Date::7/17/2008
Anna Mkapa ana hisa chache katika kampuni ya Bayport
Na James Magai
WAKATI Kampuni ya Bayport Financial Services imethibitisha kwamba viwango vya riba wanazokata wateja wanaokopa fedha ni kikubwa zaidi ya kinachokatwa na mabenki nchini, pia imeeleza kwamba Mama Anna Mkapa ana hisa kwenye kampuni hiyo.
Meneja wa Tawi la Bayport nchini, Robert Washokera, akizungumza na Mwananchi jana, alisema kwamba ingawa viwango vyao viko juu lakini havizidi asilimia 50 kama serikali ilivyoagiza.
Alisema wanatoza viwango hivyo tofauti na benki kwa kuwa wao hawana ankaunti yoyote na wateja kama ilivyo kwa benki, ambapo kutokana na wateja kuwa na ankauti katika benki hizo kuna makato ambayo benki zinapata zikiwezo gharama za huduma mbali ya kiwango cha riba kwa mkopo.
Hata hivyo, Washokera alipotakiwa kutaja viwango vya riba wanavyotoza, hakuwa tayari kwa madai kwamba si vema kibiashara kutaja viwango hivyo kwenye vyombo vya habari.
''Unajua biashara ni ushindani, sasa si vema kutaja viwango hivyo kwenye media (vyombo vya habari) kwa sababu ni sawa na kumpa adui yako mbinu unazotumia. Lakini kama nilivyosema viwango vyetu haviko nje na tamko la serikali na mtu yeyote akija tunampa na yeye ndiye anachagua kiwango atakachoridhika nacho,'' alisisitiza Washokera.
Kadhalika, msemaji huyo alisema kwamba madai yaliyotolewa na Mbunge wa Mbozi Mashariki (CCM), Godfrey Zambi bungeni wiki hii kwamba Mama Anna Mkapa ndiye mmiliki wa kampuni hiyo si sahihi, kwa sababu anamiliki kiwango kidogo cha hisa.
''Mama Anna Mkapa na Kaduma si wamiliki wa kampuni hii bali wao ni wanahisa tu. Wao ni miongomi mwa Wakurugenzi tu kwa sababu wamenunua hisa katika kampuni hii na hisa zao ni ndogo mno,'' alisema Washokera.
Washokera alisema ingawa Mama Anna Mkapa na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Ibrahim Kaduma ni miongoni wa Wakurugenzi wa kampuni hiyo kutokana na kuwa na hisa, hawahusiki na wala hawajui shughuli zozote za utoaji mikopo katika kampuni hiyo.
?Wao ni sawa mtu yeyote aliyenunua hisa TBL (Kampuni ya Bia nchini), yeye anachojua ni gawio lake tu kwa hiyo haiwezekani TBL ikiuza mazao yenye hitilafu, umtaje huyu mwenye hisa mmoja tu kuwa ndiye anahusika,? alisema Washokera.
Maelezo ya Washokera yanafuatia kauli ya Zambi bungeni wakati wa mjadala wa kupitisha makadirio ya matumizi ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwamba Bayport inayomilikiwa na Mama Mkapa na Kaduma, inawaibia walimu kwa kukata fedha nyingi kutokana na mikopo kidogo.
''Kuna kampuni ya Bayport inamilikiwa na mke wa Rais Mstaafu, Anna Mkapa. Lakini wapo wengine wazito walioitumikia nchi hii, kama Kaduma. Mwalimu akikopa Sh1 milioni analipa Sh3milioni. Hii imetoka wapi kama si wizi?'' alihoji Zambi bila kueleza muda wa ulipaji wa mkopo ulitolewa na kampuni hiyo.
Washokera alidai kwamba kauli ya mbunge huyo kuwa Mama Anna ndiye mmiliki wa kampuni hiyo ililenga kumchafua jina pengine kutokana na baadhi ya tuhuma ambazo zimewahi kuibuliwa zikimuhusisha na mumewe, Rais Mstaafu Benjamini Mkapa.
''Kama alipata taarifa hizi kwa wananchi wake, hatujui ni kwa nini yeye alishindwa kuwahoji zaidi ili wampe taarifa za kina na sahihi. Lakini pia tunashangaa ni kwa nini alishindwa kwenda walau halmashauri tu akapata historia ya kampuni maana huko kuna nyaraka zinaonyesha na majina ya wakurugenzi wote,'' alihoji Washokera.
Washokera pia alisema kampuni hiyo ambayo imeanza kufanya shughuli zake hapa nchini mwaka 2006 ni ya Afrika Kusini na kwamba kwa sasa ina matawi katika nchi tano katika Afrika.
Alizitaja nchi hizo mbali na Afrika Kusini kwenye makao makuu kuwa ni Tanzania, Uganda, Ghana, Zambia na Mauritius.
Kuhusu tuhuma za kuwaibia wateja wao, Washokera alisema madai hayo hayana msingi kwa kuwa kampuni hiyo inaendesha shughuli zake kwa taratibu za wazi na kwa mujibu wa kanuni na taratibu za nchi.
