Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, ameagiza kutenguliwa uteuzi wa viongozi 22 wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kutokana na kuonyesha udhaifu wa kiutendaji na kusababisha utekelezaji wa miradi ya maji kusuasua.
Viongozi hao ni mameneja 20 wa RUWASA ngazi ya wilaya, Meneja wa Wakala huo Mkoa wa Geita na Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa RUWASA, Deusdedith Magoma.
Akitoa taarifa ya uamuzi huo jana jijini hapa, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Anthony Sanga, alisema pamoja na mafanikio ya kuongezeka upatikanaji wa maji vijijini kutoka asilimia 64.9 hadi 72.3, imebainika kuwapo tatizo la kiutendaji linalochangiwa kwa kiasi kikubwa na baadhi ya viongozi.
"Udhaifu umejionesha zaidi wakati huu ambapo kasi ya utekelezaji wa miradi ya maji vijijini haiendani na mtiririko wa fedha na hasa zinazotolewa na washirika wa maendeleo," alisema.
Aliwataja viongozi hao kuwa ni Meneja wa RUWASA Mkoa wa Geita ambapo kasi ya utekelezaji wa miradi hairidhishi licha ya ufuatiliaji wa mara kwa mara unaofanywa na uongozi wa juu wa wizara na wakala huo.
Vilevile, alibainisha kuwa kwa ngazi ya wilaya, Waziri Aweso ameagiza uteuzi utenguliwe kwa viongozi 20 kutokana na miradi kusuasua kwenye Wilaya za Buhigwe, Uvinza, Mbulu, Musoma, Mbarali, Rungwe, Tandahimba, Nkasi, Kishapu, Bariadi, Songwe, Uyui, Misungwi, Magu, Bukoba, Babati, Igunga, Bunda, Ikungi na Newala.
"Waziri Aweso pia ameagiza Bodi ya Wakurugenzi wa RUWASA kuchukua hatua mara moja ya kuwatengua viongozi hao na kujaza nafasi zilizoachwa wazi kwa kuteua watumishi wa RUWASA walioonyesha bidii na umahiri mkubwa katika utekelezaji wa majukumu yao," alisema.
Aliagiza ujazaji wa nafasi hizo ufanyike ndani ya wiki moja ili kuhakikisha shughuli za wakala huo hazikwami.
Katika hatua nyingine, katibu mkuu huyo alisema Waziri Aweso amemteua Ndele Mwansanga kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi za Wakala huo. Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira jijini Mbeya.
"Waziri Aweso amemhamisha Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Iringa Mjini, Gilbert Kayange kwenda Mamlaka ya Mbeya Jiji na amemteua David Pallangyo kuwa Mkurugenzi wa Mamlaka Iringa," alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA, Clement Kivagalo, aliahidi kutekeleza kwa haraka agizo hilo la waziri ili kuimarisha Sekta ya Maji.
Alisema RUWASA imetia saini makubaliano kati yake na Idara ya Rasilimali Maji ya wizara hiyo, ili kuhakikisha tatizo la kutokuwa na vyanzo vya maji endelevu linapatiwa ufumbuzi mkubwa.
Chanzo: Ippmedia