Wananchi wa Kijiji cha Machemba, Wilaya ya Tunduru wameiomba Serikali kuwapatia vyanzo salama vya maji baada ya kueleza kuwa wanategemea kisima ambacho, kwa mujibu wao, hakikidhi viwango vya usalama kwa matumizi ya kila siku.
Ombi hilo limetolewa Seotemba 23, 2026 baada ya Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Ado Shaibu Ado kumaliza kuzungumza na wananchi hao katika ziara yake ya Kijiji kwa Kijiji, ambapo wananchi waliongozana naye hadi kwenye kisima wanachokitumia kwa shughuli zao za kila siku.
Wananchi hao wamemweleza Ado kuwa hali ya kisima hicho ni changamoto, huku wakidai kuwa matumizi ya maji hayo wakati mwingine yamekuwa yakisababisha matatizo ya kiafya.
“Hayo ndo maji tunayokunywa tuna visima vitatu hali yake ndo hiyo na tukinywa haya maji muda mwengine tunaharisha”
Akijibu kilio hicho, Mbunge Ado ameahidi kulifikisha suala hilo kwa Waziri mwenye dhamana ya Maji, Jumaa Aweso kwa lengo la kutafuta suluhisho la changamoto hiyo na kuwawezesha wananchi kupata maji safi na salama.