- Tunachokijua
- Kumekuwepo na chapisho linalosambazwa na mtumiaji wa Facebook likidai kuwa wamiliki wa visima wanaosambaza maji kwa wengine wanapaswa kuanza kushitakiwa.
Chapisho hilo limewekwa kwenye ukurasa wa Kwinyara kwinyara lets talk likinukuu kauli inayodaiwa kutoka kwa Mhandisi Aron Joseph, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma.
Hata hivyo, kauli hiyo haikutolewa na mhandisi huyo alipokuwa akizungumza na chombo cha habari cha Clouds TV. Badala yake, chapisho hilo limehaririwa kwa lengo la kupotosha ujumbe halisi alioutoa wakati wa mahojiano.
Katika mahojiano hayo ambayo yalifanyika March 16 2026 Mhandisi Aron Joseph alieleza kuwa: “Kama mtu amechimba kisima cha maji, tumekuwa tukimsisitiza atumie yeye na familia yake, na asitoe huduma kwa watu wengine. Sababu ya kufanya hivyo ni kwamba wananchi wanaokuzunguka ambao ungependa kuwapatia maji, hasa wakati wa mgao, mara nyingi hatuhimizi hilo. Hii ni kwa sababu wengi wa wenye visima hawapimi ubora wa maji, na maji ya chini ya ardhi hubadilika sifa zake mara kwa mara."
"Leo yanaweza kuwa salama, lakini kesho yakabadilika; au maji yakachafuliwa kutokana na uvujaji kutoka kwenye choo cha jirani. Hivyo, ukianza kusambaza maji kwa watu wengine, unaweza kujikuta unasababisha madhara makubwa kiafya, hata kwa jamii nzima ya mtaa.”