Cha muhimu ni kuwa Waziri mwenye dhamana na afya ya Watanzania leo amewataka Watanzania wote kuchukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa huu kama wanavyopatiwa taarifa na elimu mara kwa mara kupitia njia mbali mbali. Aidha, kwa kuzingatia Kanuni ya 46 ya Sheria ya Afya ya Jamii, 2012 (Reg. 46 of the Public Health Regulation (Sanitisation and Hygiene Practices), 2012); waziri wa afya leo kaelekeza mambo yafuatayo:-
I. Watanzania wasiokuwa na safari za lazima, wanashauriwa kwa sasa kusitisha safari zao kwenye nchi zenye maambukizi
2. Amezitaka Taasisi zote zikiwemo Shule, Hoteli, Maduka ya Biashara, Nyumba za Kulala Wageni (Lodges/Guest Houses), Makanisa, Misikiti, Ofisi za Umma na za Binafsi, Vituo vya kutolea Huduma za Afya, taasisi za fedha, vyombo vya Usafiri, pamoja na maeneo ya mikusanyiko ya watu kama vile masoko, viwanja vya mpira, na vituo vya abiria kuweka vifaa vya kunawia mikono kwa maji tiririka na sabuni au maji yenye Klorini kwa ajili ya kuhakikisha usafi wa mikono. Aidha kwa kadri itakavyowezekana, maeneo hayo yawekewe vifaa maalum vya kuwekea vitakasa mikono (Sanitizer Dispensers)
3. Kuweka maji yenye dawa ya Klorini au vitakasa mikono (hand sanitizers) katika mageti ya kuingilia hifadhini au mahotelini kwa ajili ya kusafisha mikono ya watalii na waongoza watalii wote.
4. Kuweka maji yenye dawa ya Klorini katika Vituo vya Mabasi ya abiria na Mwendokasi kwa ajili ya kusafisha mikono ya wasafiri.
5. Kuepuka kusalimiana kwa kushikana mikono, kukumbatiana, kugusa pua, mdomo pamoja na macho kadri itakavyowezekana.
6. Hospitali zetu amezitaka zihakikishe kuwa ndugu/jamaa wanaokwenda kuona wagonjwa waliolazwa idadi yao isizidi wawili kwa kila mmgonjwa
7. Kutoa taarifa kwenye Ofisi za Afya au Vituo vya Kutolea Huduma za Afya endapo watamwona mtu mwenye dalili za ugonjwa wa COVID- 19
Imetolewa na: Ummy Mwalimu,Mb.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Dar es Salaam.