BIBLIA IPO WAZI SANA UKIISOMA KWA MAOMBI,
ILA MOST YA MAKANISA YANAPOTEA NA KUPOTEZA WAUMINI, HASA KWA KUTOELEWA MAANDIKO YA PAULO
NA KUPITIA MAANDIKO YA PAULO (AKILI NYINGI) NDIO WENGI WAMEANZISHA MAKANISA NA MADHEHEBU MAANA WANASHINDWA KUTAFSIRI MAANA SAHIHI
KUPITIA maandiko ya Paulo utakutana na mafundisho Kama kunena kwa Lugha kwa kufokafoka ,kula nguruwe wakidai Paulo karuhusu ,n.k
Asilimia 90 ya MAKANISA na MADHEHEBU yanayoibuka Ni kupotosha maandiko ya vitabu vya Paulo
Petro mwanafunzi wa Yesu aliposoma maandiko ya Paulo alichanganyikiwa ,itakuwa Mwamposa ,au Gwajima wenye Njaa ?
JUZI nilikuwa safarini , njiani nilimsikia muislamu akiponda Sana Agano jipya akidai limeruhusu kula nguruwe , wakati agano la Kale limekataza, nikajisemea Moyoni , NI KUTOKUELEWA TU.......
Mtume Petro alitoa angalizo juu ya usomaji wa nyaraka za Paulo na akatoa onyo lifuatalo:
#2 Petro 3:15-17
Nanyi uhesabuni uvumilivu wa Bwana wetu kuwa ni wokovu, kama vile na ndugu yetu mpenzi Paulo alivyowaandikia kwa hekima aliyopewa;
vile vile kama katika nyaraka zake zote pia, akitoa humo habari za mambo hayo; katika nyaraka hizo yamo mambo ambayo ni vigumu kuelewa nayo; na mambo hayo watu wasio na elimu, wasio imara, huyapotoa, kama vile wayapotoavyo na maandiko mengine, kwa uvunjifu wao wenyewe.
Sio Petro tu ndio anadai kwamba nyaraka za Paul ni ngumu, bali hata watu wengine pia wanasema nyaraka za Paul ni ngumu, Na Paul yeye mwenyewe anashuhudia kwamba watu wanasema nyaraka zake ni nzito/ ngumu:
2 Wakorintho 10:9-10
nisije nikaonekana kana kwamba nataka kuwaogofya kwa nyaraka zangu.
Maana wasema, Nyaraka zake ni nzito, hodari; bali akiwapo mwenyewe mwilini ni dhaifu, na maneno yake si kitu.
.
Hivyo inabidi umakini mkubwa sana unapokutana na aya tata katika Nyaraka za Paul, pia ieleweke kwamba Nyaraka zote za Paul alikuwa anashugulika na kutatua migogo ya kiimani iliyokuwa inatokea ndani ya Kanisa baina ya washiriki, na pia alikuwa anashugulika na walimu wa uwongo waliokuwa wakiingiza mafundisho potofu ndani ya kanisa. Ikumbukwe kwamba makanisa yote ambayo Paul anayaandikia nyaraka ni makanisa ya watu waliokuwa na mchanganyiko baina ya Wayahudi na watu wa Mataifa, mengine yalikuwa ni machanga katika imani.
#Sasa kabla ya yote inabidi tuzingatie mambo yafuatayo ili tuweze kuelewa nyaraka za Paulo na vitabu vingine:
1. Waraka huo aliwaandikia watu gani?
2. Kulikuwa na changamoto gani ?
3. Alishughulika vipi na hiyo changamoto.
Kwa hiyo kwa utangulizi huo, naomba tuchungze baadhi ya hoja zinazo patikana katika Warumi 14. Miongoni mwa hoja ambazo hujengwa na baadhi ya wakristo katika kitabu hiki ni
1. Siku zote ni sawa, hivyo unaweza kuabudu siku yoyote ile.
2. Ikiwa mwenzako anakula nguruwe wewe kumnyoshea kidole.
3. Hakuna kitu kilicho najisi kwa asili yake.
Kanisa la Rumi lilikuwa na mchanganyiko wa Wayahudi na Watu wa mataifa, Rumi ilifikiwa na injili na mitume baada ya Yesu kupaa mbinguni, watu wengi wa mataifa waliokuwa wakisali katika kanisa la Rumi na Korintho, mwanzo walikuwa ni wapagani, wakijihusisha na ibada za sanamu, na hivyo baada ya kuipokea injili waliachana na upagani. Hata hivyo changamoto zilizokuwa zinalikabili Kanisa la Rumi, ndizo changamoto zilizokuwa zinalikabili Kanisa la Korintho.
