WAJINA WANGU "Robert Amsterdam" USITUTISHE
Na, Robert Heriel
Kuna watu wapuuzi wanafikiri nchi hii itaogopa mtu yeyote atakaye bana maslahi ya taifa hili na watu wake. Tanzania ni nchi huru, ina watu wake na mali zake, ina utamaduni wake na sheria zake. Mtu yeyote bila kujali nafasi yake atakayedhani anaweza kuharibu nchi hii atatoboka mapema kabla hajafanikiwa.
Wajina wangu Robert Amsterdam ambaye nimemfahamu baada ya mteja wake, Tundu Lisu kurudi hapa nchini. Sikuwahi kumfahamu Wajina wangu Robert Amsterdam hapo kabla. Ninafuraha kumjua ';Bob' Mwenzangu, kwani nafahamu watu wenye majina ya Robert jinsi tulivyowatulivu, wapenda haki, werevu na wenye busara.
Robert Amsterdam ni Mwanasheria wa Kimataifa mwenye asili ya Kikanada ambaye amebobea katika fani ya sheria, na kujikita katika sheria za Kimataifa za umma(public international law), sheria za jinai ya Kimataifa(international criminal law), na Utetezi wa mambo ya kisiasa(political advocacy) Kutokana na umashuhuri wake na kushinda kesi nyingi za kimataifa anakampuni ya sheria iitwayo "Amsterdam & Partners LLP" Yenye Ofisi zake katika jiji la London, Uingereza na Washington Dc, Marekani.
Wajina wangu 'Bob' nakupongeza kwa kumtetea Ndugu yetu Tundu Lisu. Tunajua upo katika majukumu yako ya kazi. Lakini majukumu yako yasizidi mipaka na kuingilia mambo yasiyokuhusu.
Wajina wangu 'Bob' katika chaguzi zozote zinazofanyika hapa nchini kwetu kuna mambo ya msingi ambayo kama Watanzania tunayazingatia kuliko kitu chochote. Mambo hayo yanaweza kuwa yapo kisheria au yasiwepo kisheria, lakini itoshe kusema yapo;
Nitagusia machache kwa upendeleo kwa sababu wewe ni wajina wangu;
1. Amani ya nchi yetu
Watanzania ni watu wapendao amani, na hapa nimedhamiria kuzungumzia amani ya kutokuwa na vita, vurugu, kadhia, maandamano yenye mauaji, majeraha, uharibifu wa mali n.k.
Pengine tukawa hatuna amani ya kukosa mali, chakula na pesa. Lakini tunaamini amani ya kwanza ni kutokuwa na vita na matumizi ya mabavu.
2. Kulinda Muungano
Wajina wangu Bob, najua wafahamui nchi yetu ni muunganiko wa nchi mbili ambazo ni Tanganyika na Zanzibar na kuunda taifa la Tanzania. Hatupendi mtu ambaye tuna mashaka naye, ambaye atashindwa kulinda muungano. Mtu yeyote mwenye dalili za namna hiyo atapingwa, atadhibitiwa kwa heri au kwa shari. Ilimradi muungano usivunjike.
3. Uzalendo
Bob, bila kuvuka walau 70% ya uzalendo huwezi kuwa Rais wa taifa hili. Moja ya dalili za mtu Mzalendo ni kuitetea nchi hii kwa kukemea maadui zetu bila kificho. Bob wewe ni Mzungu wa Kanada, nataka nikuambie kuwa ninyi ndugu zetu wazungu mmekuwa mkitumia janja janja kutuibia mali zetu. Mnatupa 10 mnachukua 1000. Mnatuibia mali zetu kwa kile kiitwacho mikataba ya kimataifa, misaada, haki za binadamu n.k
Sasa sisi kwenye uchaguzi tunaangalia ni nani ataweza kukabiliana nanyi, nani ataweza kuhimili mikiki mikiki yenu, nani ataweza kuwatolea maneno ya shombo kama baadhi ya viongozi wa jamii za kizungu wanavyotutolea. Bob, Rejea kauli ya Bwana Donald Trump ambaye alitusimanga kwa maneno ya hovyo akiziita nchi zetu ni "shithole countries''
4. Kukomboa fikra za Watanzania.
Ndugu Amsterdam, nchi yetu ipo huru lakini bado hatupo huru kiuchumi na kiutamaduni. Na ili tuwe huru kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamadani sharti tukombolewe Kifikra. Bob, wewe unajua kile ninachozungumzia. Huwezi kuwa huru kama u mtumwa wa kifikra.
