A
Anonymous
Guest
Mimi ni mzazi mwenye mtoto anayesoma katika Shule ya Msingi Bonyokwa iliyopo Wilaya ya Ilala, Kata ya Segerea, Dar es Salaam. Ninaomba kuwasilisha kilio changu kuhusu hali ya mazingira ya kujifunzia ambayo watoto wetu wanapitia shuleni hapo.
Changamoto kubwa ni wanafunzi wa Darasa la Tatu ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikaa chini wakati wa masomo kwa kukosa madawati ya kutosha. Watoto hao hukaa kwenye vumbi kwa muda mrefu wakiwa darasani, hali ambayo inaumiza na inaweza kuathiri afya zao pamoja na uwezo wao wa kujifunza.
Nimeshafika hadi kwa uongozi wa shule kuwasilisha malalamiko yangu kuhusu hali hii, lakini bado sijaona hatua za kutosha zinazochukuliwa. Kinachoniumiza zaidi ni kuona tatizo hili likiendelea wakati serikali ipo na inajitahidi kuboresha elimu nchini.
Hali ya madawati pia ni mbaya. Hata baadhi ya wanafunzi wanaopata nafasi ya kukaa kwenye madawati wanakaa kwa msongamano mkubwa, ambapo dawati moja linakaliwa na watoto hadi watano. Hii inafanya iwe vigumu kwa mtoto kupata nafasi nzuri ya kuandika, kusoma na kushiriki vizuri katika masomo.
Naumia kama mzazi kwa sababu watoto hawa ndiyo taifa la kesho. Elimu bora haiwezi kupatikana katika mazingira ambayo mtoto anakaa chini au anabanana kwenye dawati na wenzake wengi kupita kiasi.
Kinachoshangaza ni kwamba shule imepakwa rangi na inaonekana kwa nje kuwa imeboreshwa, lakini ndani watoto bado wanakabiliwa na changamoto ya kukosa madawati. Tunaomba mamlaka husika, ikiwemo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Wizara ya Elimu, ifuatilie suala hili na kuhakikisha watoto wanapata mazingira bora ya kujifunzia.
Tunaiomba serikali itoe msaada wa madawati na kuboresha mazingira ya shule hii ili watoto wa Bonyokwa nao wapate elimu katika mazingira yanayostahili, bila kulazimika kukaa chini wakati wa masomo.