Mkuu
Gavana labda nikuongeze kwenye huo mstari wa 14(wengine) kwamba na wewe unamuita mtume."""ila Yupo aliejibu kwa ufasaha zaidi(Petro)
Katika Injili za Mathayo, Marko na Luka, Yesu ameitwa mara 22 kwa jina la "Mwana wa Mungu",
lakini hata mara moja yeye mwenyewe hakujiita kwa jina hilo.
Katika Mathayo 27.43 yanatajwa maneno ya wakuu wa makuhani wa Kiyahudi pamoja na waandishi na wazee waliokuwa wakimdhihaki, si maneno yake yeye Yesu.
Hao walikuwa wakimzulia kuwa anadai uwana wa Mungu, na anadai kuwa ni Mfalme wa Israeli.
Mara nyingi waliokuwa wakimwita Mwana wa Mungu walikuwa ama wendawazimu, wenye pepo wachafu, au askari wa Kirumi ambao tokea hapo wao ni washirikina, mapagani.
Ama mwenyewe Yesu alikuwa daima akipendelea kujiita mwana wa Adamu kwa Kiebrani, lugha yake, Bin Adam, yaani ni binaadamu, mtu tu.
Katika Injili, jina hili la Yesu kuitwa mwana wa Adamu limetajwa yapata mara 80.
Makhasimu zake wa Kiyahudi walimzulia kuwa alidai kuwa ni Mfalme wa Mayahudi ili kumchongea kwa watawala wa Kirumi, na kuwa alidai kuwa ni Mwana wa Mungu ili apate kuchusha kwa Mayahudi.
Majina haya, basi, ya "mungu", "mwana wa mungu" na "Bwana" kwa kuwa yalikuwa yameenea na maarufu katika nchi za bahari ya Kati (
Mediterranean) katika zama za Yesu haiwezi kukosa kuathiri mawazo ya watu ambao bado haijawavaa imani ya Mwenyezi Mungu Mmoja kama ilivyokuwa ikifunza dini ya Kiyahudi.
Majina kama hayo yalikuwa yakitumiliwa ovyo na kila mtu takriban.
Na hizo hadithi za watu kama hao, ikiwa ni watu wa hadithini tu si wa kweli kweli, au watu walioishi kweli kweli duniani, zimefanana mno na hizo ambazo khalafu yake zikaaminiwa na Wakristo kuwa zimemkhusu Yesu Kristo peke yake.
Tukirejea kuyanukulu yaliyomo katika Biblia tunamwona Yesu mahkamani alikataa kukiri mashtaka aliyoshtakiwa kuwa yeye alidai kuwa ni Mwana wa Mungu, kama wendawazimu na mapagani walivyokuwa wakimuenezea: Kisha Kuhani Mkuu akasimama akamwambia, Hujibu neno? Hawa wanakushuhudia nini? Lakini, Yesu akanyamaza. Kuhani Mkuu akamwambia, Nakuapisha kwa Mungu aliye hai, utuambie kama wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu. Yesu lakini nawaambieni, Tangu sasa mtamwona Mwana wa Adamu ameketi mkono wa kuume wa nguvu, akija juu ya mawingu ya mbinguni.
------Mathayo 26.62-64
Injili tatu za Mathayo, Marko na Luka (ambazo zimefanana) hazimtaji kabisa Yesu kuwa ni Mwana "Pekee" wa Mungu. Ni Injili ya Yohana tu ndiyo iliyokazania kumpa ungu Yesu na kumwita Mwana Pekee wa Mungu. Injili ya Yohana inasema:
Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.
-------Yohana 1.14
Lugha ya Yohana ni ya namna ya peke yake.
Injili tatu za mwanzo, Mathayo, Marko na Luka zinamweleza Yesu ni binaadamu.
Lakini hata kulitumia neno "Mwana wa Mungu" kuna maana gani hasa?
Tukiipitia Biblia na kufungua sahifa zake tutaona kuwa jina hilo limetumiliwa kwa watu wengi licha Yesu.
Katika Agano la Kale ambalo lote limeandikwa hata kabla ya Yesu hajazaliwa tunakuta mifano kama hii:
Ikawa wanadamu walipoanza kuzidi usoni pa nchi na wana wa kike walizaliwa kwao,wana wa Mungu waliwaona hao binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri; wakajitwalia wake wo wote waliowachagua.
