ADHABU YA KIFO KWA KUCHINJWA MBELE YA KADAMNASI
SEHEMU YA TATU
Inaendelea kutoka ilipoishia sehemu ya pili….
Yapata kama saa 7 na nusu hivi, polisi walipogiwa simu na kufika nyumbani kwa familia ya Otaibi.
Walipofika mama mwenye nyumba akawaeleza kwamba Rizana amemuua mtoto wake kwa kumnyonga shingo.
Mama mwenye nyumba alieleza maelezo haya mara baada ya watoto wake kumwambia kuwa walisikia Rizana analia chumba cha pili na walipoenda wakamkuta anamgeuza geuza mgeuza mtoto mikononi mwake. Kwa maelezo haya ya watoto, mama huyu akahitimisha kuwa Rizana amemuua mtoto wake kwa kumnyonga shingo.
Pamoja na maelezo hayo, mama mwenye nyumba aliwaeleza polisi kuwa asubuhi ya siku hiyo alikuwa amemfokea Rizana kutokana na kutofanya usafi vizuri, kwa hiyo aliamini kuwa Rizana alimuua mtoto wake ili kulipa kisasi kwa hasira za kufokewa.
Moja kwa moja Rizana akachukuliwa mpaka kituo cha Polisi. Alipofikishwa na kituoni na kuanza kuhojiwa ndipo ambapo alijua ni namna gani kutokujua kuunga hata sentesi moja ya kiarabu kuna mgharimu.
Ilikuwa ni ngumu hata kumafanyia mhojiano… Rizana alikuwa hajui kuongea kiarabu, lugha pekee aliyokuwa anaifahamu ni Tami na hakukuwa na polisi yeyote yule ambaye alikuwa anajua kuongea Tamil.
Kwa hiyo alipokuwa anaulizwa ajieleze ni nini kimetokea alibakia kuduwaa tu asijue aseme nini na ukijumlisha kipigo alichopewa na mwenye nyumba pamoja na mtoto kumfia mikononi mwake, Rizana alikuwa katika mshituko kana kwamba amechanganyikiwa.
Baadae polisi wakapewa taarifa ya daktari kwamba mtoto amefariki kwa sababu ya "suffocation" (kukosa hewa) na si kunyongwa shingo kama mama yake alivyoeleza. Lakini hii haikutosha kuwafanya polisi wamuone Rizana labda hana hatia.
Kuna suala moja kubwa lenye ukakasi mwingi kuhusu adhabu ya kifo nchini Saudi Arabia.
Watu wote ambao huwa wanahukumiwa adhabu hii na hatimaye kuchinjwa hadharani huwa wanakili kufanya kitendo hicho na huwa wanakiri kwa maandishi na kuweka sahihi zao.
Hili ni suala la kushangazo mno, ni vipi kila anayechinjwa lazima akiri kwa maandishi juu ya kitendo anachoshutumiwa nacho.
Kupitia mkasa huu wa Rizana, kuna masuala nyeti mengi yaligundulika kuhusu utesaji ambao polisi huwa wanawafanyia washtakiwa ambao kesi zao zina adhabu ya kifo ili waweze kukiri na kusaini nyaraka za kuthibitisha kujutia kwao walichokifanya.
Hiki ndicho ambacho pia kilimkuta Rizana alihojiwa kwa wiki kadhaa pamoja na kuteswa na polisi ili akiri kumuua mtoto wa muajiri wake.
Shida kubwa ilikuwa na lugha kutofautiana. Kila ambavyo Rizana alijitahidi kueleza upande wake wa nini kilitokea hakuna mtu ambaye alimuelewa hapo polisi alipokuwa anashikiliwa kwa kuwa hakukuwa na mtu ambaye alikuwa anazungumza lugha ya Tamil.
Baada ya wiki kadhaa alipatikana mtu ambaye alidai kuwa anaifahamu lugha ya Tamil. Kijana huyu alikuwa ni raia kutoka Malaysia ambaye alikiwa hapo Saudi Arabia akifanya kazi ya kuchunga kondoo.
