BARUA KWA RAIS SAMIA SULUHU KUHUSU UFISADI KWENYE SUKARI
11 December 2021
Mheshimiwa Rais nakusalimu kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini ningependa badala ya kusema Kazi Iendelee basi uitikie haki, ustawi wa watu na uhuru wa kweli.
Mheshimiwa Rais nina mengi ya kukueleza kuhusu nchi yetu lakini leo ningependa kukueleza moja ambalo ni maombi yangu kwamba utalifanyia kazi ili kuitoa nchi yetu katika uchafu huu mkubwa. Jambo hili ni ulanguzi katika bei ya sukari na ufisadi mkubwa uliopo katika eneo la bidhaa muhimu (nipatapo wasaa nitakuandikia barua zaidi kuhusu bidhaa nyingine kama mafuta ya kula). Nakiri kwamba bei ya bidhaa hizi inachangiwa na mwenendo wa bei ya soko la dunia lakini pia inachangiwa na ufisadi uliopo katika soko la ndani.
Kwenye sukari tuna kundi dogo la wazalishaji nchini na hawa wana kikundi chao ambacho kisheria si sahihi (cartel). Kikundi hiki kiko chini ya Seif Ally Seif ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Superdoll (wamiliki wa Mtibwa na Kagera Sugar). Bei za sukari zinaweza kupandishwa kwa namna mbili, kwanza kwa kuamua kiasi gani cha sukari viwanda vya ndani vizalishe, maana yake hapa unaamua kiasi gani cha sukari kiwe kwenye maghala. Ukishaamua kiasi basi bei itapanda kuendana na kiasi. Maana yake ukiamua sukari uzalishe kidogo basi bei itapaa sababu bidhaa inakuwa chache na wahitaji ni wengi. Namna ya pili ni kushirikiana na watendaji walio serikalini kuhakikisha kwamba unapobana uzalishaji soko la ndani ili kuwe na uhaba na bei iwe juu basi serikali haitoi vibali kwa watu kuingiza sukari nchini sababu kwa kufanya hivyo uhaba hautakuwepo na bei unayotaka wewe itavurugika. Huo ndio mchezo unaochezwa Tanzania.
Ilikuwaje?
Mheshimiwa Rais zamani ilikuwa vibali kuagiza sukari nchini vinatolewa kwa kampuni yoyote inayofanya biashara ya vyakula na kukidhi vigezo lakini alipoingia madarakani Rais Magufuli kikundi hicho hapo juu kilimpotosha kwamba vibali vinauzwa kwa madalali (lengo likiwa wao wapewe nguvu hiyo ili waweze kuendelea kupangia wananchi wanyonge bei ya sukari). Bahati mbaya Rais Magufuli akakubaliana nao, akapitisha sheria kwamba atakayepewa kibali kuagiza sukari sharti awe mzalishaji wa sukari. Hapa Mheshimiwa Rais tukawa rasmi tumewapa kikundi hicho haramu nguvu zote mbili, ya kuamua kiasi gani wazalishe kwenye viwanda vya ndani na kiasi gani kiingie kutoka nje. Tukawa tumekamilisha lengo lao la kuamua bei ya sukari kwa wananchi badala ya soko kuamua. Kama si kundi hili haramu kuna uwezakano mkubwa sukari nchini isingezidi shilingi elfu mbili kwa kilo tofauti na ilivyo sasa.
Mchezo huu umechezwa kuanzia wakati wa Mwinyi, Mkapa, Kikwete, Magufuli (yeye kaurasimisha kabisa) na sasa wanasubiri kuona kama na wewe utaucheza.
Nani wahusika? Wahusika kwa sasa wa mchezo huu ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda, Waziri Jenista Mhagama na nduguye kwa jina la Alex Mhagama.
Hapa chini Majaliwa anaongea uongo huku akijua fika nini kinaendelea.
