Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 5,352
- 15,876
TAARIFA KWA UMMA
HAKUNA MARIDHIANO BILA UKWELI, HAKI NA UWAJIBIKAJI
Kauli hiyo imetolewa leo, Novemba 1, 2026, wakati Chama kikiwa kimeanza ziara katika Kanda ya Ziwa, kwa lengo la kuzungumza na wananchi kuhusu masuala mbalimbali yanayoendelea nchini.
Mkutano wa kwanza wa ziara hiyo umefanyika katika Kata ya Mwandoya, Jimbo la Kisesa, na kuongozwa na Ndg. Isihaka Mchinjita, Waziri Mkuu Kivuli, akifuatana na Ndg. Luhaga Joelson Mpina, Naibu Waziri Mkuu Kivuli na aliyekuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia ACT Wazalendo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Katika mkutano huo, viongozi hao wa Chama wameeleza kutoridhishwa kwa ACT Wazalendo na hali ya kisiasa nchini pamoja na hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kufuatia matukio ya mauaji ya raia ya Oktoba 29, 2025, uporaji wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, pamoja na kuendelea kubinywa kwa demokrasia na kudhoofishwa kwa utawala bora.
Chama kimeeleza kuwa kuundwa kwa Tume ya Jaji Chande na Tume ya Jaji Lila hakujajibu kikamilifu madai ya wananchi kuhusu ukweli, haki na uwajibikaji. Badala yake, ACT Wazalendo inaona hatua hizo kama jitihada zinazoweza kutumiwa kufunika ukweli na kuhamishia lawama kwa watu wengine, badala ya kuwawajibisha wale wenye dhamana ya kisiasa na kiutendaji kwa hali iliyofikisha nchi katika mgogoro huu.
ACT Wazalendo inataka haki na uwajibikaji kuhusu mauaji na utekaji wa raia. Chama kimelaani vikali mauaji yaliyofanywa na vyombo vya dola wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025. Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa kuhusu matukio hayo, watu 518 waliuawa, wakiwemo wanawake, watoto na watu wenye ulemavu. Aidha, watu 758 waliripotiwa kupotea katika kipindi cha mwaka 2023 hadi 2025, ambapo hadi sasa watu 205 hawajulikani walipo.
Kuhusu kinachoitwa maridhiano ya kitaifa, viongozi hao wamehoji "Tunaridhiana na nani, kwa misingi ipi na kwa maslahi ya nani?" ACT Wazalendo imesisitiza kuwa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan haiwezi kudai kujenga maridhiano ya kitaifa huku ikikwepa kuwajibika kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na uharibifu wa misingi ya demokrasia.
Maridhiano hayawezi kuwa mbinu ya kuwasahaulisha wananchi maumivu yao, kufuta kumbukumbu ya damu iliyomwagika au kuwapa kinga wale waliohusika na vitendo vya uhalifu dhidi ya raia.
Chama kimesisitiza kuwa Tanzania haiwezi kujenga mustakabali wa kidemokrasia kwa kufumbia macho mauaji yaliyotokea, watu waliotekwa na familia zinazoendelea kusubiri kujua hatima ya ndugu zao. Serikali inapaswa kukubali ukweli, kuwajibika na kuruhusu uchunguzi huru. Hatua zozote za kisiasa zinazochukuliwa bila kushughulikia kiini cha mgogoro huu ni jitihada za kujenga utulivu wa juu juu badala ya kuleta maridhiano na mabadiliko ya kweli.
Ili kuhakikisha ukweli, haki na uwajibikaji vinapatikana, ACT Wazalendo inataka kuundwa kwa Tume Huru ya Kimataifa ya kuchunguza matukio ya mauaji, utekaji na upotevu wa raia. Aidha, Chama kinataka kuondolewa kazini kwa Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa (DGIS), Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), pamoja na Wakuu wa Mikoa na Wilaya katika maeneo yalipotokea mauaji, ili kujenga upya imani ya wananchi kwa taasisi za dola.
Chama pia kinataka wote watakaobainika kuhusika na ukiukwaji huo kupitia uchunguzi wa Tume huru itakayoundwa wachukuliwe hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza katika mkutano huo, Ndg. Luhaga Joelson Mpina amesema: "Ujumbe wetu uko wazi: hakuna maridhiano bila ukweli, haki na uwajibikaji kwa waathirika wa ukandamizaji unaofanywa na mtawala."
Kuhusu mageuzi ya kisiasa na kikatiba, viongozi hao wamesisitiza kuwa Tanzania inahitaji Katiba Mpya sasa, si viraka wala maboresho ya Katiba iliyopo. Chama kinataka kupatikana kwa Katiba Mpya ya Wananchi kabla ya mwaka 2029, itakayoweka misingi imara ya demokrasia, utawala bora, uwajibikaji na ulinzi wa haki za wananchi.
Imetolewa na:
Abdallah Khamis
Afisa Habari
ACT Wazalendo
01 Novemba 2026