Habari wana JF,
Wakati mwingine tunapojadili au kutafsiri maandiko ya watu ni vyema kuweka chanzo cha makala husika na au kuweka wasifu wa mhusika.
Mimi si mtaalamu wa sayansi ya unywaji maji ila ni mtaalamu wa afya/daktari LAKINI naona kuna maelezo yanayotolewa kwa jumlajumla bila tahadhali yoyote. Hii inaweza kuwabadili watu kutoka kwenye jambo jema kiafya na kuwapeleka kwenye hali tata kwa kuogopeshwa na maelezo waliyoyasoma.
Suala la unywaji maji hutegemea vichocheo vywa mwili ambavyo humpa taarifa binadamu/mnyama juu ya uhitaji wa maji/kiu. Upataji wa kiu hutegemea zaidi na size ya mwili wa mtu, hali ya hewa, aina ya kazi au mazoezi na utimamu wa vichocheo husika vya mwili juu ya utoaji taarifa ya kiu.
Ni kweli kwamba unywaji wa maji mengi unaweza kuwa na madhara kwa mhusika kutokana na moja kudilute kiasi cha madini yaliyoko mwilini lakini pia kutokana na mfumo wa mzunguko wa damu kuwa hauna nafasi ya ziada ya kubeba kiasi cha maji yaliyonywewa basi unaweza kusababisha kujaa kwa mfumo/overload.
Madhara tajwa hapo juu huweza kujitokeza zaidi pale binadamu au mnyama anapotundikiwa maji/drip. Lakini kutokana na mfumo wa mrejesho hasi/feefback kwa upande wa anaekunywa maji si rahisi kusababisha hilo labda tu kama mfumo wake wa kuondoa kiu na kuridhika/satisfaction utakuwa una shida.
Kitaalamu kwa siku, inakisiwa kisayansi kuwa kwa ujumla (jasho, kupumua, choo kikubwa, kuongea pamoja na mkojo) vinasababisha kiwango cha maji lita moja na nusu kutoka mwilini. Njia ipi hutoa zaidi, hutegemeana na hali ya mazingira husika
Hivyo ni vizuri kurudisha kiasi hiki cha maji mwilini japo si kwa wakati mmoja.
Ni kweli kwamba kadri unavyokunywa maji ndivyo mwili utakubali kutoa maji kama jasho au mkojo. Na kadri usivyokunywa maji ya kutosha ndivyo mwili hautayatoa hayo maji, hii haimaanishi kuwa uko salama zaidi au na afya njema bali mwili unang'ang'ania maji hayo kutokana na kutokuwa na maji toshelevu. Hivyo, kama ukipata choo kitakuwa kigumu, mkojo utakuwa ni wanjano/concentrated, jasho kidogo na lenye chumvi nyingi. Hii ni hatari kwa afya kwani mwili utabakiza uchafu mwingi mwilini kwa kukosa maji ya kuandamana na huo uchafu.
Nini kifanyike?
Tii kiu yako, kunywa maji kwani mahesabu mengi hayazingatii hali ya mazingiira uliyopo ambapo kila mmoja huitaji ku-adjust kulingana na hali yake na mazingira. Isipokuwa kwa wale wenye shida maalumu kama matatizo ya digo nk.
Pale unapoona wewe unakunywa maji mengi kupindukia kuzidi watu wanaokuzunguka, fika kwa wataalamu wa afya wakufanyie uchunguzi kwani matatizo ya vichocheo tajwa hapo juu yapo.
Kunywa maji kwa afya.