Bwana Mayalla wewe ni mwanasheria mpaka kubishana na TLS?
Kwa heshima, Mwongozo huu wa Mh. Rais wa TLS na Baraza lake la Uongozi, kwa maoni yangu, haupo sahihi, au umejipotosha wenyewe kuhusiana na tafsiri sahihi ya matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT).
Mwongozo una dosari ya dhahiri ya namna ya kutafsiri Katiba, lakini pia haujazingatia uwazi/ubayana wa nini Ibara husika za Katiba zili/zinanuia, au Katiba ilidhamiria.
Kwanza, kanuni ya harmonisation, kama kanuni ya kisheria ya msaada wa kutafsiri sheria au Katiba hutumika katika mazingira ambapo Ibara kadhaa za sheria au Katiba husika zinaonesha mkanganyiko bayana, au dosari, au jitihada za kutumia tafsiri ya moja kwa moja inasababisha mkanganyiko. Haitumiki katika mazingira ambapo Ibara za Katiba zipo wazi na bayana. Kwahiyo, kwa maoni yangu, Mwongozo ulipaswa kuanza kwa kuonesha mkanganyiko au dosari za tafsiri za Ibara husika. Mimi sioni ugumu katika tafsiri ya nini Ibara husika za Katiba zinadhamiria.
Pili, kanuni ya awali na pengine kuu katika kutafsiri Katiba ni "purposive approach" na sio "harmonisation". Hii inasaidia kuielezea zaidi hoja yangu ya kwanza. Mathalan, msomaji wa Katiba ya JMT ya 1977, kama ilivyorekebishwa mpaka sasa, akiisoma kwa kutumia purposive approach atayaona masuala yafuatayo bayana na yapo wazi:
Moja, kutakuwa na Rais wa JMT (Ibara ya 33),
Pili, kutakuwa na Serikali ya JMT, na mamlaka ya Serikali hiyo yatakuwa mikononi mwa Rais wa JMT (Ibara ya 34, pia Ibara ya 35),
Tatu, kutakuwa na Makamu wa Rais wa JMT... ambaye atakuwa Msaidizi Mkuu wa Rais (Ibara ya 47),
Nne, kutakuwa na Waziri Mkuu na Baraza la Mawaziri (Ibara ya 51, Ibara ya 54).
Kimtiririko, ni dhahiri kuwa Ibara nilizozitaja hapo juu, na nyingine ambazo sijazitaja, zipo katika SURA YA PILI ya Katiba... yenye kichwa, "Serikali ya JMT"... Sehemu ya Kwanza ni Ibara zinanazomhusu Rais... Sehemu ya Pili ni zile zinazomhusu Makamu wa Rais... na Sehemu ya Tatu ni zile zinazomhusu Waziri Mkuu na Baraza la Mawaziri...
Mpaka hapo hakuna ugumu wowote wa tafsiri au mkanganyiko, au ugumu. Purpose iko wazi pia... ni kuandika masharti yanayoihusu Serikali ya JMT na masuala yanayoihusu.
Tano, Rais na Makamu wa Rais wanapatikanaje? Ibara za 38, 39, 40, 41, 42 na 47, 48, 49 na 50 zinahusika. Ibara hizi zikisomwa purposively katika mtiririko huo, ni dhahiri kuwa Rais na Makamu wa Rais watachaguliwa kwa pamoja katika uchaguzi mmoja/ule ule... na wakishatangazwa kuwa hivyo, watashika nafasi zao kama masharti ya Katiba yanavyosema au taka.
Lakini, kuna kitu kimoja cha msingi sana cha kuzingatia katika masharti ya Katiba hii, kwamba, SIO KILA WAKATI KITI CHA RAIS KITAKAPO KUWA WAZI, kwasababu kadhaa zilizoainishwa na Katiba, kama vile KIFO CHA RAIS au MAKAMU WA RAIS, basi utaitishwa uchaguzi wa Rais, au Makamu wa Rais (Ibara ya 38 (2) ).
