WALIVYOFUNGUA GETI LA KUJINUFAISHA KWA TAKRIMA, RUSHWA, KINGA MAALUMU N.K
Sasa tunaelewa kwanini waliondoa baadhi ya vifungu hivi na pia kutunga sheria za kujikinga wakati wakiwa madarakani
Ibara 28 za Tume ya Warioba zilizoondolewa
updated on Machi 11, 2021
Jaji Warioba.PICHA|MAKTABA
Muktasari:
- Ibara ya 15 iliyokuwamo katika Rasimu ya Warioba ilisema: “Kiongozi wa umma wakati anapotekeleza shughuli za kiserikali, akipewa zawadi, zawadi hiyo itakuwa ni mali ya Jamhuri ya Muungano na ilitaka Bunge kutunga sheria itakayosimamia, pamoja na mambo mengine, thamani, kiwango, aina na uhifadhi wa zawadi kwa Jamhuri ya Muungano. Mbali na ibara hiyo, pia Ibara ya 16 iliyohusu ufunguaji akaunti nje ya nchi, imeondolewa.
Dar/Dodoma.
Rasimu ya Katiba inayopendekezwa iliyowasilishwa bungeni juzi,
imeondoa Ibara
28 zikiwamo zinazowataka viongozi wa umma kutopokea zawadi kwa manufaa yao binafsi wala kufungua akaunti ya benki nje ya nchi pasipo sababu maalumu, Mwananchi limebaini.
Ibara ya 15 iliyokuwamo katika Rasimu ya Warioba ilisema: “Kiongozi wa umma wakati anapotekeleza shughuli za kiserikali, akipewa zawadi, zawadi hiyo itakuwa ni mali ya Jamhuri ya Muungano na ilitaka Bunge kutunga sheria itakayosimamia, pamoja na mambo mengine, thamani, kiwango, aina na uhifadhi wa zawadi kwa Jamhuri ya Muungano.
Mbali na ibara hiyo, pia Ibara ya 16 iliyohusu ufunguaji akaunti nje ya nchi, imeondolewa.
Ibara nyingine zilizo ondolewa ni pamoja na ya 17 iliyopendekeza uwazi wa mali ikimtaka kiongozi wa umma kutangaza thamani ya mali na madeni yake mara tu baada ya kupata uongozi.
Pia
Ibara ya 129 iliyokuwa inawaruhusu wananchi kumvua madaraka mbunge ambaye atashindwa kuwasilisha au kutetea kwa dhati hoja zinazotokana na kero za wapigakura wake au ataacha kuishi au kuhamisha makazi yake kutoka eneo la jimbo la uchaguzi kwa zaidi ya miezi sita bila sababu za msingi imeondolewa.
Ibara 28 zilizoondolewa
15. (1) Kiongozi wa umma wakati anapotekeleza shughuli za kiserikali, akipewa zawadi, itakuwa ni mali ya Jamhuri ya Muungano na ataiwasilisha kwa Katibu Mkuu Kiongozi kupitia kwa katibu mkuu wa wizara au kiongozi wa taasisi ya Serikali inayohusika, akiainisha:
(a) aina ya zawadi;
(b) thamani ya zawadi;
(c) sababu ya kupewa zawadi; na
(d) mtu au mamlaka iliyotoa zawadi hiyo.
(2) Neno “zawadi” kama lilivyotumika katika ibara hii linajumuisha kitu chochote chenye thamani atakacho pewa kiongozi wa umma katika utekelezaji wa shughuli za umma.
(3) Bunge litatunga sheria itakayosimamia, pamoja na mambo mengine, thamani, kiwango, aina na uhifadhi wa zawadi kwa Jamhuri ya Muungano.
16. Kiongozi wa umma-
(a) Hatafungua au kumiliki akaunti ya benki nje ya Jamhuri ya Muungano isipokuwa tu kwa namna ambayo sheria za nchi zinaruhusu; na
(b) hataomba au kupokea mkopo au faida yoyote kwa namna au mazingira ambayo yanashusha hadhi au heshima ya utumishi wa umma.
