Mlinda lango wa Yanga Farouk Shikhalo huenda akachelewa kujiunga na wenzake kutokana na Serikali ya Kenya kuwa bado imefunga mipaka kutokana na janga la corona.
Wachezaji wa Yanga walifanyiwa vipimo vya Afya juzi na jana kuanza mazoezi huku nyota huyo akikosekana sambamba na kocha mkuu Luc Eymael ambaye hata hivyo anaweza kuwasili wiki ijayo.
Uongozi wa Yanga umesema unafuatilia taratibu za kumrejesha nchini mlinda lango huyo.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga Fredrick Mwakalebela amesema pamoja na kuwa suala lake liko nje ya uwezo wao, wanapambana kuhakikisha anarejea nchini kwa wakati ili aungane na wenzake
"Suala la Shikalo lipo nje ya uwezo wetu, ila tunapambana kuhakikisha mchezaji huyo anarejea kwa wakati na kuwahi kabla ya ligi haijaanza rasmi," amesema Mwakalebela
Kwa sasa Yanga itamtegemea mlinda lango mmoja Metacha Mnata huku wakimsubiri Ramadhani Kabwili ambaye hivi karibuni alishonwa nyuzi nane baada ya kupata ajali ya pikipiki.