Elias Msuya
Platinum Member
- Dec 23, 2011
- 267
- 1,014
Mkutano wa Rais Samia Suluhu Hassan, na viongozi wa vyama vya siasa uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam Julai 30, umeibua tena mjadala kuhusu mwelekeo wa maridhiano nchini baada ya kipindi cha mvutano wa kisiasa kilichofuatia uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Kwa upande wa Serikali, mkutano huo umeelezwa kuwa ni mwendelezo wa juhudi za kuimarisha maridhiano, demokrasia ya vyama vingi na mshikamano wa kitaifa. Katika taarifa yake, Ikulu ilisema mazungumzo hayo yalijikita katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, huku Rais Samia akisisitiza kuwa Serikali yake itaendelea kufungua milango ya mazungumzo.
Hakuna ubishi kwamba mazungumzo ni sehemu muhimu ya kutafuta suluhu za migogoro ya kisiasa. Taifa lolote linalotaka kujenga utulivu wa kudumu haliwezi kutegemea nguvu za dola pekee; lazima pia liwe na uwezo wa kusikiliza sauti tofauti.
Baadhi ya wachambuzi wametilia shaka mwenendo huo wa kutafuta mariidhiano kwa kudhani kuwa yanapatikana kwa vyama vya siasa pekee.
Maridhiano ni makubwa kuliko siasa za vyama
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Richard Mbunda, anaona kuwa mjadala wa maridhiano umejikita zaidi kwenye vyama vya siasa kuliko jamii nzima.Anasema ni kosa kufikiri kwamba mkwamo wa kisiasa uliojitokeza baada ya uchaguzi wa mwaka 2025 unaweza kutatuliwa na viongozi wa vyama pekee.
"Kuna jambo huwa tunalikosea sana kudhani kwamba mambo yaliyotokea Oktoba 29, 2025, au huu mkwamo wa kisiasa tulionao uliofanya mpaka nchi ikavimba, wanaopaswa kuushughulikia ni vyama vya siasa tu."
Hoja yake inatokana na ukweli kwamba malalamiko yaliyopo nchini hayajaanzia kwenye vyama vya siasa pekee.
Kwa mfano, wananchi wengi bado wanalalamikia huduma za msingi kama maji, barabara, elimu na umeme. Wengine wanaona viongozi wa ngazi za wilaya, mikoa na halmashauri hawawajibiki ipasavyo kwa wananchi kwa kuwa wengi wao ni wateule wa mamlaka ya juu.
Dk. Mbunda anasema ndiyo maana kila Rais au Waziri Mkuu anapofanya ziara za mikoani hulazimika kupokea hata malalamiko ambayo kwa kawaida yangepaswa kutatuliwa kwenye ngazi za chini za Serikali.
Hali hiyo, kwa maoni yake, inaonyesha kuwa changamoto si za kisiasa pekee, bali pia za utawala na uwajibikaji.
Makundi mengi yana malalamiko
Mbali na wananchi wa kawaida, Dk. Mbunda anaorodhesha makundi mengine yenye malalamiko.Anataja wafanyakazi wanaolalamikia kuchelewa kwa nyongeza za mishahara, wanataaluma wanaohofia uhuru wa kitaaluma, asasi za kiraia zinazolalamikia mazingira ya kazi, pamoja na vyombo vya habari vinavyohoji sheria na hatua za kufungiwa mara kwa mara.
"Ni makosa makubwa kudhani kwamba maridhiano ni suala la vyama vya siasa tu, ni makundi yote katika jamii."
Kwa mtazamo wake, maandamano yaliyoshuhudiwa katika vipindi tofauti tangu uchaguzi yanaonyesha kuwa wanaodai mabadiliko si viongozi wa vyama pekee bali pia wananchi kutoka makundi mbalimbali.
“Kwa mfano kuna malalamiko ya wananchi kwenye ngazi za Serikali za mitaa, kuhusu utoaji huduma za jamii kama maji, barabara, umeme, elimu na mengineyo. Wananchi hawana mamlaka ya kuwawajibisha viongozi waliopo katika kata, wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa na wakurugenzi wa halmashauri, kwa sababu hao wote ni wateule wa rais.
“Ndiyo maana Rais au waziri mkuu wakifanya ziara mikoani, wanapokea malalamiko madogo madogo yanayoweza kutatuliwa kwenye ngazi za chini, ni kwa sababu wananchi hawana Imani na uongozi uliopo ngazi hizo.
“Kuna malalamiko ya wafanyakazi, mwaka mzima unapita hakuna nyongoza ya mshahara, kuna malalamiko ya wasomi, leo imefika wakati mhadhiri anakamatwa akiwa anafundisha darasa! Pia kuna kuna malalamiko ya asasi za kiraia, ambako kumekuwa na kuviziana na Serikali. Kuna malalamiko ya vyombo vya habari, sharia mbovu, vinafungiwa kila mara,” amesema Dk Mbunda.
Kauli hiyo inaibua hoja muhimu. Ikiwa sababu za kutoridhika zinatokana na huduma za umma, haki za kiraia, uchumi na utendaji wa taasisi za Serikali, je, viongozi wa vyama vya siasa peke yao wanaweza kuwakilisha hisia za makundi yote hayo?
Wawakilishi wa maridhiano ni kina nani?
Mhadhiri mwingine wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Faraja Krisostom, anagusia suala la uwakilishi.Kwa maoni yake, baadhi ya vyama vinavyoshiriki mazungumzo vina ushawishi mdogo kwa wananchi kiasi kwamba haviwezi kubeba uzito wa maridhiano ya kitaifa.
