Mara ya kwanza kusafiri nilikuwa naenda Sehemu hivi kupitia Paris. Ila siku hiyo ndege ya Air France ikawa imeharibika na hivyo ikaja ndege ya Madagascar Airlines Boeng 747, mzinga wa pipa.
Uzuri ni kuwa nilipigwa shule nyumbani nzuri sana jinsi ya kufunga mkanda, kulaza kiti na kukirudisha, kufungua headphones na kuzitumia na wapi zipo tundu za kuchomeka.
Ila nakaa, pembeni kuna Dada wa Kiganda na Mudhungu wake, akawa anahangaika jinsi ya kufunga, bwana wake akamsaidia kufunga. Sijui siku hizi anajisikiaje akikumbuka ushamba huo wa siku ya kwanza.
Kasheshe ilikuwa wakati wa kula. Ila Mungu bariki nilishaambiwa kuwa kuna vikaratasi vya kufuta uso na asubuhi mnaletewa taulo za motomoto kufuta uso pia. Msosi kufika, maajabu matupu kwani nusu ya vyakula navifahamu na nusu sivifahamu. Mie na kundi langu lote tukawa tumekubaliana tutakula kila kitu na hatubakizi hata kama watakuwa CHURA wa Kifaransa maana hawa jamaa WALA VYURA hawakawii kumlisha mtu nyama zao.
Kila kitu kilienda safi ila ikawa kasheshe kuzila OLIVE ila nikajikaza nikazila. Kulikuwa na nyama nyeusi nyeusi, sikujali ni nini, nikazila bila huruma. Mwisho vikabaki vipaketi vitatu. Kimoja kukifungua ni Sukari, nikaibugia. Kingine kufungua ni jibni, nikaila bila huruma. Cha mwisho kufungua (nilikuwa nafahamu unafungua kwa kuvunja ncha iliyochomoza) ikawa kumbe maziwa ya kwenye kahawa ambayo nilishaimaliza mapema sana bila sukari wala maziwa. Basi nikaangalia kushoto kulia hakuna anayeangalia, nikabugia. Mwisho nikasema hata kama Mjinga fulani kaniona, sijali maana hatakuja kuniona tena. Mwisho sahamu yote ikawa tupu na wakaja akina dada kuchukua makasha matupu.
Kuna jamaa alikuwa anawasumbua akina dada kuagiza pombe basi ilipofika saa 9 usiku, wakamuita na kumuonyesha Friji la Pombe lilipo na wakaenda kulala. Jamaa alipofika Paris, alikuwa anatambaa kutoka ndani ya ndege.