Unaposema kabila katika uwanda wa
mwambao wa pwani lugha halisi ni
kiswahili lakini tofauti ni lahaja kwa
unguja kuna
kiunguja,kihadimu,kipemba bara huku
kuna kimtangata, kimrima, kiamu nk.
Kuna wengi suala la mabila hasa ya
wenyeji wa mwambao hawaelewi
pengine maelezo yafuatayo yatatoa
mwanga:-
Swahili ni Taifa la makabila yaliopo
katika Pwani ya Afrika ya Mashariki na
visiwa vyake tokea Barawa hadi Sofala.
Baadhi ya makabila hayo ni
Wabarawa, Wapate, Waamu,
Wagiriama, Wadigo, Waduruma,
Wakauma, Wakambe, Wachoni,
Warabai, Waribe, Wajibana,
Wakilindini, Wajomvu, Wamtwapa,
Wachangamwe, Watangana, Wamvita,
Wapokomo, Wavanga, Wamakunduchi,
Wapemba na Wangazija. Kabila hizi
zote zilikuwa zikizungumza lugha
ilokuwa ikijulikana kama Kingozi. Hata
hivyo, makabila yote haya yalikuwa na
ndimi (dialect) zao na miji yao; baadhi
yao bado wangali na ndimi zao na miji
yao. Ndimi zote hizi zina ukhusiano au
ukuruba mkubwa wa maneno na
maana zake. Kwa mfano, utakuta
kwamba kuna ukuruba fulani baina ya
Kipemba na Kiamu.
Kila kabila ina ndimi yake, dasturi
zake, mila zake, tungo zake, na
kadhalika. Haya yote ni kabla ya
Waarabu na Washirazi hawajaanza
kuhamia kimaisha katika Pwani ya
Afrika ya Mashariki - takriba karne
nane hadi kumi zilizopita (yaani baina
ya miaka 800 hadi 1000).
Washirazi hawakuathiri mno mila,
dasturi, mapisi, na lugha hiyo ya Watu
wa Pwani. Waarabu ndiyo walioathiri
sana, khususa Makabila ya Kati na
Kati (kwa mfano, Wamvita, Watangana
na Wakilindini). Makabila haya
yaliathirika mno hadi ya kuwa majina
haya yalipotea na ndimi zao za kiasili
zilipotea vilevile. Ndimi ambazo bado
zipo ingawa zimeazima maneno fulani
ya Kiarabu (kama ambavyo pengine
Kiarabu kimeazima kutoka Lugha ya
Kingozi) ni ndimi za kaskazini na zile
za kusini.
Ndimi za Kaskazini ambazo bado zipo
na wenyewe wanatambuliwa ni kama
vile Kibarawa, Kiamu, Kipokomo, na
kadhalika. Ama Ndimi za Kusini
ambazo hazikuathiriwa mno ni
Kingazija, Kimakunduchi, Kipemba na
Kivanga. Ndimi za Kati na Kati ambazo
bado zikalipo ni kama vile, Kigiriama,
Kiduruma, Kijibana; hizi ni miongoni
mwa kabila ambazo leo zajiita au
zatambuliwa kama Mijikenda (yaani
miji tisia).
Utakuta ya kuwa katika makabila ya
kati na kati, yale ambayo
hayakuathiriwa sana ni yale ambamo
watu wake hawakuwa Waislamu. Na
ndiyo maana mpaka hii leo utaona ya
kuwa makabila ya Mijikenda
(isipokuwa Digo), ni makabila ambayo
wengi katika watu wake si Waislamu.
Hii ni kwa sababu makabila kama ya
Mvita, Tangana na Changamwe
hayakujitahidi au kujishughulisha
kufanya usambazaji wa Risala ya U-
Islam kwa makabila haya; Waarabu
piya walipokuja hawakuwa na lengo
hilo la kuingia vijijini kufanya Dawah.
Lengo lao kubwa ilikuwa ni biashara.
Kama tujuavyo U-Islam ulifika
Kaskazini Mashariki mwa Bara la
Afrika kabla haujafika katika sehemu
nyengine za bara Arabu kama vile,
Yemen, Omani na hata katika mji wa
Madina na sehemu nyingi za nchi
tunayoijua leo kama Saudi Arabia.
Yaani U-Islam ulifika Abisinia (Ethiopia
ya leo) katika mwaka wa 615, miaka
mitano tu baada ya Mtume Muhammad
(s.a.w.) kupewa risala (610). Mtume
alizaliwa mwaka wa 570. Ingawa wale
Waislamu waliokuja kuomba hifadhi
Abisinia walikwenda zao Madina baada
ya kutawazwa kwa serikali ya kwanza
ya Islam mwaka wa 623 (huu ni
mwaka wa kwanza wa Hijria),
walikuwa washawasilimisha watu
kadha wa kadha (akiwemo Mfalme
wao, Najash); hii ndiyo ilikuwa ni
sababu ya kuanza kusambaa kwa U-
Islam katika bara la Afrika. Kwa hivyo
ni muhimu kutambua na kuamini ya
kuwa makabila fulani ya Afrika ya
Mashariki yalisilimu kabla ya kuja kwa
Waarabu hawa tuwajuwao leo,
waliokuja kwa biashara katika pwani
ya Afrika ya Mashariki kutoka Yemen,
Omani, na kadhalika.
Na khususa ni Waarabu hao wa Yemen
na Omani ndiyo waloowana na baadhi
ya hao Wangozi, au wanaojulikana leo
kama Waswahili. Kwa hivyo, baadhi ya
Waswahili wana damu za Kiarabu na
baadhi yao hawana damu ya Kiarabu.
Katika dasturi za Kizungu za kufuata
ukoo, mtu anapotanganya tu damu na
asekuwa Mzungu, basi azaliwae katika
mtanganyiko huo katu hakubaliwi
kuwa ni Mzungu. Na ndiyo twaona ya
kuwa ingawa kuna asili mia thalathini
(30%) ya Wamarekani Weuse (African-
Americans) ndani ya Marekani, lakini
wanasibishwa na U-Afrika na U-weuse
(Blacks) pekee, na katu hawanasibishwi
na uzungu. Kwa Waarabu nao ni rahisi
zaidi kunasibishwa na taifa hilo ikiwa
mtu lugha yake ya kwanza ni Kiarabu.
Ama kwa Waswahili tukati na kati,
yaani aghlabu mtu hunasibishwa na
Uswahili kwa lugha na asili. Kwa hivyo
leo wako baadhi ya Waswahili wenye
damu za Kiarabu ambao wametagua,
kwa sababu mbalimbali, kujinasibisha
zaidi na U-Arabu kuliko U-Afrika;
kadhalika, kuna baadhi yao, kwa
sababu moja au nyengine, wameamua
kujinasibisha zaidi na U-Afrika kuliko
U-Arabu.