Uhusiano kati ya Ukristo na upagani
Katika kuhalalisha dini yake hiyo ya Ukristo, Bwana Paulo aliibua madai mazito kuwa ametokewa na Bwana Yesu na kumtuma aende kwa watu wa mataifa (wapagani) kuwapelekea dini (neno la Mungu)!
Uthibitisho wa hilo tunaupata katika maelezo yake (Paulo) yafuatayo kama alivyokaririwa na Biblia tukufu:
"Basi katika kazi hiyo nilipokuwa nikienda Dameski, mwenye mamlaka na maagizo ya wakuu wa makuhani; Ee Mfalme, ndipo wakati wa adhuhuri njiani naliona nuru inatoka mbinguni ipitayo mwangaza wa jua, ikinimulikia mimi, na wale waliofutana nami pande zote. Tukaanguka chini sote, nikasikia sauti ikisema nami kwa lugha ya Kiebrania, Sauli! Sauli! Mbona waniudhi? Ni vigumu kwako kumpiga mateke mchokoo. Nami nikasema, Wewe U nani, Bwana? Bwana akaniambia, Mimi ni Yesu, ambaye wewe unaniudhi. Lakini inuka, usimame kwa miguu yako, maana nimekutokea kwa sababu hii, nikuweke wewe uwe mtumishi na shahidi wa mambo haya uliyoyaona, na wa mambo ambayo katika hayo nitajidhihirisha kwako; nikiuokoa na watu wako, na watu wa mataifa ambao nakutuma kwao; uwafumbue macho yao, na kuwageuza waiache giza na kuelekea nuru, kumwelekea Mungu; kisha wapate msamaha wa dhambi zao, na urithi miongoni mwao waliotakaswa kwa imani iliyo kwangu mimi". (Matendo ya Mitume 26:12-18).
Madai hayo ya Bwana Paulo ya kwamba katumwa na Bwana Yesu (a.s.) aende kwa watu wa mataifa kuwapelekea neno la Mungu, kimsingi hayakubaliki. Kwa sababu Bwana Yesu (a.s.) hana sifa ya kukiuka kauli zake mwenyewe zifuatazo:
"Hao thenashara Yesu aliwatuma, akawaagiza, akisema, katika njia ya mataifa msiende, wala katika mji wowote wa Wasamaria msiingie. Afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Lakini watakapowafukuza katika mji huu, kimbilieni mwingine; kwa maana ni kweli nawaambia, Hamtaimaliza miji ya Israeli, hata ajapo mwana wa Adamu". (Mathayo 10:5-6,23)
Akajibu, akasema, Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli". (Mathayo 15:24)
Aidha, maadai hayo ya Bwana Paulo, pia hayakubaliki kwa sababu kumwepusha mbali Bwana Yesu (a.s.) na sifa hatari ya kukiuka mipaka ya kazi yake aliyowekewa na Mungu kabla hata mwenyewe (Yesu a.s.) hajazaliwa, kama maandiko yafuatayo yanavyothibitisha ukweli huu:
"Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale tangu milele". (Mika 5:2)
"Nawe Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, Hu mdogo kamwe katika majumba ya Yuda; Kwa kuwa kwako atatoka mtawala Atakayewachunga watu wangu Israeli". (Mathayo 2:6)
Kinyume na dai lake hilo, ukweli wa mambo unaonyesha kuwa Bwana Paulo alikwenda kwa watu wa mataifa (wapagani) kufuata dini yao, kama yeye mwenyewe asemavyo hapa chini:
"Lakini Kefa alipokuja Antiokia, nalishindana naye uso kwa uso, kwa sababu alistahili hukumu. Kwa maana kabla hawajaja watu kadhaa wa kadhaa waliotoka kwa Yakobo, alikuwa akila pamoja na watu wa mataifa; lakini walipokuja wao, akarudi nyuma akajitenga, huku akiwaogopa waliotahiriwa. Na hao Wayahudi wengine wakajigeuza pamoja naye, hata Barnaba pia akachukuliwa na unafiki wao. Walakini, nilipoona ya kuwa njia yao haiendi sawa sawa na ile kweli ya Injili, nalimwambia Kefa mbele ya wote, Ikiwa wewe uliye Myahudi wafuata desturi za mataifa, wala si za Wayahudi, kwanini unawashurutisha mataifa kufuata desturi za Wayahudi? Sisi tulio Wayahudi kwa asili, wala si wakosaji wa mataifa, hali tukijua ya kuwa mwanadamu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria, bali kwa imani ya Kristo Yesu; Sisi tulimwamini Kristo Yesu ili tuhesabiwe haki kwa imani ya Kristo, wala si kwa matendo ya sheria; kwa maana kwa matendo ya sheria hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki. Lakini ikiwa sisi wenyewe, kwa kutafuta kuhesabiwa haki katika Kristo, tulionekana kuwa wenye dhambi, Je! Kristo amekuwa mtumishi wa dhambi? Hasha! Maana nikiyajenga tena yale niliyoyabomoa, naonyesha ya kuwa mimi mwenyewe ni mkosaji. Maana mimi kwa njia ya sheria naliifia sheria ili nimwishie Mungu". (Wagalatia 2:11-19)
Maelezo yake hayo juu, yanaonyesha jinsi Bwana Paulo alivyokuwa akimshutumu Kefa (Petro), Barnaba na Wayahudi wengine alipokutana nao huko Antiokio (kwa watu wa mataifa) kwa kutofuata kwao moja kwa moja desturi za watu wa mataifa (wapagani) kama walivyokuwa wakifanya hivyo hapo awali, kabla Wayahudi waliotoka kwa Yakobo (Myahudi) hawajaja.
Aidha, Bwana Paulo anaonekana pia hapo akimlaumu Kefa (Petro) kwa kitendo chake cha kuwashurutisha watu hao wa mataifa, yaani wapagani kufuata desturi za Wayahudi (yaani kufuata Torati ya Nabii Musa) akidai kwamba mwanadamu hatohesabiwa haki kwa matendo ya sheria; lakini kwa imani ya Kristo Yesu! Kwa maelezo yake hayo, ni wazi kuwa Bwana Paulo, Petro na wenzio wao wote yaonyesha dhahiri kuwa hawakwenda kwa watu wa mataifa huko Antiokia kwa jambo lingine lolote ila kufuata desturi za dini yao. Na kama tulivyoona hapo awali, dini yao hii watu hao wa mataifa (wapagani) ilikuwa ina miungu yao (Zeu na Herme) yenye desturi ya kujigeuza kuwa mfano wa wanadamu.
Pia ilikuwa na ibada zake wanazoifanyia miungu yao hiyo.
Kwa hali hiyo basi, kwa kuwa Bwana Paulo anafuata mia kwa mia desturi za dini ya watu wa mataifa, yaani wapagani, hapana shaka ni lazima pia huo ndio utakaokuwa msimamo wa dini yake ya Kikristo, kama tutakavyokuja kuona kwa urefu zaidi baadaye, In sha Allah.