EYMAEL KUMBADILISHIA MAJUKUMU YONDANI
Kocha Mkuu wa Yanga Luc Eymael ameeleza kuvutiwa na kiwango kilichoonyeshwa na mkongwe Kelvin Yondani wakati alipomtumia namba sita kwenye mchezo dhidi ya Gwambina Fc.
Eymael amesema ataendelea kumtumia Yondani kwenye nafasi hiyo kila atakapoona inafaa.
Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa Yondani kucheza namba sita kwani kwa miaka zaidi ya 15 Yondani amekuwa akitumika nafasi ya ulinzi wa kati.
Hata hivyo kasi yake imeanza kupungua kutokana na umri wake kuendelea kumtupa mkono "Nilivutiwa na jinsi Yondani alivyocheza namba sita kwa mara ya kwanza tangu nimejiunga na timu hii, nimempanga kucheza nafasi hiyo baada ya kumuona ana kontroo nzuri, pia ukabaji wake ni wa kipekee," amesema Eymael "Katika timu ninataka kuwa na wachezaji wa aina hiyo wenye uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya moja ndani ya uwanja, nitaendelea kumtumia kwenye nafasi hiyo kila nitakapoona inafaa".
Mwenyewe Yondani amesema anaweza kucheza nafasi zote uwanjani isipokuwa golikipa tu "Pengine mashabiki wamezoea kuniona nikicheza beki, lakini ukweli ni kwamba mimi naweza kucheza nafasi zote, labda kuwa golikipa tu ndio nitashindwa," ametamba Yondani.
Kwa sasa safu ya ulinzi ya Yanga inawategemea zaidi Lamine Moro na Said Juma Makapu ambaye msimu huu ameonyesha uwezo wa hali ya juu jambo lililomuhakikishia namba kwenye kikosi cha kwanza akiwapiku Andrew Vicent, Ally Mtoni, Ali Ali na hata Yondani.