---Mwanzo 6.1-2
Misingi yake ilikazwa juu ya kitu gani? Au ni nani aliyeliweka jiwe lake la pembeni, Hapo nyota za asubuhi zilipoimba pamoja, Na wana wote wa Mungu walipopiga kelele kwa furaha?
-----Ayubu 38.6-7
Tena itakuwa ya kwamba hesabu ya wana wa Israeli itafanana na mchanga wa bahari, usioweza kupimwa wala kuhesabiwa; tena itakuwa, badala ya kuambiwa, Ninyi si watu wangu, wataambiwa, Ninyi ndio wana wa Mungu aliye hai.
-----Hosea 1.10
Ni dhaahiri tunaona ilikuwa ni jambo la kawaida hata kwa waandishi wa Kiyahudi wanaoamini Mwenyezi Mungu mmoja kutumia maneno kama "wana wa Mungu" kwa kukusudia "vipenzi vya Mungu", au "waja wa Mungu", yaani watu wema.
Mwanachuoni wa Biblia wa Kitaliana, Marcello Craveri, aliyeandika kitabu chake, Maisha ya Yesu (
The Life of Jesus), anaamini kuwa neno hilo "Mwana wa Mungu" limegeuka maana kwa kupitiwa na miaka ya makosa ya kufasiri. Ameandika:
"Kwa hakika, Agano la Kale limetumia neno ebed Yahweh, ambalo maana yake ni 'mtumishi wa Mungu', 'mtumwa wa Mungu', 'khaadimu wa Mungu'. Matini ya Kigiriki ya Septuagint imeipa tafsiri ambayo yaweza kuwa na maana mbili, (Pais Theou), hali ya kuwa pais, kama neno puer laweza kuwa maana ya 'mvulana mdogo' au 'mtumwa'. Baada yake ilikuwa ni wepesi kuliondoa neno pais lenye maana ya 'mvulana' likatiwa neno (hyos)ambalo maana yake ni 'Mwana'."
Lugha ya Kiyahudi ya Kiebrani na lugha ya Kiarabu zina asli moja. Mfano wa hayo ni kama mathalan kutumia neno la Kiarabu Abd kama katika "
Abdu-Llahi" kwa maana ya "Mtumwa wa Mwenyezi Mungu",na likaja baadae kugeuzwa na kubuniwa neno
"
Ghulam" ambalo lina maana ya "Mtumishi" na vile vile "Kijana". Na khatimaye likatumiwa neno "
Ibn" ambalo maana yake ni "Mwana" tu.
Hii ndio shida inayompata mtu ye yote anapotaka kujua hakika ya mafunzo ya Kikristo.
Hapana kitabu cho chote duniani chenye asili ya matamshi yake Yesu wala wanafunzi wake.
Wao wakisema Kiaramia, lugha ya mazungumzo zama zile huko Palastini, kama ilivyo lugha ya Kiswahili kwetu.
Na lugha yao ya dini ni Kiebrania, kama ilivyo lugha ya Kiarabu kwa Waislamu po pote pale walipo, au Kilatini kwa Wakatoliki.
Injili zote ziliopo hapana hata moja iliyoandikwa na kubaki katika lugha ya Kiebrania ya asli, ambayo tungeweza kuirejea tupate ukweli wa kauli za Yesu.
Ziliopo zote ni tafsiri za Kigiriki.
Injili za Kiebrania ziliamrishwa zote zichomwe moto.
Hiyo ni amri ya Wazee wa Kanisa, na ye yote aliyeonakana nayo hukumu yake ilikuwa kifo.
Inakubaliwa pia kuwa Injili zote zimeandikwa miaka mingi baada ya Yesu kwisha ondoka duniani, na zimeandikwa na watu ambao hawakumwona bali ni kwa kufuata masimulizi waliyoyasikia. Na ziliopo ni tafsiri, na tafsiri za tafsiri.
Yesu hakusema maneno yake kwa Kiswahili, wala Kiingereza, wala Kilatini wala Kigiriki. Kama si kwa Kiebrania basi akifunza kwa lugha iliyofanana nayo, nayo ni Kiaramia.
