Mbunge adai Mke wa Rais Mstaafu Tanzania anawaibia walimu
Na Muhibu Said, Dodoma
Mwananchi
WAKATI tuhuma dhidi ya Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa na mkewe Anna, kwamba walijihusisha na biashara wakiwa Ikulu zikiwa hazijatolewa maelezo ya kina hadi leo, Anna anakabiliwa na tuhuma mpya kwamba amekuwa akishiriki katika mikataba ya kilaghai ya kuwaibia walimu.
Tuhuma hizi mpya dhidi ya Anna zimetolewa na Mbunge wa Mbozi Mashariki (CCM), Godfrey Zambi, wakati wa majadala wa kupitisha makadirio ya matumizi ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa mwaka wa fedha wa 2008/09 bungeni juzi jioni.
Pamoja na Anna, pia Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Ibrahim Kaduma, naye aliingizwa kwenye tuhuma hizo wakidaiwa kuwaibia walimu mamilioni ya shilingi kupitia kampuni yao ya kutoa mikopo.
Mbunge huyo alidai kuwa Kampuni ya Bayport Financial Services, ambayo inajishughulisha na utoaji wa mikopo kwa watumishi wa umma, inamilikiwa na Anna na baadhi ya vigogo wastaafu serikalini, akiwamo Kaduma, imekuwa ikiwakopesha walimu Sh1milioni, huku ikiwataka walipe Sh3milioni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kampuni ya Bayport inamilikiwa na mke wa Rais Mstaafu, Anna Mkapa. Lakini wapo wengine wazito walioitumikia nchi hii, kama Kaduma. Mwalimu akikopa Sh1milioni analipa Sh3milioni. Hii imetoka wapi kama si wizi??alihoji Zambi bila kueleza muda wa ulipaji wa mkopo ulitolewa na kampuni hiyo.
Akijibu hoja hiyo ya Zambi, Waziri Profesa Jumanne Maghembe, alisema kiwango cha ulipaji mkopo kinategemea muda wa kulipa, kauli ambayo ilisababisha karibu ukumbi mzima wa Bunge kuzomea, kuashiria kwamba wabunge hawajaridhishwa na majibu hayo.
Hata hivyo, Waziri Maghembe alijibu tuhuma hizo akisema: "Kama mkopo huo ni wa muda mfupi, hiyo riba ni kubwa. Hata hivyo, nawaahidi kwamba suala hilo tutalifuatilia ili kupata ukweli wake."
Pia Waziri Magheme alitoa hadhari kwa walimu kuwa makini wanapoingia katika mikataba mbalimbali hasa ya kukopa.
Baada ya Bunge kuahisishwa, mwandishi wa Mwananchi alimuomba Zambi ampe ufafanuzi juu ya mikopo hiyo na muda wa kurejesha.
Alidai kwamba, kwa mujibu wa nyaraka alizonazo, mkopo huo unatakiwa ulipwe katika kipindi cha miaka mitatu, ambayo ni sawa na asilimia 67 ya riba inayotozwa kwa mwaka na alidai kuwa kampuni hiyo haijaweka bayana riba ambayo mkopaji anatakiwa atozwe.
Mbunge huyo alidai kuwa kiasi hicho cha fedha, ambacho kinatakiwa kilipwe, ni zaidi ya asilimia 200 ya malipo na riba inayotozwa kutokana na mkopo huo.
Alidai kuwa kwa mujibu wa nyaraka hizo, kampuni hiyo ilipewa kibali cha kuendesha shughuli zake na Ikulu, lakini ndani ya kibali hicho ambacho ndani yake kuna maelezo yanayeosema kuwa lolote litakalotokea katika biashara hiyo, litamalizwa na kampuni na mteja wake.
"Kampuni hiyo inakopesha watumishi wa umma. Walioingia kwenye mtego huo ni walimu. Na walimu ndio walionipa taarifa hizo. Hivi sasa huko Mbeya kuna crisis (mgogoro) kubwa," alisema Zambi.
Tuhuma hizo zimetolewa na Zambi siku chache baada ya asilimia kubwa ya wabunge kuibana serikali kuitaka iboreshe kipato cha walimu kinachotokana na mishahara yao.
Mwananchi jana ilifika katika ofisi za Bayport kwa nia ya kupata ufafanuzi juu ya tuhuma zilizoelekezwa kwake na mbunge huyo, hata hivyo mwandishi wetu baada ya kusubiri kwa saa kadhaa kwenye ofisi hizo jengo la Water Front jijini Dar es Saam, alipewa mihadi ya kukutana na msemaji wa kampuni hiyo leo.
Tuhuma hizi mpya dhidi ya Mama Mkapa zinatolewa huku kukiwa na mlolongo mrefu wa tuhuma dhidi yake, zikiwamo za kufungua kampuni ya ANBEM yeye na mumewe, Rais Mkapa wakiwa Ikulu na kujihusisha na biashara.
Akiwa kijijini kwake Lupaso, Mtwara, Rais Mkapa aliwataka wananchi kupuuza tuhuma zinazotolewa dhidi yake kwa madia kwamba ni za uongo. Hakufafanua ni tuhuma ipi ni ya uongo na ipi ni ya kweli.