubwa huku Ginimbi akijaribu kujinasua mahakamani kwa kutupa lawama zote kwa
Chivhayo.
Uhusiano wao pia ulitawaliwa na
ushindani mkubwa wa kuringishia utajiri kwenye mitandao ya kijamii.
Kabla ya kifo cha Ginimbi, wawili hao walikuwa wakiviziana na kurushiana vijembe mtandaoni kuhusu nani mwenye ukwasi mkubwa zaidi, nani anamiliki magari ya bei ghali zaidi kama vile Lamborghini, Bentley, na Rolls-Royce, na nani anatumia fedha nyingi zaidi kwenye starehe.
Wakati Ginimbi alijulikana kwa kuandaa sherehe za kifahari za nguo nyeupe ("All-White Parties"), Chivhayo alijulikana kwa mtindo wake wa kutoa misaada mikubwa ya magari na fedha taslimu, huku wote wawili wakikosolewa mara kwa mara kuhusu chanzo cha utajiri wao.