Hata bila ya ubabaishi wa tafsiri ni jambo la hakika kuwa katika maandishi ya vitabu vya Biblia hili neno "mungu" likitumiwa ovyo. Tunasoma katika Agano la Kale Mwenyezi Mungu anamwambia Musa vipi yatavyokuwa makhusiano yake na nduguye Haruni:
Naye (Haruni) atakuwa msemaji wako kwa watu, hata yeye atakuwa mfano wa kinywa kwako, nawe (Musa) utakuwa mfano wa Mungu kwake.
---Kutoka 4.16
Angalia tena isemavyo Zaburi:
Mimi nimesema, Ndinyi miungu, Na wana wa Aliye juu, nyote pia.
---Zaburi 82.6
Utumiaji ovyo ovyo maneno hayo matakatifu kama "Mungu" au ya kufuru kama "mwana wa Mungu" yaliyotumiwa na waandishi wa Biblia yaonyesha wazi vipi imani na agano la Ibrahimu na Manabii wengine walilofungamana kwalo na Mwenyezi Mungu lilivyopotoshwa.
Mayahudi ambao kumshirikisha Mwenyezi Mungu na cho chote ni mwiko walishawishiwa na watawala wao na makafiri waliokuwa wakikaa nao kutumia lugha na maneno ya kikafiri bila ya wenyewe kutambua. Sisi tunaona vipi hii leo tulivyoharibiwa hata Kiswahili chetu na watawala ambao mila na dini zao ni mbali na yetu.
Tunaona vipi maneno kama "Halali na Haramu" yalivyopotoshwa hata imekuwa yanatumiwa kuwa ni kilichoruhusiwa au kukatazwa na serikali au chama kinachotawala, wala sio kama ilivyo asli kuwa alichohalalisha na kuharimisha Mwenyezi Mungu. Tunasikia inasemwa kuna pombe ya "halali", yaani inayoruhusiwa na serikali.
Tunasikia kuna majumba au mashamba yaliyopokonywa (kughusubiwa) na serikali yanaambiwa ati "yametaifishwa" kihalali. Na ilhali hapana unyan'ganyi, au wizi wa halali. Yote ni haramu.
Hata hili neno "sharia" limepotoshwa pia. Sharia ni sharia ya Kiislamu tu. Ya Serikali ni "Kanuni" si sharia. Sharia ni ya Mwenyezi Mungu. Makosa anayoyafanya mcheza mpira (faul) sasa yanaitwa: Dhambi.
Ni namna hivyo basi waandishi wa Biblia wa Kiyahudi ambao walikuwa wakimuamini Mwenyezi Mungu mmoja waliikoroga lugha yao kwa kuwa maneno ya kikafiri ya watawala wao wa kipagani wa Kirumi na jirani zao mapagani wa Kigiriki, wa Kimisri na wengineo waliokuwa katika pande zile za mashariki ya Bahari ya Kati (
Mediterranean Sea) yaliwaathiri hata wao wakawa wanayatumia kama jambo la dasturi.
Niliyokwisha kuyanukulu ni maneno ya kutokana na sehemu ya Biblia iitwayo
Agano la Kale, yaani ile sehemu iliyoandikwa kueleza mambo ya Manabii waliokuwa kabla ya Yesu. Hebu tuangalie sasa yaliyosemwa na Agano Jipya lilioandikwa baada ya Yesu.
Luka anatusimulia katika Injili yake alivyohubiri Yesu:
Bali wapendeni adui zenu, tendeni mema, na kukopesha msitumaini kupata malipo, na thawabu yenu itakuwa nyingi; nanyi mtakuwa wana wa Aliye juu, kwa kuwa yeye ni mwema kwa wasiomshukuru na waovu.
---Luka 6.35
Hapo twaona Yesu anawaambia wafwasi wake kuwa katika malipo ya watendao mema na kuwapenda maadui zao ni kuwa watakuwa "wana wa Aliye juu" yaani Mwenyezi Mungu. Katika Injili ya Mathayo Yesu anasema:
Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu
-----Mathayo 5.9
Hata Paulo naye amesema katika barua yake aliyowapelekea Warumi:
Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu.
-----Warumi 8.14
Yohana na Paulo ndio wakubwa wa kumfanya Yesu ni Mungu, au mwana wa Mungu, lakini hata wao wametoa ushahidi wa kutosha kuwa huo "uwanamungu" wa Yesu ndio ule ule kama walio nao wote walio wema.