KERO Wanafunzi wa Shule ya Sekondari MUNGUMAJI - Singida wanasoma kwa shida, hawafundishwi vizuri, chakula shida

KERO Wanafunzi wa Shule ya Sekondari MUNGUMAJI - Singida wanasoma kwa shida, hawafundishwi vizuri, chakula shida

Hii ni kero ambayo mwananchi ameiwasilisha JF akitaka wahusika kuchukua hatua
A

Anonymous

Guest
Naishi Mkoa wa Singida, naomba kuwasilisha changamoto zinazowakabili wanafunzi wa Kidato cha Tano na Sita katika MUNGUMAJI SECONDARY SCHOOL, Singida Mjini. Mdogo wangu alifaulu kujiunga na shule hiyo, lakini mpaka sasa amekataa kabisa kuendelea na masomo pale na amekuwa akitaka ahamishwe.

Mwanzoni tulidhani labda ni changamoto za kawaida za mwanafunzi mpya, lakini baada ya kufuatilia kwa kina tuligundua kuwa kuna mambo kadhaa yanayowasumbua wanafunzi wa A-Level.
476486552_2628867787311001_3729087581036204257_n.jpg
480881286_945106824485156_9046770621996454153_n.jpg
Changamoto kubwa ni ufundishaji. Kwa mujibu wa kile nilichofuatilia, kuna baadhi ya walimu ambao inadaiwa huwatoza wanafunzi shilingi 3,000 kila mmoja ili waje kuwafundisha.

Inadaiwa kwamba mwanafunzi ambaye hajachangia kiasi hicho anaweza kukosa somo kwa sababu mwalimu hataki kuingia darasani mpaka wanafunzi wote wachangie. Hali hii inawaweka wanafunzi katika mazingira magumu, hasa kwa kuwa elimu ya A-Level inahitaji muda wa kutosha wa kufundishwa na kuelekezwa na walimu.

Changamoto nyingine ni chakula. Wanafunzi wamekuwa wakilalamikia ubora na kiasi cha chakula wanachopewa. Wakati fulani, baadhi ya wanafunzi walifikia hatua ya kwenda kwa Mkuu wa Wilaya ya Singida, Godwin Gondwe, kueleza malalamiko yao.

Baada ya Mkuu wa Wilaya kufika shuleni na kuzungumza na walimu, aliagiza kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula kwa kiwango kinachostahili. Kwa muda wa takribani wiki mbili baada ya maagizo hayo, hali ilionekana kuwa nzuri, lakini baadaye, kwa mujibu wa malalamiko ya wanafunzi, changamoto ziliendelea tena.

Pia, kuna suala la wanafunzi kutakiwa kutafuta kuni wakati wa vipindi. Kwa mujibu wa malalamiko haya, Wanafunzi wa A-Level huambiwa kwenda kutafuta kuni badala ya kuwa kwenye vipindi vyao. Hali hii inaweza kuathiri muda wao wa kujifunza, hasa kwa wanafunzi ambao tayari wana muda mfupi wa kujiandaa kwa mitihani ya taifa.

Naomba TAMISEMI, uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida pamoja na Wizara ya Elimu wafuatilie kwa kina hali hii katika Shule ya Mungumaji, wazungumze na wanafunzi, walimu na wazazi ili kubaini ukweli wa malalamiko haya.

Sisi wazazi na ndugu tunataka watoto wetu wapate elimu katika mazingira salama, wapate chakula kinachostahili na walimu wafundishe bila kuwawekea wanafunzi masharti yanayoweza kuathiri masomo yao. Kwa sasa tunaona wanafunzi wa A-Level wanapitia changamoto kubwa, na tunaomba mamlaka zichukue hatua kabla hali haijawa mbaya zaidi.
481023548_945106894485149_4579759103699161606_n.jpg
480981310_945107017818470_952715534259393260_n.jpg
 
  • Thanks
Reactions: Lax
Poleni sana
Nikistaafu kazi yangu ya uhandisi huku ulaya, nitarudi kuwa najitolea kufundisha mashule ya vijijini bure
 
Back
Top Bottom