Mimi ni mkristo mkatoliki, lakini kamwe siwezi kuunga mkono harakati zozote za kutafuta haki katika Taifa letu kwa kupalilia utengano au ubaguzi wa kidini.
Utawala huu ni mbaya kwa kila mpenda haki, bila ya kujali dini yake. Utawala huu unateka na kuua watu bila ya kujali ni wa dini gani. Ali Kibao (Mungu amrehemu), alikuwa muislam, lakini alitekwa na kufanyiwa unyama wa kila aina na kisha kuuawa. Wapo wakristo waliotekwa na kuuawa, na wengine hatujui kama wapo hai au wamekwishauawa. Huu utawala haujali wewe ni muislam, mkristo au mpagani, alimradi unapenda haki, unapigania haki, unakemea matendo ya kishetani kama hayo ya kuteka na kuua watu, wewe tayari unakuwa ni adui kwao.
Hata hawa watawala wanaotenda huu uharamia hawatendi hayo kwa misingi ya dini zao, bali ni kutokana na ushetani uliomo ndani ya mioyo yao. Rais ni muislam, lakini wasaidizi wake ni wa dini zote, na hata hao wauaji ni wa dini zote, kinachowaunganisha ni kupenda dhuluma. Kwa kuwa wao wanaunganishwa na uovu, sisi tunaofanyiwa uovu, tunatakiwa kuunganishwa na dhamira ya kuitafuta haki, na siyo kitu kingine.
Kumbukeni wapo mashekhe walioamua kuungana na wadhulumaji haki, lakini wapo pia wachungaji na maaskofu walioamua kuungana na wadhulumaji haki. Tusipotee njia wala lengo. Tusilete fikra za uwongo kuwa kila mkristo ni mpenda haki, wapo wadhulumaji, watekaji na wauaji. Wala tusitake kuwadanganya watu kuwa kila muislam ni mdhulumaji wa haki au anapenda dhuluma, wapo waidlslam wengi ni wahanga wa dhuluma, na wanaililia na kuitafuta haki.
Jambo la muhimu, wapenda haki tuunganishe nguvu za kuitafuta haki, tusiangalie huyu ni wa dini gani, ana dini au hana dini, msomi au hana elimu, tajiri au maskini, alimradi anachukia dhuluma, huyu ni mmoja wetu katika kuililia haki.