Mkuu 'macho_mdiliko'
Nami nilitaka kuanzisha mada juu ya hii 'project' ya Bagamoyo, lakini zimekuwepo nyingi kiasi kwamba huenda mada nitakayoanzisha itaishia kwenye kuunganishwa na hizi ndefu na kuishia bila kusomwa.
Ni dhahiri, mradi huu una makundi yenye maslahi wanaouchochea kuupa nguvu, hasa hawa wa upande wa wachina, bila kujali maslahi ya Tanzania.
Mimi ningependa kuuliza na kupata maoni ya wachangiaji juu ya ugumu wa mradi huu kuufanya uwe wetu halafu tuwakaribishe wawekezaji wafanye wanavyotaka kuwekeza kwenye mradi wetu.
Hapo majirani Kenya na mradi wao wa Lamu wameuanzisha wenyewe, baada ya kuona kwamba wakitegemea wawekezaji ndio wauanzishe, huenda mradi huo usiwepo kabisa.
Kenya wamejenga Ghati tatu sasa; moja iko tayari na mbili hazipo mbali. Bandari inaweza kuanza kufanya kazi, na atakayetaka kwenda kuwekeza hapo kwa kujenga ghati nyingine, hadi zitimie 32, anakaribishwa.
Bagamoyo, kwa hakika ina sifa tofauti zaidi ya Lamu, sifa zinazovutia kwa uwekezaji; kama hali ya usalama, na ukaribu zaidi na nchi zitakazotumia bandari hiyo.
Je, sisi hatuna uwezo, hata kama utakuwa ni kukopa, kuanza ujenzi wa ghati chache hapo Bagamoyo, na wakati huo huo tukiiuza kwa wawekezaji, hata hao wachina waje kuwekeza, kama wanavyotaka kuwekeza sasa?
Mpangilio huu utakuwa na masharti tofauti na haya tunayokabiliana nayo wakati huu na huyu mwekezaji anayetaka bandari iwe ya kwake.
Nadhani katika hoja zinazotolewa kwenye mijadala hapa ukumbini, kuna mambo pia watu wanayasahau kwamba yapo.
Kwa mfano: Mchina hawekezi kwa asili mia katika mradi wa Bagamoyo, yeye anazo asili mia kadhaa atakazowekeza kwenye mradi huo, na yeye atatafuta wawekezaji wengine waje wawekeze chini ya himaya yake.
Mchina hatoi hiyo $30 bilioni, siku tutakayomkubalia kuwekeza hapo. Mu-Oman yeye za kwake zinajulikana ni asili mia kumi za mradi unaopangwa hapo, na hata sisi Tanzania tukisema tuwekeze zaidi ya hicho kiasi cha mchango wa ardhi kitakachohesabika kuwa ndizo hisa zetu katika uwekezaji, hilo pia linawezekana (sijaona popote linapokatazwa). Hata matajiri wetu hapa, akina Bakhresa, huenda watajitosa kuwekeza wakitaka, lakini kwa kwa hali ya sasa, uwekezaji huo utakuwa ni chini ya himaya ya mchina na siyo yetu (Tanzania).
Ninachoomba kujuwa, kuna tatizo lipi la kuufanya mradi huo uwe wetu? Bila shaka majibu mengi yatahusu hilo la uwezo wetu kujenga hizo ghati za mwanzo, lakini mbona Kenya wameweza?
Wengine watahoji tutawapataje wawekezaji ambao bado hawajaonekana Lamu - ukweli hapa ni kwamba Bagamoyo inauzika sana, ndiyo maana wachina hawabanduki kwenye mradi huo, vinginevyo ungekwishasikia wamekimbilia Lamu au kwingine.
Kama hatutaweza kupata mkataba wenye maslahi stahiki kwa nchi yetu, napendekeza, tuwe jasiri, tuuanzishe huu mradi wenyewe, halafu , kama tunavyofanya juhudi za kuwakaribisha wawekezaji nchini mwetu kwenye sekta hizi nyingine, tuweke jitihada kubwa za kutafuta wawekezaji kokote watakakopatikana, waje wawekeze kwenye eneo hilo kama ilivyopangiliwa katika uwekezaji wa sasa.