Mheshimiwa Rais huu mchezo hauumizi wananchi tu kwenye bei ya sukari lakini umeleta madhila makubwa kwa wakulima wadogo wadogo wa miwa na wengi wamerudi kwenye umaskini mkubwa. Unapokuwa na kundi linakaa na kuamua bei ya sukari maana yake linaamua kiwango cha uzalishaji, kiwango cha miwa na hata bei ya miwa. Imefikia mahali Mheshimiwa Rais huyo Seif anawaambia wananchi hamna la kufanya zaidi ya kuuza miwa kwa nusu bei. Yako maelfu ya ajira yanapotea katika mchezo huu haramu.
Mheshimiwa Rais, wakati Kikwete anaondoka madarakani alijaribu kutaka kuinasua serikali toka kwa mdomo huo wa mamba wa kilanguzi. Ukaandikwa mpango wa kuwa na shamba na miwa na kiwanda cha sukari cha serikali chini ya NSSF kule Mkulanzi (shamba) na Mbigiri (kiwanda). Magufuli akaingia madarakani akataka kuuendeleza mpango huo mzuri ila akatekwa na genge hilo hapo juu la wauza sukari chini ya Seif (Seif alimtumia Mkapa kumweka sawa Magufuli, naamini unazo taarifa kwamba Mkapa alikuwa mmoja ya wamiliki wa Kagera Sugar). Pale Kyaka nako Magufuli na Seif wana hekta zaidi ya elfu 60 wametumia pesa za serikali kusafisha shamba, njia na mitambo walitaka kujenga shamba lao la miwa na kiwanda cha sukari. Baada ya Magufuli kufariki sijui mpango ukoje. Hii habari ni ya siku nyingine, turudi kwenye hili la sasa.
Hao mabwana wakamuhakikishia Magufuli kupata chake, naye akaingia tamaa. Kwa kuanzia Magufuli akamtoa Profesa Godius Kahyarara pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaama akamuweka NSSF akijua Kahyarara angekuwa mtu wa YES tu ili kuhakikisha hicho kiwanda cha sukari cha NSSF hakisimami. Bahati mbaya au nzuri Kahyarara alikuwa mtu makini, akausoma mchezo huo wa ufisadi wa kimafia kwa nchi kupitia sukari na akakusudia kuhakikisha kiwanda cha NSSF kinakamilika.
Kahyarara akatangaza tenda pale NSSF kwamba anataka mitambo ya kuzalisha sukari kwa ajili ya kiwanda cha sukari Mbigiri. Kikundi kile cha mafia wa sukari kikaona kitumbua chao kitaingia mchanga. Ile tenda ilishindaniwa na kampuni mbili moja toka India (Isgec Heavy Engineering Ltd) na nyingine toka Ethiopia. Kampuni ya Ethipoia ilipenyezwa na hao mafia wa sukari na sababu walikuwa tayari wako karibu na Magufuli wakashinda tenda ila Magufuli akaifuta mwishoni. Hakuishia tu kuifuta tenda lakini pia akamuondoa Kahyarara kwa aibu NSSF akamrudisha UDSM na badala yake pale NSSF akamuweka mtoto wa shemeji yake Mkapa, bwana William Erio (rudi nyuma unganisha kwamba Mkapa ni mmoja ya wamiliki wa Kagera Sugar, mnufaika wa ulanguzi wa sukari na godfather wa Magufuli).
Wakati wa sarakasi zote hizo za kutaka kujikwamua kwa kuwa na kiwanda cha sukari cha nchi yetu pesa bado inaingia shambani kule Mbigiri na wakulima wadogo wadogo wanaendelea kulima wakijua mashine zitakuja, miwa watauza na maisha yataboreka. Wastaafu nao wanajua pensheni zao ziko salama na shirika linazifanyia uwekezaji mzuri. Kumbe nyuma ya pazia hayo ndiyo yanaendelea. Sijamaliza Mheshimiwa Rais, naomba kuendelea. Zaidi ya shilingi bilioni 500 zimeingia kwenye kuandaa shamba Mkulazi, kulima na miundombinu shambani na kiwandani na hakujazalisha hata kilo moja ya sukari. Mheshimiwa hizi ni pesa za wastaafu. Leo hii kila ofisi ya NSSF malipo ni shida nadhani sasa wananchi wataanza kujua nini kinaendelea kwenye huo mfuko.
