TANZANIA ambayo iliasisiwa na Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Aman Karume baada ya muungano mwaka l964, ilijengwa katika misingi ya undugu, usawa na haki.
Kwa mantiki hii, nchi yetu ilijizolea heshima dunia nzima, licha ya kuwa na umaskini wa kutisha, kuwa ilikuwa kisiwa cha amani.
Nikiwa nchi za nje mara nyingi nilipotaja natoka Tanzania, nilisikia maofisa wa Uhamiaji wakisema: Hawa ni watoto wa Mwalimu Nyerere. Basi tulikuwa hatuna shida ya kusumbuliwa kama wanavyosumbuliwa Wakongo na Wanigeria wakisafiri kwenda Ulaya.
Lakini Tanzania ya leo ni tofauti kabisa, sasa inajulikana kama kitovu cha maovu, kama vile rushwa ya uchaguzi, ujambazi, hata ndani ya vyombo vya dola, wizi wa mali ya umma, utapeli na kadhalika.
Mwalimu Nyerere kama nabii na kiongozi wa nchi yetu alipewa uwezo wa kuona mambo mengi, ambayo viongozi wengine hawakujaliwa kuyaona.
Ndiyo maana aliweza kukabiliana na hatari zilizokuwa zinakuja mbele yake, hivyo kuchukua hatua stahiki, tofauti na Serikali ya Awamu hii ya Nne ya Jakaya Kikwete. Mwalimu Nyerere alikuwa na uwezo wa kukemea maovu juu ya mtu yeyote bila kujali alikuwa rafiki au mtu wa Musoma au Mzanaki mwenzake.
Azimio la Arusha lilikuwa na msingi mkubwa katika uongozi wake, ambao ulikuwa na maadili ya hali ya juu, ingawaje watovu wachache wa nidhamu walikuwapo, lakini cha moto walikipata na ndilo lilikuwa fundisho kwa wengine.
Leo kuna uongozi wa kirafiki au kishikaji, yaani wa kupendeleana na kubebana bebana. Kwa mtindo huu kweli tutafika?
Tumefika hapa tulipofikia, tumethubutu na tunaendelea kuthubutu kuliangamiza taifa kwa porojo na propaganda nyingi ambazo kuna baadhi ya Watanzania wanazishabikia bila kujua madhara yake kwa taifa.
Rais wa Awamu ya Nne ana mengi ya kujifunza kutoka kwa Mwalimu Nyerere, lakini je, kuna dalili ya kuchukua yale mazuri? Hotuba za wosia wa Baba wa Taifa, zinatufundisha nini?
Sana sana tumebaki kumkejeli tu, na hii ni kufuru, kwani wahenga husema asiyesikia la mkuu huvunjika guu. Je, serikali ya CCM haijavunjika mguu?
Kama sivyo, kwa nini sasa ina tapatapa kama siku ya nyani kufa, ambapo miti yote inateleza?
Mauaji ya kidini ambapo mchungaji wa Kipentekoste amepoteza maisha kutokana na suala la kuchinja huko Geita ni aibu kubwa kwa serikali ya CCM.
Serikali ya CCM haiwezi kukwepa lawama hii, pamoja na kwamba rais anajaribu kukemea na kutoa ahadi za kuchunguza, hatuwezi kumaliza matatizo makubwa ya kuhatarisha amani ya nchi kwa kuahidi kila siku unachunguza na kuwa utachukua sheria.
Hii ni hadaa kwa wananchi. Hii lugha imekuwa kiinimacho tu kwa masuala mengi ya msingi katika taifa letu.
Suala la kuchinga si la serikali ni la kiimani. Kama nchi yetu na serikali havina dini, kwa nini serikali isitoe mwongoza kwamba kila watu wachinje kadiri ya imani yao? Anayependa kwenda kununua katika bucha ya Waislamu sawa, za Wakristu sawa, za Wapagani sawa.
