Mnamo Mei 2017 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilitaarifiwa kukamatwa kwa Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya jamii Forums, ilitolewa na afisa Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SSP Ramadhan Kindai iliyotokana na kinachodaiwa kwamba mkurugenzi mtendaji wa Jamii Forum, Maxence Melo na Mwanahisa wa Kampuni hiyo, Mike William kushindwa kutoa taarifa sahihi iliyochapishwa kwenye mtandao wa Jamii Forums.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Mohamed Salum, Kindai alidai kuwa waliomba taarifa kutoka kwenye kampuni ya jamii Forums kutokana na kesi iliyofunguliwa na Afisa Msimamizi wa Mauzo ya rejareja wa Oil Com, Usama Mohammed. Kwamba Usama alifika kwenye ofisi yao na kulalamika kuwa Februari 13,2016 kuna habari ilichapishwa kwenye mtandao wa Jamii Forums kuhusu kampuni ya Oil Com kukwepa kodi bandari ya Dar es Salaam na kwamba wanaiibia serikali.
Katika kufuatilia kupata ukweli, ASP Fatuma Kigondo aliingia kwenye mtandao huo kutafuta aliyechapisha taarifa hizo ambapo waligundua kuwa ni Fahara JF Expert member ndiye aliyechapisha taarifa hiyo.
Kufuatia hayo, Februari 23, 2016 Kigondo aliandika barua kwenda kwa Mkurugenzi wa Jamii forums ili awapatie taaarifa za mtu huyo ambapo walipokea barua toka Jamii Forums ikidai kuwa wanahaki ya kulinda faragha za wateja wao.