Watu wa Pwani kupitia TAA na baadae TANU wana mchango mkubwa kwenye zile harakati...(Japo Watanganyika wa mahali pengine pia walishiriki).
Usisahau ni wao (Wazee wa Dar es salaam )walimpokea Mwl.Nyerere kumpa Uenyekiti wa TAA baadae TANU Kisha kumshinikiza aache Ualimu kule Pugu na wao kumlipa kwa pesa zao.
Hakuna anaepinga mchango wa watu wa pwani katika harakati za kupigania uhuru wetu. Hao watu wa pwani hawakuwa waislamu peke yao maana walikuwepo wakina Mhando, waanglikana kutoka Tanga.
Huo uongo wa kuwa wazee wa Dar ndio waliompa Uenyekiti Nyerere unahitaji ufafanuzi maana unadogosha juhudi za watu kama Hamza Mwapachu.
Nyerere alijiunga na Tanganyika African Association akiwa mwanafunzi Makerere miaka ya 1940s. Akiwa Makerere alikutana na Hamza Mwapachu, Andrew Tibandebage. Hao marafiki watatu walianzisha the Tanganyika Welfare Students Organisation mwaka 1943 ambayo walitaka iwe tawi la TAA lakini Makao Makuu ya TAA haikuwajibu. Marafiki hao walikuwa wote Tabora, Mwapachu akifanya hospitali na Tibandebage wakifundisha shule ya sekondari ya St. Mary. Wakiwa Tabora walijiunga na tawi la TAA la Tabora na mwaka 1946 Hamza Mwapachu alichaguliwa kuwa Rais wa tawi hilo, Nyerere Katibu na Tibandebage Mweka Hazina. Mwaka 1947, Hamza Mwapachu aliacha kazi hospitali. Alienda Wales kusomea Diploma ya Social Work. Baada ya Mwapachu kuondoka Nyerere alichaguliwa kuwa Rais wa tawi la TAA Tabora. Nyerere nae aliondoka 1949 kwenda masomoni UK ambako alijiunga na Chuo Kikuu cha Edinburg. Alihitimu mwaka 1952 na Masters.
Mwapachu alirudi Tanganyika 1949 ambako alianza kazi kama Assistant Welfare Officer Ilala. Rashid Kawawa alifanya nae kazi kama karani wa welfare. Mwapachu aliungana na Abdul Wahid Sykes katika mpango wa kuigeuza TAA kuwa chama cha siasa. Juhudi hizo ziliungwa mkono na Dr. Lucian Tsere, Dr. Vedast Kyaruzi, Stephen Mhando na Paul Rupia. Mwapachu na Sykes ndio walio ongoza mapinduzi dhidi ya uongozi uliokuwepo wa TAA. Baada ya hayo mapinduzi Dr. Tsere alichaguliwa kuwa Rais wa muda. Katika uchaguzi wa kwanza wa TAA baada ya mapinduzi uongozi wa TAA ulikuwa kama ifuatavyo:
1. Rais alikuwa Vedasto Kyaruzi
2. Abdulwahid Sykes alikuwa Katibu Mkuu
3. John Rupia Mweka Hazina
4. Hamza Mwapachu Katibu wa Uchumi na
5. Stephen Mhando Katibu wa Elimu.
Uongozi huu (uliokuwa na vijana wa kiislamu wawili na wagalatia watatu) ulipeleka waraka wa kwanza Umoja wa Mataifa kudai ratiba ya wazi ya kuelekea kwenye uhuru wa Tanganyika. Mwandishi mkuu wa huu waraka alikuwa Hamza Mwapachu.
Baada ya huu waraka, Dr. Kyaruzi alihamishwa kutoka Sewa Haji Hospital kwenga jela ya Kingolwira na Mwapachu alihamishiwa Ukerewe. Akiwa Ukerere alimgundua Paul Bomani Mwanza ambae alimwambia rafiki yake Nyerere aliyekuwa Edinburg wakati ule kuwa Bomani atakuwa na mchango mkubwa katika mapambano yao. Akiwa Ukerewe Hamza Mwapachu alijadiliana na Nyerere kuhusu yeye kuongoza TAA 1953. Mwapachu ali mu endorse rafiki yake kuwa Rais wa TANU 1954 ingawa yeye mwenyewe alinyimwa ruhusa kuja Dar kutoka Ukerewe wakati wa uanzishwaji rasmi wa TANU.
Ukisoma hili bandiko vizuri utaona wazi ushirikiano ulivyokuwa mkubwa kati ya waislamu na wakristu. Utagundua pia kuwa Nyerere hakuingizwa TAA na wazee wa kiislamu wa Dar es Salaam. Ni kijana mwenzake Hamza Mwapachu ndiye aliyemuunganisha na wakina Abdulwahid Sykes. Nyerere kwa muda mrefu alikuwa mwalimu kwa hiyo hakuihitaji kulishwa na mtu. Alipoacha kazi Saint Francis alirudi kwao ambako alisaidiwa na masista wa Maryknoll.
Wazee wa Dar hawakumshinikiza kuacha kazi bali aliambiwa na muajiri wake achague moja kati ya siasa na ajira, yeye akachagua siasa. Ni kweli wazee wa kiislamu walishiriki kikamilifu katika juhudi za kudai uhuru lakini hii haimaanishi kuwa walikuwa wao peke yao. Vijana wa kiislamu wakina Hamza, Abdulwahid hawakuona tatizo kushirikiana na wakina Julius, Vedasto na Stephen. Wakina Bibi Titi walishirikiana kikamilifu na wakina Oscar na wakina Lucy katika juhudi hizo.
Kuziangalia juhudi hizi kwa misingi ya dini ni kunajis mchango wa hawa wazee wetu walio tupigania mpaka tukapata uhuru wetu bila kujali dini, kabila au jinsia. Kufanya hivyo kunatufanya kusahau mchango mkubwa wa watu kama Hamza Mwapachu. Hiyo sio sahihi hata kidogo. Uhuru wetu haukuchangiwa na wazee wa Gerezani peke yao. Watanganyika karibu wote walichangia. Sio tuu watanganyika, hata wanyasa, wakenya, wazungu, wahindi nao walichangia.
Amandla...