NCHIMBI AFURAHIA KUCHEZA NA MOLINGA
Mshambuliaji wa Yanga Ditram Nchimbi, amemtaja David Molinga kuwa ndiye anayempa raha kila wanapocheza pamoja, ikiwa ni baada ya kutengeneza pacha hatari hivi karibuni
Tangu aliposajiliwa na Yanga katika dirisha dogo la usajili mwezi uliopita, Nchimbi ameonekana kuelewana vilivyo na straika Mkongo, Molinga, wakiisaidia timu yao hiyo kuendelea kukusanya pointi msimu huu.
Kombinesheni yao ilianza kuonekana katika mchezo wa Ligi Kuu kati ya Yanga na Mtibwa Sugar, Nchimbi akitoa asisti tamu kwa Molinga, pia, alikuja kufanya hivyo tena Wanajangwani walipomenyana na Ruvu Shooting.
Nchimbi maarufu kama Duma, amesema baada ya kucheza michezo michache sambamba na Molinga ameanza kuielewa mikimbio ya mshambuliaji mwenzake huyo na jinsi gani ya kumpenyezea pasi za kufunga mabao. "Nafurahi mno ninapocheza na Molinga. Sasa nafahamu ni aina gani ya pasi za kumpenyezea na katika mazingira yapi ili aweze kufunga mabao. "Uzuri ni kwamba Molinga ana uelewa mkubwa wa mchezo wa soka, hata kama hana kasi, lakini anajua aina ya pasi ninazomletea njiani kutokana na mimi pia nimeshafahamu nimchezeshe vipi"
Tangu ajiunge na Yanga, Nchimbi bado hajafanikiwa kuifungia bao, lakini uwezo wake wa kukaba na kukokota mpira unaonekana kuwa na faida ndani ya timu hiyo kupitia kwa wachezaji wenzake
Leo Jumamosi Yanga itashuka dimba la Taifa kuikabili Tanzania Prisons katika mchezo wa ligi kuu mzunguuko wa 22
Yanga ilishinda bao 1-0 katika mchezo wa kwanza baina ya timu hizo uliopigwa mkoani Iringa
Baadae ikashinda 2-0 kwenye mchezo wa kombe la FA hatua ya 32 bora
Bila shaka Molinga na Nchimbi watajumuishwa kwenye kikosi kitakachoshuka dimbani