Alisema kila mtu anayehitaji mkopo kwanza huelezwa masharti na taratibu za mikopo ikiwa ni pamoja na kiwango cha makato na riba na muda wa kurejesha mkopo, ambao huanzia mwezi mmoja hadi miaka mitano na iwapo ataridhika ndipo anapewa fomu ambazo atazijaza na kisha kusaini.
Alisema kiwango cha makato hutegemeana na muda wa kurejesha mkopo na kwamba ikiwa kipindi cha kurejesha mkopo ni kirefu basi kiwango cha makato kinakuwa ni kidogo, lakini riba yake inakuwa ni kubwa kidogo tofauti na mkopo unaorejeshwa katika kipindi cha muda mfupi ambapo kiwango cha makato huwa kikubwa, lakini riba yake inakuwa ni ndogo.
Akizungumzia madai ya kuwakata viwango vikubwa wateja wao, Washokera alisema malalamiko hayo yamekuwapo na wamekuwa wakiyapokea ofisini kwao kutoka kwa wateja, lakini akasema kuwa hayo yamekuwa yakitolewa na baadhi ya wateja ambao mwisho wa mwezi kujikuta hawana salio baada ya makato.
''Hii inatokea kwa sababu kuna watu wengine ambao wamekopa sehemu mbalimbali sasa inapofika mwisho wa mwezi wanajikuta hawana kitu ndio wanakuja hapa na kuanza kulalamika kuwa tunawakata viwango vikubwa licha ya kwamba walikubaliana na viwango vyetu,'' alisema Washokera na kuongeza:
''Kuna mama mmoja alikuja hapa akiwa ana shida ya shule ya mtoto, tulipoangalia akiba yake alikuwa habaki na kitu, kumbe alikuwa amekopa katika taasisi tatu tofauti, ikiwemo NMB, Baclays na Nufaika.''
Alisisitiza kuwa hadi sasa wamekwishatoa mikopo kwa watumishi wengi wakiwemo wafanyakazi wa wizara mbalimbali ikiwemo Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na katika manispaa nyingi lakini hawajawahi kusikia malalamiko yoyote kutoka kwao.
Alisema kabla mteja hajapewa mkopo kuna fomu ambazo anazijaza baada ya kuzisoma na kukubaliana na masharti na taratibu zao.
''Haiwezi kuingia akilini kuwa mtu amesaini kitu asichokielewa kwani kuna mambo ya msingi ambayo kwanza mteja inabidi ayaelewe. Anapaswa kufahamu kiasi cha mkopo muda wa kurudisha mkopo, kiwango cha riba atakachokatwa,'' alisema.
?Wapo wengine ambao wameomba kuongeza (mkopo) hata kabla hawajamaliza kulipa mkopo wa kwanza na wale ambao ulipaji wao hauna matatizo tunawakubalia.
''Hivi juzi kuna wengine nao walikuja hapa kutoka Kilwa wakiwa na mbunge wao wa zamani wakilalamika kuwa tunawakata kiwango kikubwa, lakini tulipokaa nao na kuwaeleza matokeo yake ni kwamba wote waliomba kuongeza mkopo na mbunge wao huyo akabaki anashangaa.''
''Kuna mteja mwingine kutoka Kibaha alifika ofisini kwetu kulalamika kuwa tunamkata kiwango kikubwa kiasi kwamba habaki na kitu. Baada ya kugundua kuwa tatizo lake ni kwamba alikuwa habakii na akiba yoyote tulimpa njia za kumsaidia na tukamtaka achague, matokeo yake alichagua kuongeza mkopo tena na tukampa Sh600,000 kwa kiwango kile kile cha makato,'' alisema Washokera.
Alisema kuna watumishi wengine wanakuwa wakiomba mkopo na kuomba wakatwe hata zaidi ya nusu ya mshahara wao kwa mwezi, lakini wamekuwa wakikataa kwa kuwa hilo ni nje ya utaratibu wa serikali na badala yake wanajaribu kuwapa ushauri mwingine namna ya kufanya.
"Kuna mama mmoja alikuja hapa akihitaji mkopo lakini tulipoangalia 'balance' yake ilikuwa ni sifuri, alikuwa amechukua mkopo NMB, Barclays na Nufaika,'' alisema Washokera na kuongeza:
''Kwa kuwa alilia sana tulichokifanya ni kuangalia ni wapi alikuwa anakaribia kumaliza deni hivyo tulikwenda NMB wakatuthibitishia kuwa alikuwa anatarajia kumaliza deni mwezi uliokuwa unafuata, hivyo tulikubali tukampa mkopo wa jinsi hii wapo wengi wanaokuja hapa.''
Washokera alisema kwa sasa kampuni hiyo ina matawi manne jijini Dar es Salaam na mikoani hadi sasa wana matawi tisa na kwamba kwa hali hiyo jinsi walivyojizatiti si rahisi kufanya upateli kama huo.
Tuma maoni kwa Mhariri