Sita, sasa, baada ya kuona hilo, ndipo Ibara ya 37, Ibara ndogo ya 5 itabisha hodi, hususan katika mazingira tuliyonayo sasa... yaani,
"Endapo kiti cha Rais kitakuwa wazi kutokana na Rais kufariki dunia..., basi Makamu wa Rais ataapishwa na atakuwa Rais kwa muda uliobaki katika kipindi cha miaka mitano na kwa masharti yaliyoelezwa katika ibara ya 40, kisha baada ya kushauriana na chama cha siasa anachotoka Rais atapendekeza jina la mtu atakayekuwa Makamu wa Rais na uteuzi huo utathibitishwa na Bunge kwa kura zisizopungua asilimia hamsini ya Wabunge wote."
Ibara hii iko wazi na bayana, kwamba Makamu wa Rais ataapishwa kuwa Rais... kisha atashauriana na chama chake kuteua mtu atakaye kuwa Makamu wa Rais...
Hakuna Ibara inayosema au hata kuashiria kuwa Waziri Mkuu atakoma kuwa Waziri Mkuu, na au Baraza la Mawaziri litavunjwa... kumbuka, Ibara ya 54 inawataja wajumbe wa Baraza la Mawaziri kuwa ni Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Rais wa Zanzibar na Mawaziri wote... Rais atahudhuria vikao vyake, na ndiye atakayeongoza vikao vyake.
Mpaka hapo, ni rahisi kubaini kuwa purposively Katiba hii haikudhamiria kuleta "mkwamo" au "ugumu" wa muendelezo wa shughuli za Serikali pale ambapo Rais atafariki... Katiba hii kama chombo kinachoishi na jamii yake, kilidhamiria kuwa ikitokea Rais akafariki, basi Makamu wake ataapishwa kuwa Rais kuendeleza Serikali ile ile... au kama yeye atakavyoona inafaa kwa mamlaka aliyopewa kwa mujibu wa Katiba. Hili nitalielezea zaidi hapa chini.
Saba, katika hali ya kawaida ni wakati gani Waziri Mkuu atateuliwa? Swali hili ni la msingi sana, na ndipo Mwongozo unapopotoka na kutaka kuleta mkanganyiko usiokuwa wa lazima au manufaa kwa nchi yetu.
Ibara ya 51 ipo wazi, kwamba, kutakuwa na Waziri Mkuu atakaye teuliwa na Rais; na kwamba, "Mapema iwezekanavyo, na kwa vyovyote vile ndani ya siku kumi na nne, baada ya kushika madaraka yake, Rais atamteua Mbunge wa kuchaguliwa kutoka katika jimbo la uchaguzi..." kuwa Waziri Mkuu ambaye atathibishwa na Bunge (Ibara ya 51 (2) ).
Swali hapa ni, Je, mara tu baada ya Makamu wa Rais kuapishwa kuwa Rais kufuatia kifo cha Rais, kwa mujibu wa Ibara ya 37, Ibara ndogo ya 5, atatakiwa kuteua Waziri Mkuu mwingine? Kwa maoni yangu ni HAPANA. HAPANA KUBWA. Kwanza, kwasababu, kama nilivyokwishasema awali, Katiba hii haijadhamiria kuleta mkwamo au kusimama kwa shughuli za Serikali kufuatia kifo cha Rais. Katiba imedhamiria mwendelezo wa maisha ya Serikali na nchi kwa ujumla. Pili, hakuna Ibara yoyote au hata sheria inayotamka bayana kuwa pindi Rais akifariki, basi Waziri Mkuu atakoma kuwa Waziri Mkuu, na Baraza la Mawaziri litavunjwa... HAKUNA. Aidha, Ibara ya 51, Ibara ndogo ya 3 haisemi kuwa Waziri Mkuu atakoma kuwa Waziri Mkuu kufuatia "kifo cha Rais". Kuegemea fasili (e) ya Ibara hiyo kuwa, "atakapoacha kushika kiti cha Waziri Mkuu kwa mujibu wa masharti mengineyo ya Katiba hii." ni kupotoka, kwasababu hakuna "masharti" au matakwa yaliyo bayana ndani ya Katiba ya eti kuwa, Rais akifariki, basi Waziri Mkuu atakoma kuwa Waziri Mkuu. Na kwa vyovyote vile, Katiba ya nchi ni lazima idhamirie utulivu na muendelezo wa shughuli za Serikali, na sio kuzisimamisha, au kuleta mkwamo au ugumu. Labda Mh. Rais wa TLS na Baraza lake warejeree upya hoja yao katika Mwongozo walioutoa kwa umma na waoneshe bayana sharti hilo ndani ya Katiba, la kwamba endapo Rais akifariki, basi Waziri Mkuu atakoma kuwa Waziri Mkuu.