Nauliza, je, kule kijijini kwangu Langiro- Mbinga, ambako hakuna Mwislamu hata mmoja, itakuwaje?
Natoa rai kwamba serikali iache kuingilia masuala haya nyeti ya imani ya watu katika jambo linalohusu imani yao.
Naungana na maaskofu wa Mwanza kuhusu suala hilo, kwamba hakuna aliye na mamlaka ya kuchinja, bali ni ya wote, na serikali kupitia mwakilishi wake katika suala hilo, Waziri Steven Wassira na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza walipata wapi mwongozo wa kusema haki ya kuchinja ni ya Waislamu? Haya mamlaka walipewa na nani?
Serikali inaonekana kuwa kinara wa udini nchini, ukiangalia hata katika kampeni za chaguzi mbalimbali kama kule Igunga na Arumeru CCM walijaribu kutumia udini kwa kiasi kikubwa.
Rais asishangae yanayotokea kwa sababu serikali yake ndiyo iliyoasisi suala la udini kwa masilahi ya chama chake. Unajua Waswahili husema ukiudharau mwiba hata kama ni mdogo utakuja kujutia.
Au mfano wangu mwingine ni wa mtu kufuga nyoka mdogo, baadaye akawa mkubwa na kuanza kumfukuza mwenye nyumba.
Kule Zambia miaka ya l980 kuna padri mmoja alikuwa na nyumba ya makumbusho, alikuwa akifuga nyoka, siku moja nyoka huyo alimngata ikabidi akatwe kidole chake.
Hiki ndicho kinachotokea kwa CCM nyakati hizi. Ile sumu ya udini iliyopandikizwa na CCM ndani ya chama chake, ndani ya vyama vya upinzani, hasa CHADEMA na ndani ya madhehebu ya dini, hasa Katoliki, sasa imeanza kuidhuru CCM yenyewe na wamebaki wakishangaa.
Mimi nasema bado madhara makubwa yanakuja, na Tanzania nzima, Afrika nzima na dunia nzima watajua wazi kwamba CCM ni muasisi wa udini nchini Tanzania.
Mungu ataonesha wazi kabisa ni nani aliasisi dhana ya udini katika nchi yetu.
Ukiangalia matukio ya hivi karibuni kuanzia mwaka jana, utaona wazi kwamba nchi yetu inaelekea shimoni au imekwisha kutumbukia shimoni.
Migogoro ya kila siku ya wafugaji na wakulima, migororo ya wafanyakazi, madaktari, walimu, migogoro ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, mahujaji ya mashambulizi ya viongozi wa dini, uporaji wa wanyanyama, usafirishwaji wa meno ya tembo, migogoro kuhusu rasilimali kama gesi ya Mtwara, makaa ya mawe Mbinga, madini Kahama na kadhalika ni dhahiri kwamba nchi hii imefikia hatua mbaya pamoja na kujigamba kwamba tumesherehekea miaka 51 ya uhuru.
Maadhimisho ya miaka 36 ya kuzaliwa kwa CCM yaliyogeuka kuwa mapambano ya kivita na CHADEMA ni alama nyingine mbaya kwa chama hicho kwamba kimefika pabaya.
Huhitaji shahada kujua ukweli huo. Kibaya zaidi, utovu wa nidhamu uliotokea wiki mbili zilizopita huko bungeni juu ya ukandamizaji wa demokrasia kwa wabunge wa upinzani ni ishara wazi kwamba, kweli taifa limefika pabaya.
Sasa tunataka CCM ifanye nini kuwaonesha Watanzania na dunia nzima kwamba imeshindwa kuongoza nchi hii? Watanzania mnangoja muujiza gani tena?
Someni alama za nyakati, Mungu ameamua kuwaonesha kila kitu wazi kwamba CCM imegawanyika na haiwezi kuwa alama ya umoja na uongozi makini katika nchi yetu.
Kuiongelea Tanzania ya leo bila kumwongelea Mwalimu Nyerere ni kujidanganya.
