YANGA KUREJEA DAR KUIWINDA PRISON.
Jumapili ya Januari 26 2020 kwenye uwanja wa Uhuru, kikosi cha Yanga kitashuka dimbani kuikaribisha Tanzania Prisons katika mchezo wa raundi ya nne kombe la FA (ASFC).
Timu hizo zinakutana kwa mara ya pili msimu huu, Yanga ikishinda kwa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza wa ligi kuu uliozikutanisha timu hizo mkoani Iringa.
Wakati kikosi cha Tanzania Prisons kikiwa hakina mabadiliko, hali itakuwa tofauti kwa Yanga iliyosukwa upya katika usajili wa dirisha dogo.
Wachezaji wapya saba wameongezwa Yanga huku wengine sita wakionyeshwa mlango wa kutokea.
Maboresho hayo yameiongezea Yanga makali, sasa ikicheza kandanda la kushambulia muda mwingi tangu ujio wa kocha Luc Eymael.
Yanga inatokea mkoani Singida ambako jana ilipata ushindi wa mabao 3-1 huku kiungo wake mshambuliaji Bernard Morrison aliyetua wiki iliyopita akiwaongezea makali mabingwa hao wa kihistoria.
Baada ya kukosa taji lolote kwa misimu miwili, Yanga imedhamiria kuondoka na taji msimu huu hesabu kali zikipigwa kwa taji hili la FA na ligi kuu.
Ushindi katika mchezo huo utawahakikishia kutinga hatua ya 16 bora mchezo mmoja kuelekea hatua ya robo fainali.
@Yangafulldozz