Kwa maoni yangu, kama uko sehemu ambayo ugonjwa unaoenea kwa njia ya hewa kama kuna watu wawili - mmoja amevaa barakoa na mwingine hajavaa - unadhani ni nani kati ya hao anaweza kuambukizwa au kuwaambukiza wengine kwa urahisi? Au kabla ya corona haijaja, siku zote tangu nikiwa mtoto tumekuwa tukifundishwa kuwa ukitaka kukohoa funika mdomo wako kwa kitambaa safi na kama huna tumia mkono au kiganga chako. Nikuulize pia: katika sehemu ambayo mtu anaweza kuambukizwa au kuambukiza ugonjwa unaoenea kwa njia hewa, kati ya mtu anayekohoa bila kutumia kitambaa (mkono au kiganga) na yule anayekohoa bila kujali, unadhani ni nani anaweza kuwaambukiza wengine kwa urahisi zaidi? Kwa hiyo, ingawa hizi njia hazimkingi mtu kwa asilimia zote (100), walau zinaweza kupunguza maambukizi kama zikitumika kwa usahihi. Hivyo, ni juu yako wewe mwenyewe kupima - kama unaona hakuna haja ya kuvaa barakoa usivae, lakini hakikisha huhatarishi maisha ya wengine kwa kutojali kwako. Na kuvaa barakoa ni njia mojawapo tu, njia zingine ni lazima zizingatiwe pia.
Njia zinazoshauriwa na wataalamu wa afya ni hizi:
1. Safisha mikono yako mara nyingi iwezekanavyo. Tumia sabuni na maji, au 'sanitiser'.
2. Zingatia umbali wa kutosha kutoka kwa mtu anayekohoa au kupiga chafya.
3. Vaa barakoa mahali ambapo uwezekano wa kuwa na umbali wa kutosha kutoka kwa mtu anayekoa au kupiga chafya haupo.
4. Usiguze macho yako, pua au mdomo (na kama ukigusa angalia Na 1).
5. Funika pua na mdomo wako kwa kutumia kiwiko cha mkono au kitambaa safi kama unakohoa au kupiga chafya.
6. Kaa nyumbani kama hujisikii vizuri (kama unaumwa).
7. Kama una homa, kohoa na unashida ya kupumua, tafuta ushauri wa daktari.
Zingatia: kinga ni bora kuliko tiba.