Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa amewasilisha hoja kwa mkutano mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa Mwenyeiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan awe mgombea urais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Pia, Kimbisa amesema Makamu Mwenyekiti Zanzibar wa CCM, Dk Hussein Mwinyi awe mgombea urais wa Zanzibar.
Baada ya kutoa hoja hiyo leo Jumapili, Januari 19, 2025 katika kikao hicho kinachoongozwa na Rais Samia, wajumbe wote wa mkutano huo wakasimama kushangilia na kuunga mkono hoja hiyo.
Hoja kama hiyo imetolewa wakati wajumbe wa mkutano huo wakichangia taarifa za utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/25 kwa upande wa Zanzibar na Tanzania Bara.
Hoja za wachangiaji wote zinaeleza kuwa ni kutokana na ubora na ufanisi wa utekelezaji wa ilani wakisema hakuna mbadala wa wawili hao kuwania Urais.
Kikwete Azungumza na Wajumbe Kuhusu Rais Samia Kugombea Urais 2025
"Azimio liwe Rais Samia amechaguliwa kuwa mgombea Rais wa CCM 2025"
Rais mstaafu na Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Jakaya Kikwete, alilazimika kutoa busara zake baada ya wajumbe wa mkutano mkuu maalum wa CCM kutaka kuanzisha mjadala kuhusu wagombea wa urais katika Uchaguzi Mkuu ujao kupitia chama hicho.
Katika kikao hicho, ilikubalika kuwa Rais Samia Suluhu Hassan atakuwa mgombea urais wa CCM kwa uchaguzi wa 2025, huku Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, pia akijitokeza kama mgombea mwenye nguvu.