Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam KIPA Ally Mustafa ‘Barthez' anaweza kupumzishwa katika mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baina a timu yake na Rhino Rangers ya Tabora, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mechi tisa alizodaka Barthez hadi sasa, amefungwa mabao 11 na inaonekana kudaka mfululizo tangu msimu uliopita kunamchosha na bila shaka Deo Munishi ‘Dida' atasimama langoni kwa mara ya kwanza kesho katika Ligi Kuu tangu asajiliwe na Yanga msimu huu kutoka Azam.
Kwa ujumla, kocha Mholanzi Ernstus ‘Ernie' Wilhelmus Johannes Brandts anatarajiwa kufanya marekebisho makubwa katika safu yake ya ulinzi kesho baada ya matokeo ya sare ya 3-3 na wapinzani wa jadi Simba SC Jumapili, Uwanja wa Taifa, wakitoka kuongoza 3-0 hadi mapumziko.
Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro' anaweza kuanzia benchi, wakati Juma Abdul ataenda beki ya kulia kuchukua nafasi ya Mbuyu Twite, atakayehamia katikati kucheza na Kevin Yondan.
Kuna uwezekano pia wakongwe Athumani Iddi ‘Chuji' na Haruna Niyonzima nao wakapumzishwa ili ‘kuweka akili sawa' baada ya sare isiyotarajiwa mwishoni mwa wiki na Frank Domayo akatengeneza safu ya kiungo kwa pamoja na Salum Telela au Hamisi Thabiti.