Wengine wanathubutu kusema ati awamu hii imefanya maendeleo makubwa kuliko ya Nyerere, ni kwa vigezo gani?
Mwalimu alisema hatutaki maendeleo ya vitu; majumba, barabara na magari, bali tunataka maendeleo ya watu. Je, watu wetu wana maendeleo gani? Umaskini, ujinga na maradhi bado vinawasumbua kwa kiasi kikubwa.
Tafsiri ya maendeleo kwa Mwalimu Nyerere ni maendeleo ya watu na si vitu. Watanzania tufumbue macho yetu ili tuone tuko wapi, tunapelekwa wapi na utawala huu wa Awamu ya Nne?
Kuhusu ukabila, ukanda na udini, Mwalimu Nyerere ambaye sasa ni mtumishi wa Mungu, yaani yumo katika mchakato wa kufanywa mtakatifu, alionya tangu mwanzo kwa kusema kwamba: Ukabila bado upo.
Kwa hiyo, ukabila lazima uendelee kupigwa vita. Hapana kukaa na kusema; Tanzania hatuna ukabila. Hapana. Kwa hiyo, lazima tuendelee kuupiga vita. Na watu wana udini dini. Kuna watu wanatamani nchi hii iwe ya Kikristu, wajinga.
Kuna watu wanatamani nchi iwe ya Kiislamu, wajinga. Natumia neno zuri wajinga, sisemi wapumbavu. Wajinga! Huyu ndiye Rais wa Awamu ya Kwanza na alikuwa anamaanisha kile alichokisema, lakini awamu yetu hii ni awamu ya propaganda na porojo.
Zaidi kuhusu suala la udini na msimamo wa rais wa nchi, mwalimu Nyerere alitoa msimamo huu: Tunataka rais wetu, akiwa Mkristu, ajue hatumchagui kwa sababu ya Ukiristu wake. Akiwa Mwislamu, ajue hatukumchagua kwa sababu ya Uislamu wake. Hatumchagui awe rais wa Wakristu wala awe wa Waislamu, na tunataka hilo alijue na alikubali kwa dhati na alisimamie na ndiye kiongozi wetu. Alisimamie kwa dhati bila woga, ndiye kiongozi wetu. Katika nchi changa namna hii, ambayo watu haraka sana hukimbilia ukabila, haraka sana hukimbilia udini, tunataka kiongozi awe imara kabisa katika mambo kama haya.
Kipindi hiki cha Kwaresma ni muda mwafaka kwetu sote kuomba na kufunga katika kipindi hiki cha neema ili Mungu atuepushe na machafuko yatokanayo na viongozi wabovu wa kisiasa na jamii.
Kila mmoja wetu, hasa viongozi Wakristu wajiulize wanafanya nini kutetea haki ya wanyonge, wanajenga Tanzania yenye haki na usawa katika masuala yote?
Kwa nini, kwa mfano wabunge hawapingi suala la kuiingiza nchi katika Jumuiya ya nchi za Kiislamu, au kuiingiza Mahakama ya Kadhi katika Katiba mpya, wakati tukijua masuala hayo ni hatari sana kwa mshikamano na amani ya nchi yetu?
Watanzania tunahitaji kuomba sana ili Mungu aiepushe nchi yetu na mipango ambayo ninaamini haifanikiwi kamwe, kwa sababu Mungu wetu ni Mungu wa Upendo na ni baba wa wote, bila kujali dini, itikadi wala kabila.
Sote tusimame imara kama unavyosema ujumbe wa maaskofu Katoliki katika kipindi hiki cha Kwaresima pamoja na Mungu wetu, tuupige vita ukabila, ukanda, na hasa udini katika nchi yetu.
Hiki kipindi kituletee neema na kweli na hatimaye tukafufuke na Kristu mtawala, aliyeshinda maovu yote, ukiwamo ukabila na udini. Mungu ibariki Tanzania na watu wake!
| |
|