Tunamchagua Rais atakaye wakomboa Watanzania Kifikra. Rais atakayejenga fikra za watanzania kuwa wanaweza kujitegemea, wanaweza kuendesha maisha yao bila ya msaada wa wageni.
Rais atakaye waambia wananchi waache kutegemea wanasiasa, waache kutegemea mambo ya kupewa, bali wafanye kazi kwa bidii.
Hatutaki Rais anayewategemea ninyi ndugu zetu wazungu, watani wa jadi.
Ndugu wajina, mteja wako ni mtu mashuhuri hapa nchini, ni mwanasheria mzuri ambaye ninampenda, jambo pekee ambalo natamani kuliona kutoka kwake ni kuona akiwatukana ninyi watani zetu wa Jadi ambao mmetuweka kwenye kumi na nane zenu za ukoloni mamboleo.
Hatuogopi barua zako ikiwa zitagusa maslahi ya watanzania, hatutaogopa kuchukua hatua kulingana na sheria za nchi yetu pale mteja wako atakapovunja sheria za nchi hii.
Mimi namkubali sana Tundu Lisu ambaye ni mteja wako, lakini haitakuwa sababu ya yeye kututisha na ninyi watani zetu wa jadi.
Mteja wako atachaguliwa na watanzania ikiwa ataonekana na dalili zozote za mambo manne niliyoyataja hapo juu.
Kuhusu Kukatwa kwa Mteja wako.
Bob, sipendi Tundu Lisu aenguliwe na NEC, lakini kama itabainika anashirikiana na adui zetu kwa namna yoyote ile basi napendekeza akatwe mapema sana
Lisu ni Rafiki yangu, sijawahi kujificha kumtetea, kumpendekeza, kumsifia, kulaani hata siku aliyopigwa risasi. Lakini kama ataungana na ninyi watani zangu, wazungu ambao Taikon nawachukulia kama adui wa nchi yangu hakika nitapendekeza akatwe.
Ikiwa Lisu atabainika atahatarisha muungano basi aenguliwe.
Niliwahi kumsikia kipindi cha nyuma akiongea maneno yenye ukakasi ambayo bila shaka yanaukweli ndani yake, lakini ni ukweli usio na faida kwa nchi yetu zaidi ni ukweli wenye hasara ya kuleta utengano kwa nchi hii. Tunapenda ukweli, lakini ukweli wenye faida.
Ndugu Amsterdam, nilimpa mteja wako homework ambayo ingetoa muelekeo kwa wale wanaokaribia kumuamini na kutaka kumchagua. Nilimpa kazi mbili:
i. Azungumzie suala la ushoga, alikemee kwa nguvu zote.
Bob, Nchi yetu hairuhusu mambo hayo, ni kosa kisheria. Nafahamu nchi zenu sio kosa. Lakini kwetu ni kosa kubwa.
Tundu Lisu hakuwahi kuteteaa ushoga, lakini alionekana kupata kigugumizi kupinga ushoga pale alipoambiwa anazungumziaje suala la wapenzi wa jinsia moja. Lisu alikuwa na nafasi ya kuonyesha msimamo wake. Sasa kama alishindwa kipindi kile, nimempa homework kabla ya uchaguzi atoe msimamo wake. Aklishindwa majibu atayapata kwa watanzania. Mimi msimamo wangu ni kuwa nitampinga kila nipitapo nafasi ikiwa hatatoa ufafanuzi.
ii. Kuwakashifu ninyi wazungu
Nilimpa kazi ya pili kuwa, kama kweli anaipenda nchi hii basi angalau siku moja nimsikie akiwatukana ninyi, awatolee maneno ya kuudhi, kuchoma, kuteketeza. Mteja wako ameonekana kushindwa kuwasema ninyi vibaya. Hali inayonifanya nimuone kama kibaraka wenu.
Lisu ni rafiki yangu, ndugu zangu wanajua, maandiko yangu yanajieleza mara kadhaa, mchumba wangu anajua jinsi ninavyomkubali Lissu. Lakini kitu pekee wanachokijua watu hao pia kutoka kwangu ni kuwa sina unafiki.
Lisu kama utashindwa homework zangu, nakuhakikishia hutaenda popote Taikon angalipo, kama Mungu aishivyo.
Nimalize kwa kusema; Ndugu wajina wangu Robert Amsterdam, Mteja wako bado kuna mambo ameshindwa kujipapambanua. Hivyo barua zako hazitutishi kwa lolote lile.
Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
0693322300
robertheriel99@gmail.com