Kiungo mshambuliaji wa Yanga Said Ntibazonkiza amesema ujio wake Yanga ni kwa ajili ya kazi moja tu, kuhakikisha anawasaidia mabingwa hao wa kihistoria kushinda mataji
Ntibazonkiza alisajiliwa na Yanga mapema wiki hii kwa mkataba wa mwaka mmoja na nusu akiwa mchezjai huru Yanga ikimnasa baada ya kumalizika mchezo wa Kimataifa wa kirafiki kati ya Tanzania dhidi ya Burundi uliomalizika kwa Burundi kupata ushindi wa bao 1-0 ambalo aliliweka kambani yeye
Ntibazonkiza amekiri ujio wake Yanga una mkono wa kocha mpya wa timu hiyo Cedric Kaze ambaye aliwahi kumfundisha kwenye timu ya Taifa mwaka 2011.
"Mimi nimekuja Yanga sio kwa bahati mbaya, wapo wanaofikiria nimesajiliwa baada ya mchezo dhidi ya Tanzania. Tulikuwa na mazungumzo na Yanga miezi miwili au mitatu nyuma lakini nilishindwa kujiunga nao kutokana na changamoto kadhaa zilizokuwepo wakati huo. Sasa nilipokuja tena hapa ikawa rahisi kumalizana nao kwani hata yale yaliyotukwamisha mwanzo hayapo," amesema
"Nimekuwa nikiwasiliana na kocha Kaze mara kwa mara hata kabla mpango wa kujiunga na Yanga haujaibuka. Kabla sijasaini mkataba, alinipigia simu na kunielekeza ananihitaji hivyo niwasikilize viongozi wa Yanga. Nimezungumza nae pia baada ya kusaini amenieleza mipango yake hapa"
Ntibazonkiza ataanza kuitumikia Yanga mwezi Disemba pale dirisha dogo la usajili litakapofunguliwa lakini atakuwa na muda wa kuzoeana na wenzake kwani ataanza kujifua na mabingwa hao wa kihistoria Novemba 15 siku ambayo mkataba wake utaanza rasmi.