17.-(1) Kiongozi wa umma atalazimika kutangaza na kuwasilisha, ndani ya siku thelathini baada ya kupata uongozi na baada ya kuacha uongozi, mali na thamani yake na madeni yake katika Tume ya Maadili ya Uongozi na Uwajibikaji.
(2) Bila ya kuathiri masharti ya ibara ndogo ya
(1), Kiongozi wa umma atalazimika kutangaza na kuwasilisha taarifa ya mali na madeni:
(a) yake binafsi;
(b) ya mwenza wake wa ndoa; na
(c) ya watoto wake walio chini ya umri wa miaka kumi na nane, mara moja kila mwaka kwa Tume ya Maadili ya Uongozi na Uwajibikaji.
(3) Bunge litatunga sheria itakayosimamia, pamoja na mambo mengine:
(a) ngazi au orodha ya viongozi wa umma wanaopaswa kutangaza mali na madeni yao; na
(b) utaratibu wa kuwasilisha taarifa ya mali na madeni kwa Tume ya Maadili ya Uongozi na Uwajibikaji kwa mujibu wa Katiba hii.
18.-(1) Kiongozi wa umma hatashiriki katika kufanya uamuzi wa jambo au shughuli yoyote ambayo ana masilahi nayo yeye binafsi, mwenza wake, mtoto wake, jamaa yake, rafiki au mtu yeyote wa karibu.
(2) Kiongozi wa umma hatazungumzia kitu chochote katika Baraza la Mawaziri, Bunge, Kamati au chombo kingine chochote rasmi ambacho ana masilahi nacho ya moja kwa moja au vinginevyo, isipokuwa tu kama atatoa taarifa ya mgongano huo wa masilahi katika chombo hicho.
(3) Itakuwa ni marufuku kwa kiongozi wa umma kushiriki katika uamuzi unaohusu kuongeza au kuboresha masilahi kwa namna yoyote ile yanayohusu wadhifa alionao na endapo atashiriki, basi masharti hayo mapya yataanza kutumika kwa kiongozi wa umma atakayekuja baada ya kiongozi husika kuondoka au kumaliza muda wa kukaa katika nafasi ya madaraka iliyompatia fursa ya kushiriki katika kuamua masilahi husika.
(4) Masharti ya ibara ndogo ya
(3), hayatamhusu kiongozi wa umma ambaye kutokana na asili ya nafasi ya madaraka au aina ya kazi zake anapaswa kushiriki katika upangaji wa mishahara au maslahi mengine ya watumishi wa umma.
(5) Kiongozi wa umma hataruhusiwa kushika nafasi za madaraka zaidi ya moja au kutumikia mihimili ya dola zaidi ya mmoja kwa wakati mmoja.
19. Kiongozi wa umma hataruhusiwa kutumia au kuruhusu kutumika kwa mali yoyote ya umma, zikiwemo zilizokodishwa kwa Serikali, kwa madhumuni ya kujipatia yeye binafsi au kumpatia mtu mwingine manufaa yoyote.
20.-(1) Bunge litatunga sheria itakayosimamia, pamoja na mambo mengine:
(a) utaratibu wa utwaaji wa mali za viongozi wa umma zilizopatikana kwa kukiuka sheria;
(b) utaratibu wa kumwajibisha kiongozi wa umma aliyekiuka maadili na Miiko ya Uongozi; na
(c) uanzishaji wa mitalaa inayohusu Katiba, maadili na uraia, shuleni na vyuoni.
(2) Masharti yaliyoainishwa katika sehemu hii ya Sura ya Tatu yatatumika pia kwa watumishi wa umma baada ya kufanyiwa marekebisho stahiki.
63. Kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano na kwa ajili ya mgawanyo wa madaraka juu ya shughuli hizo baina ya vyombo vilivyotajwa katika Ibara ya 61, Serikali ya Jamhuri ya Muungano itakuwa na mamlaka juu ya mambo ya Muungano kama yalivyoorodheshwa katika Nyongeza ya Katiba hii. Nchi Washirika.
Source : gazeti la mwananchi