Baada ya Magufuli kufuta tenda ile akawaagiza TANROADS kuichukua tenda na kununua mashine zile za kiwanda cha sukari kwa niaba ya NSSF. TANROADS chini ya swahiba wake Magufuli, marehemu Mfugale wakachukua dola milioni 5 toka NSSF karibu bilioni 11 (ikabaki bilioni 169) wakaipa kampuni moja toka Malaysia inaitwa Kay Bouvet Engineering Ltd na hadi ninapokuandikia barua hii ndefu hakuna mashine iliyofika Tanzania. Narudia tena hizi ni pesa za wastaafu mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais hao Kay Bouvet wana wakala wao raia wa Sudan ambaye hapa chini naye ana wakala wake anaitwa Alex Mhagama (ndugu yake Waziri Jenista Mhagama).
Wakati mpango unaendelea wa kuchelewesha mashine na kuchezea hela za NSSF kama hivyo, Magufuli akafirki dunia. Haraka haraka Mfugale akatuma hela iliyobakia kwenda Malaysia, yani bilioni 169. Hayo malipo yalipata baraka za Waziri Mkuu Majaliwa na yeye alipewa shilingi bilioni 4.6.
Ulipoingia madarakani ninafahamu uliuliza mashine za kiwanda cha sukari cha NSSF Mbigiri kwa miwa ya shamba la Mkulanzi iko wapi na Majaliwa akasema ziko bandarini. Uongo mtupu Mheshimiwa na vyombo vyetu ya ulinzi na usalama vinajua naamini vitakupa mkeka wote.
Katika hizi sarakasi zote Mheshimiwa najua unajiuliza kina nani wanafaidika kwa kiasi kikubwa kwa maumivu ya bei kubwa ya sukari kwa wananchi? Katika ile bilioni 180 kuna watu wana pasenti zao ndani ya fedha hizo. Hapa Mheshimiwa ndipo nakuletea Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Waziri Jenista Mhagama, Profesa Adolf Mkenda (huyu aliona yaliyomtokea Kiharara akaona bora asalimu amri na yeye akinge bakuli) na Alex Mhagama (ndugu yake Jenista).
Mheshimiwa ulanguzi huu kwa wananchi ili kuneemesha kikundi kidogo ni dhambi kubwa. Ukichelewa watakuzunguka na kusema wewe ndiye unataka kutoa vibali huku wakificha ukweli kwamba vibali wanapeana wao kwa mkakati huku wakihodhi uzalishaji wa ndani na kuhakikisha bei ya sukari kwa mlaji wa mwisho inabaki kama wanavyotaka wao. Hii ni dhulma na dhambi kubwa sana. Bei ya sukari Tanzania inawapa faida zaidi ya asilimia mia moja, huu ni moto Mheshimiwa Rais mbele ya Allah kama ukiamua kulea mfumo huo.
Huko kote sijagusa kodi ambazo hicho kikundi cha mafia kinapewa nafuu na misamaha kwa kuwaweka hao watendaji mifukoni hadi bodi ya sukari. Tukiweza kusimamia vizuri sekta hii hapa nchini Mheshimiwa Rais utapata thawabu kubwa kwa mwenyezi Mungu lakini utaziba mianya ya dhulma na kupotea kwa kodi. Tanzania sekta ya sukari ingeweza kuleta faida ya zaidi ya dola milioni 200 kwa mwaka, yani tungeweza kujenga barabara hizi za lami Dar hadi Dodoma kila mwaka kwa pesa za ndani au kujaza madawa na wataalamu katika hospitali zetu bila shida yoyote. Ila kwa sasa wanakula wachache kwa machungu ya mamilioni ya watu kama hivyo.
Wakati mwingine nitakuandikia kuhusu Mbowe, ndege, mafuta ya kula, dizeli, petroli, mafuta ya taa, bwawa la Mwalimu Nyerere, na kadhalika. Nakuombea kheri nyingi uweze kuitoa nchi yetu katika makucha haya.
Mchambuzi zaidi ya habari
www.mchambuzi.com