Kwa maoni yangu, kwa mujibu wa Katiba ya JMT, kuna namna tatu za ujumla ambapo Waziri Mkuu anateuliwa... moja, ni mara tu baada ya uchaguzi mkuu na Rais kutangazwa na kushika madaraka yake, pili, ni pale Waziri Mkuu husika atakoma kuwa Waziri Mkuu kwa mujibu wa masharti yaliyoelezwa bayana na Katiba (kujiuzulu, kufariki, Rais akimuondoa, au atapigiwa kura ya kutokuwa na imani na Bunge), na tatu, Rais atakapomteua Mbunge mwingine kuwa Waziri Mkuu.
Nane, lakini ikumbukwe kuwa, katika masharti ya mamlaka ya Rais... bila kujali kuwa ni yule aliyechaguliwa moja kwa moja na wananchi, au yule aliyekuwa Makamu wa Rais na kisha kuapishwa kuwa Rais, kufuatia kifo cha Rais, Rais anayo mamlaka ya kuteua na kutengua uteuzi wa Mawaziri wote, ikiwemo Waziri Mkuu, wakati wowote atakapoona inafaa (Ibara ya 36, 51 na 55). Pengine sasa, ni kwa kutumia mamlaka yake katika Ibara hizi, Rais huyu wa sasa anaweza kufanya teuzi au kutengua teuzi mbali mbali kwa namna hiyo... na siyo eti, kwasababu ameshika madaraka yake kufuatia kifo cha Rais aliyemtangulia, yeye akiwa Makamu wa Rais... Ikumbukwe pia kuwa, kwa dhamiri ya Katiba ya JMT, Rais na Makamu wa Rais, kiutendaji ni ofisi moja ya Urais... Makamu wa Rais akichaguliwa pamoja na Rais, na yeye akiwa Msaidizi wa Rais.
Ni kwa mantiki hiyo, kwa maoni yangu, Mwongozo huu haupo sahihi, na umepotoka. Lakini kwa vile, kwa mujibu wa Sheria inayoanzisha TLS (Kifungu cha 4), TLS inao wajibu wa kuisaidia Serikali katika masuala yanayohusu Sheria, basi ingefaa Mh. Rais wa TLS na Baraza lake la Uongozi wakashauriana na Mh. Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhusiana na tafsiri sahihi ya suala hili, na au wakiona inafaa, wapeleke shauri la kikatiba Mahakama Kuu ili kupata tafsiri sahihi, kama inavyofaa; wakifanya hivyo na Mimi nitaomba kuingia katika shauri hilo nikiwa na maoni tofauti.
Katiba ni chombo kitukuka, kilicho hai, kinachoiongoza nchi hai, na kwa namna yoyote ile, hakipaswi kutafsiriwa ili kuleta mkanganyiko, mkwamo au ugumu wa uendeshaji wa nchi husika. Wakati wote, awali ya yote, ni purposive approach ndiyo hutumika kuisoma na kuitafsiri Katiba; na pale kweli panapokuwa na mkanganyiko, basi kanuni za misaada ya kutafsiri, kama vile harmonisation hutumika. Katika mazingira yetu ya sasa, hakuna ugumu huo, kwani Katiba iko wazi na bayana. Na ndiyo maana jana, tarehe 19 Machi, 2021, Mh. Rais, Samia Suluhu Hassan alikuwa sahihi kuendesha kikao cha Baraza la Mawaziri. Kikatiba, kinachomkabili sasa, ni yeye kushauriana na chama chake juu ya uteuzi wa jina la mtu anaempendekeza kuwa Makamu wa Rais, ambaye atapigiwa kura na Bunge kuthibitishwa. Na tunafahamu, chama chake tayari kimetangaza kuitisha kikao cha Kamati Kuu yao; na Mh. Spika kwa upande wake, ameshaliitisha Bunge mara moja. Utaona hapo, hicho nilichokuwa nakirudia hapo juu kuhusu mwendelezo wa maisha ya Serikali na nchi.
©️ Godwin Simba Ngwilimi, Wakili (Na. 948)
+255 756 871 669
godwinsimba1@gmail.com