#CHANZO CHA MIGOGORO JUU YA CHAKULA:
Kwa sababu kanisa lilikuwa linajumuisha Wayahudi na Wamataifa, hivyo mgogoro ulikuwa kati ya waumini wa Kiyahudi na waumini wa kimataifa.
Sasa hawa waumini wasio wayahudi zamani kabla ya kumpokea Yesu walikuwa Wanatoa sadaka kwa masanamu, kisha ile nyama ilikuwa inapelekwa Masokoni kwa ajili ya kuwauzia watu, lakini baada ya kumpokea Yesu wakaachana na ibada za sanamu, na hata nyama zilizokuwa zinauzwa masokoni wakawa hawanunui, kwa kuhofu zitakuwa zimeolewa sadaka kwa sanamu na hivyo watajitia unajisi ,matokeo yake wakawa wanakula mbogamboga tu.
Na Baada ya Paul kupata habari hizo juu ya huo mgogoro na ndipo anaandika waraka huu kwa Warumi. Na anaanza kwa kusema:
#Warumi 14:1-2
Yeye aliye dhaifu wa imani, mkaribisheni, walakini msimhukumu mawazo yake.
Mtu mmoja anayo imani, anakula vyote; lakini yeye aliye dhaifu hula mboga.
Kwa hiyo Paul anawaambia mtu akiwa mdhaifu wa imani wamkaribishe, haijarishi anakula nyama au hali asihukumiwe kwa imani yake aliyonayo. Kwa sababu imani yake ameijenga kwa Mungu.
Ndipo sasa mgogoro ukainuka kanisani Wakristo wa kimataifa wakaanza kuwaona Wakristo wa Kiyahudi wamepotoka maana wanakula nyama zilizotolewa sadaka kwa sanamu, na Wayahudi nao wakawa wanawaona Wakristo wa kimataifa wamepotoka kwa kutokula nyama.
Lakini waumini wa Kiyahudi kwa sababu wao walikuwa hawajui historia ya zile nyama zinazouzwa masokoni, wao wakawa wananunua na kula, mbaya zaidi wakawa wanakula mbele za waumini wapya tena ndani ya mahekalu ya sanamu, na Paul anatoa onyo kwa kwa wale wanaokula nyama kwa kusema kwa dhamili zao:
# Warumi 14:22
Ile imani uliyo nayo uwe nayo nafsini mwako mbele za Mungu. Heri mtu yule asiyejihukumu nafsi yake katika neno lile analolikubali.
# 1 Wakorintho 8:10
Kwa maana, mtu akikuona wewe uliye na ujuzi, umeketi chakulani ndani ya hekalu la sanamu, je! Dhamiri yake mtu huyo, kwa kuwa yu dhaifu, haitathibitika hata yeye naye ale vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu?
#1 Wakorintho 8:7-8
Bali ujuzi huu haumo ndani ya watu wote; ila wengine kwa kuizoelea ile sanamu hata sasa hula kana kwamba ni kitu kilichotolewa sadaka kwa sanamu; na dhamiri zao, kwa kuwa dhaifu, hunajisika.
Paul anawaonya wale waliokuwa wanajiona wapo imara katika imani kwamba si vizuri kufanya mambo hayo hadharani, itawafanya wale waumini wapya kudhoofika kiroho.
Hivyo ikawa waumini wakienda sokoni kununua nyama walikuwa wanaanza kuuliza kwa wauzaji je, hii nyama imetolewa sadaka kwa sanamu au la, Na ndio maana Paul anawaambia Kanisa la Korintho wakienda sokoni wasianze kuulizauliza kwamba nyama hii imetolewa sadaka kwa sanamu au la, bali anawaambia kwa sababu ya dhamili wanunue maana hawawezi ukapata majibu sahihi:
#1 Wakorintho 10:25
Kila kitu kiuzwacho sokoni kuleni, bila kuuliza-uliza, kwa ajili ya dhamiri;
Lakini kama mtu dhamiri yake haimruhusu basi asile maana atakuwa anatenda dhambi:
#Warumi 14:23
Lakini aliye na shaka, kama akila, amehukumiwa kuwa ana hatia, kwa maana hakula kwa imani. Na kila tendo lisilotoka katika imani ni dhambi.
Fikiria hata wewe mwenyewe hivi umeenda sokoni ukaanza kuuliza nyama hii ni kibudu? unamuuliza muuzaji Au nyama hii ni ya leo au ya jana? Unadhani atakupa majibu sahihi? Ni wachache sana watakao kwambia ukweli. Hata sisi wenyewe tunanunua nyama kwenye mabucha kwa sababu dhamiri zetu zinatutuma kwamba ni nyama sahihi, lakini kiuhalisia kuna nyama nyingi haramu zinauzwa katika mabucha na wengi tumezila, hata nyingine ni za matambiko. Isitoshe vipo vyakula vingi tunavyokula sasa na tuna vipenda, ambavyo laiti tungejua mazingira na jinsi vinavyo tegenezwa hatungependa kula vile vyakula.