"Vyama vinavyoshiriki hata mazungumzo haviko katika harakati za kisiasa nchini. Ni vyama vya mkoba Mwenyekiti na Katibu. Watanzania wengi hata hawawajui viongozi wao."
Anahoji kuwa kama lengo ni kujenga maridhiano ya kweli, basi ni lazima wahusishwe wale wenye ushawishi mkubwa na wale waliobeba athari za mgogoro.
Kwa maoni yake, walioathirika na matukio ya baada ya uchaguzi hawakuwa viongozi wa vyama pekee.
"Walioumizwa na matendo na maovu ya serikali na vyombo vyake ni makundi mbalimbali ya Watanzania. Wapo viongozi wa dini, wapo wanasiasa, wapo wapinzani, zipo asasi za kiraia, vipo vyombo vya habari, wapo vijana, walemavu, wanataaluma, wanawake na kadhalika," anasema.
Anasisitiza kuwa ni kosa kuifanya ajenda ya maridhiano kuwa ya kisiasa pekee.
"Siyo sahihi kabisa na ni makosa makubwa kudhani maridhiano ni mchakato wa kisiasa."
Serikali nayo ijitathmini
Hoja nyingine iliyotolewa na Dk. Faraja ni kwamba Serikali nayo inapaswa kutafakari nafasi yake katika kuzalisha mazingira yaliyosababisha mvutano."Jambo la kwanza na muhimu ni kwa serikali kutambua mchango wake kwa haya yaliyotokea. Ikiendelea kutafuta mchawi nje hatuwezi kupata maridhiano yenye tija," anasema.
Kauli hiyo haimaanishi kuwa Serikali ndiyo pekee yenye wajibu wa kutatua matatizo yote, bali inaonyesha kuwa katika mchakato wa maridhiano kila upande unatakiwa kuwa tayari kujitazama.
Kwa mtazamo wake, wananchi wengi bado wana hisia kwamba baadhi ya taasisi za dola hazikufanya kazi kwa namna iliyojenga imani.
"Matendo na mwenendo wa serikali ndiyo umesababisha madhila yote haya."
Hoja hiyo inaweza kukubaliwa au kupingwa kisiasa, lakini inaonyesha kuwa bado kuna sehemu ya jamii inayotaka kuona tathmini ya kina ya kilichotokea badala ya kuendelea kulaumiana.
CHADEMA ndiyo tatizo pekee?
Katika mjadala wa kisiasa, mara nyingi hoja imekuwa kwamba kutoshiriki kwa CHADEMA katika baadhi ya mazungumzo kunazuia maridhiano.Lakini wachambuzi wanaonya dhidi ya kuifanya hoja hiyo kuwa ndiyo msingi wa mjadala mzima.
Kwa mujibu wa Dk. Faraja, kuangalia zaidi chama kimoja kuliko wananchi waliobeba athari za mgogoro kunaweza kufanya mchakato mzima ukose uhalali.
"Ni bahati mbaya sana kwa serikali kufikiria zaidi kuhusu Chadema kuliko Watanzania."
Kauli hiyo inaungwa mkono na Dk Mbunfa, akirejea kauli yake ya kutaka maridhiano yahusishe makundi mengine.
“Tunarudi palepale kwamba, ni makossa kudhani kwamba maridhiano ni vyama vya siasa tu. Angalia makundi huko mitaani na ndiyo yamekuwa yakiitisha maandamano. Waliitisha maandamano Oktoba 29, 2025, waliitisha Desemba 9, 2025, wameitisha tena Julai 7, 2026. Ili kuwa na maridhiano sahihi lazima makundi yote ya jamii yahusishwe,” amesema.
Hata hivyo, Dk Faraja anakiri kuwa ikiwa chama chenye ushawishi mkubwa hakitakuwa sehemu ya mazungumzo, maridhiano hayo yanaweza kukosa uzito wa kisiasa kwa kuwa sehemu kubwa ya wananchi hawatajiona wamewakilishwa.
Hii inaonyesha kuwa maridhiano yanahitaji kuwa jumuishi kwa pande zote—Serikali, vyama vikubwa vya siasa na makundi mengine ya kijamii.
Soma pia: Wasira, Maridhiono siyo na CHADEMA ni Maridhiano ya Kitaifa na kuliponya taifa
Hitimisho
Kauli ya Rais Samia kwamba milango ya mazungumzo iko wazi ni ishara muhimu ya kisiasa. Inaonyesha kuwa Serikali bado inaamini katika nguvu ya mazungumzo badala ya migongano.Hata hivyo, maoni ya Dk. Richard Mbunda na Dk. Faraja Krisostom yanaibua tahadhari kwamba maridhiano ya kweli hayatapatikana kwa kuwakutanisha viongozi wa vyama vya siasa pekee.
Maridhiano ya kitaifa yanahitaji kuwagusa wale wote waliobeba maumivu, hasara na malalamiko yaliyotokana na mazingira ya kisiasa ya miaka ya karibuni. Yanahitaji kujenga imani kwa wananchi, kuimarisha uwajibikaji wa taasisi za umma na kuhakikisha kila kundi linapata nafasi ya kusikilizwa.
Kwa hiyo, mkutano wa Ikulu unaweza kuwa mwanzo mzuri wa safari. Lakini ikiwa Tanzania inataka kupata maridhiano ya kudumu, safari hiyo italazimika kuwa pana zaidi kuliko ukumbi wa mikutano wa viongozi wa vyama vya siasa. Itahitaji taifa zima kukaa mezani, kusikilizana, kukubaliana juu ya tofauti zao na kujenga msingi mpya wa kuaminiana.