Tuesday, 19 April 2011 19:23 newsroom
*Mwanchama mwingine ajitolea kumrejesha Ngasa
Na Mwandishi Wetu
MFADHILI wa zamani wa klabu ya Yanga,Yussuf Manji, amemwaga kitita cha sh. milioni 100 kusaidia usajili wa wachezaji msimu ujao. Habari za uhakika zilizopatikana kutoka klabu hiyo, zimesema Manji alikabidhi fedha hizo wiki iliyopita. Kwa mujibu wa habari hizo zilizothibitishwa na kiongozi moja wa Kamati ya Usajili ya Yanga, fedha hizo zimeshaanza kutumika kwa kazi iliyokusudiwa.
"Kamati ya Usajili imeanza kutumia pesa hizo kwa kuwasajili wachezaji wapya na wengine wa zamani, watakaoichezea timu hiyo msimu ujao."Habari hizo zimeeleza kati ya wachezaji ambao wametua Jangwani baada ya kutolewa pesa hizo, ni kipa wa Majimaji, Said Mohamed na Nurdin Bakari. Bakari alimaliza mkataba wake wa kwanza na Yanga na hivi karibuni ameingia mkataba mpya wa miaka miwili na klabu hiyo, na kuzima ndoto za Azam kumpata mchezaji huyo.
Manji ametoa pesa hizo akiwa mwanachama wa klabu hiyo kongwe na sio kama mfadhili, baada ya kujitoa kuifadhili hivi karibuni.
Habari zaidi zimesema mwanachama mwingine wa klabu hiyo, amejitolea kutoa pesa zote za kuilipa timu ya Azam, imwachie mshambuliaji Mrisho Ngasa arejee kuichezea timu hiyo ya Jangwani.
Mwanachama huyo (jina tunalo) ambaye hakutaka jina lake litangazwe, amekubali kutoa pesa zitakazowezesha Azam kumwacha Ngasa, aichezee tena Yanga katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mwakani.
Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga, alipoulizwa jana juu ya masuala hayo, alikiri kuwepo mipango ya kutaka kumrejesha Ngasa ingawa hakuwa tayari kuzungumzia zaidi jambo hilo.
Ngasa alitua Azam mwanzoni mwa msimu uliomalizika hivi karibuni kwa uhamisho wa kitita cha karibu sh. milioni 100.
Uongozi wa Azam umeshasema iwapo Yanga inamtaka kumrejesha mchezaji huyo, uende kuzungumza nao.
Alipoulizwa jana, Mwenyekiti wa Azam FC, Said Mohamed, alieleza klabu yake haipo tayari kumwachia mchezaji huyo, lakini amewataka viongozi wa Yanga kwenda kukutana nao kwa ajili ya majadiliano.
"Milango iko wazi, kama wanamtaka Ngasa waje tuzungumze, lakini sipendi kuzungumzia mambo katika vyombo vya habari, kwa nini wao hawaji kama kweli wana nia hiyo," alihoji kiongozi huyo wa Azam.