Au ni mara ngapi umekula nyama ambayo hujui ni aina gani ya nyama au ni aina gani ya ndege?
Sasa hawa ndugu zetu wa Rumi na Korintho wakienda sokoni au wakialikwa mahali kwa mtu au katika sherehe, swali la kwanza walikuwa wanawauliza wahusika je, nyama hii imetolewa sadaka kwa sanamu? Wakiambiwa ndio basi hawali ile nyama..
Hivyo chanzo cha mgogoro ni juu ya ulaji wa nyama zilizo tolewa kafara kwa sanamu, ni makosa makubwa kutumia sura hii kuharalisha ulaji wa nguruwe, maana sio kiini cha mgogoro. Na haimaye Paul anatoa ushauri katika nyaraka zote mbili kwamba ni bora kuachana na ulaji wa nyama, ambao unasababisha migogoro ndani ya kanisa;
#Warumi 14:21
Ni vyema kutokula nyama wala kunywa divai wala kutenda neno lo lote ambalo kwa hilo ndugu yako hukwazwa.
#1 Wakorintho 8:13 Kwa hiyo, chakula kikimkwaza ndugu yangu, hakika sitakula nyama hata milele, nisije nikamkwaza ndugu yangu.
#HAKUNA KITU KILICHO NAJISI KWA ASLI YAKE
#Warumi 14:14-15
Najua, tena nimehakikishwa sana katika Bwana Yesu, ya kuwa hakuna kitu kilicho najisi kwa asili yake, lakini kwake yeye akionaye kitu kuwa najisi, kwake huyo kitu kile ni najisi.
#>>>>Watu wengi hupenda kutumia fungu hili kama kichaka cha kutetea ulaji wa nguruwe hasa katika kipengele kinachosema>>> #Najua, tena nimehakikishwa sana katika Bwana Yesu, ya kuwa hakuna kitu kilicho najisi kwa asili yake.
Kwa hiyo kama nilivyotangulia kusema hoja katika sura hii sio ulaji wa nguruwe, bali ni ulaji wa nyama zilizotolewa kafara kwa sanamu, na ulaji wa mbogamboga.
Lakini pia Paul anapoandika aya hii anaandika kulingana na tukio na mazingira, Anaposema #Hakuna kitu kilicho najisi kwa asili yake# Kauli hii anazungumza na Kanisa la Rumi kulingana na mgogoro uliokuwepo kwa sababu hakuna mnyama yeyote najisi ambaye huwa anatolewa sadaka kwa sanamu wala huwezi kusikia mganga wa kienyeji amedai mtu apeleke nguruwe, mbwa, paka, au bata kwa ajili ya kafara kwa miungu yake.
Wanyama ambao hutolewa sadaka iwe kwa sanamu au kwa waganga ni wale ambao ni safi: kama ng’ombe, mbuzi, kondoo nk.
Hivyo basi Paul anaposema #Hakuna kitu kilicho najisi kwa asili yake# alikuwa anamaanisha wale wanyama waliokuwa wanatolewa sadaka hapo Rumi yaani kama mbuzi, kondoo, ng’ombe nk.. kwa sababu ni wanyama safi, tangu asili yake, hivyo hawawezi wakawa najisi, labda kwa mtu binafsi.
Mfano; ukija kwangu mimi nikikwambia uwe huru kula nyama yoyote maana ni safi, kwa kauli hiyo sina maana ya nyama ya nguruwe, kobe, sungura nk. Sasa hii ni kauli ya kimazingira kulingana na imani yangu ina maana ya nyama ya mbuzi, kondoo, kuku, nk. Kwa hiyo huwezi ukatumia kauli hiyo kudai kwamba
hamis77 anakula nguruwe au sungura. Au nime halalisha ulaji wa nguruwe hapana.
Hata hivyo Paulo anahitimisha hoja yake ya kutatua mgogoro kwa kuwahimiza Waumini wa Kiyahudi kwamba wajitahidi kuonesha upendo kwa waumini wa Kimataifa, na sio wao Wayahudi kujipendeza wenyewe:
#Warumi 15:1-2
Basi imetupasa sisi tulio na nguvu kuuchukua udhaifu wao wasio na nguvu, wala haitupasi kujipendeza wenyewe.
Kila mtu miongoni mwetu na ampendeze jirani yake, apate wema, akajengwe.
Ukweli ni kwamba Warumi sura ya 14,haina uhusiano wowote na suala la ibada ya siku ya saba au siku ya kwanza ya juma, na wala haitetei wala kupinga ulaji wa wanyama najisi.
.