Source : Kwa kirefu : (Habari na Picha ,Kitengo cha Mawasiliano Serikalini - Wizara ya Fedha na Mipango-Abu Dhabi)
……………………………………………….
Na Benny Mwaipaja, Abu Dhabi
SERIKALI ya nchi ya Umoja wa Falme za Kiarabu ya Abu Dhabi imeahidi kuendeleza ushirikiano katika masuala ya kiuchumi na kijamii na Serikali ya Tanzania ili kuwaletea wananchi wake maendeleo.
Ahadi hiyo imetolewa mjini Abu Dhabi, Falme za Nchi za Kiarabu na Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri anayeshughulikia masuala ya Rais, Sheikh Mansour bin Zayed Al Nanyan, baada ya kupokea ujumbe maalum kutoka kwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uliowasilishwa kwake na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Ikulu ya nchi hiyo.
Akizungumza baada ya mazungumzo yao ya faragha, Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alisema kuwa Sheikh Mansour ameahidi kutuma ujumbe maalum nchini Tanzania kwa ajili ya kuangalia miradi mbalimbali ya kimkakati inayotekelezwa hivi sasa na mingine mipya kwa ajili ya kutoa fedha.
Dkt. Nchemba aliitaja miradi iliyowasilishwa kwa Serikali ya Abu Dhabi kuwa ni ile ya uendelezaji wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Kuzalisha Nishati ya Umeme wa Mwalimu Julius Nyerere JNHPP Rufiji, ujenzi wa miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege, kilimo na uvuvi pamoja na elimu.
“Kwenye sekta ya elimu tumejenga madarasa mengi, tumejenga vituo vya afya vingi sana na vingine viko vijijini lakini hatujajenga nyumba za watoa huduma wanaotakiwa kufanyakazi kwenye maeneo hayo” alisema Dkt. Nchemba.