Kupitia kijana huyu mahojiano yakaendelea kwa kasi ya ajabu.
Lakini alichokuja kuongea Rizana huko mbeleni ni kwamba kijana huyo hakuwa anajua Tamil kwa ufasaha na hakuamini kuwa alikuwa anatafsiri kwa usahihi kile alichokuwa anakiongea.
Baada ya mateso ya miezi kadhaa hatimaye Rizana alifikishwa mahakamani.
Kama ambavyo nilieleza katika sehemu ya kwanza ya mfululizo wa makala hii, kwamba nchi ya Saudi Arabia wanatumia mfumo wa Sharia ya Kiislamu (kwa tafsiri yao) katika kuendesha mashataka.
Kwa hiyo mambo mengi ya kisheria yaliyomo katika mfumo wa sheria wa kawaida huwa hayatekelezwi nchini Saudi Arabia.
Kwa mfano Rizana akishatakiwa na kesi kuendeshwa pasipo kupewa mwanasheria wa kumtetea.
Maandamano kudai haki itendeke na kuachiwa kwa Rizana
Familia ya Rizana[
Kesi ya Rizana ilizua mjadala mzito wa kimataifa.
Wanaharakati wengi walihoji ni kwa namna gani Saudi Arabia walifanya uzembe mpaka binti wa miaka 17 akaingia ndani ya nchi yao na kupewa kibali cha kufanya kazi.
Lakini pia watu walihoji namna ambavyo kesi ilikuwa inaendeshwa pasipo Rizana kupewa msaada wa kisheria.
Kesi ya Rizana ilivuta hisia za wengi sana huku watu wengi wakiamini kuwa Rizana hakuwa na hatia na kwa kuwa Rizana hakuwa raia wa Saudi Arabia na wala hatoki kwenye familia yenye ushawishi ilikuwa ni dhahili kwamba kesi hiyo lazima itaisha kwa Rizana kuhukumiwa kifo kwa kuchinjwa mbele ya kadamanasi.
Maandamano yalifanyika katika nchi nyingi za Asia na Ulaya kuishinikiza serikali ya Saudi Arabia kutenda haki katika kesi ya Rizana.
Hatimaye mwaka 2006 upande wa mashataka wakawasilisha mahakamani "confession" ya Rizana ambayo iliandikwa na polisi kwa kiarabu na Rizana kutia sahihi ya dole gumba.
Nyaraka hiyi ilisomwa mahakamani na kuonyesha kwamba Rizana alikuwa amekiri kumuua mtoto Kayed wa boss wake.
Lakini January 30, 2007 Rizana alisainu Affidavit kujieleza upande wake wa nini kilitokea.
Alisema hivi, nanukuu;
"..madam alirudi nyumbani saa 7:30 mchana na baada ya kumuona mtoto alianza kunishambulia na kunipiga mpaka damu zikaanza kunitika mdomoni na puani.
Baada ya hapo nilichukuliwa mpaka kituo cha polisi ambako nako nilidhalilishwa na kuendelea kupigwa kwa mikanda ya polisi na kulazimishwa kukiri kuwa nimemuua mtoto.
Walinipiga na kunitisha kuwa nisipokiri wataendelea kunipiga mpaka nife. Ili kujiepusha na maumivu haya na kutokana na kuchanganyikiwa kwa kipigo, nilitia sahihi yangu katika karatasi ya maelezo yalikuwa yakionyesha kuwa nimuua mtoto wa muajiri wangu. Lakini nasema ukweli na naapa kwa Allah, sikumuua yule mtoto."
Mwisho wa nukuu.
Licha ya hoja hizi za Rizana, lakini siku ya tarehe 16 June 2007, mahakama ikamuhukumu Rizana Nafeek adhabu ya kifo kwa kukatwa kichwani mbele ya umma.
Hukumu hii iliibua hasira zaidi za wanaharakati za haki za binadamu duniani kote.
Rais wa Sri Lank yeye binafsi alituma maombi maalumu mara mbili kwa mfae wa Saudi Arabia ili aweze kumpa msamaha Rizana lakini mara mbili zote hizo ombi lake lili kataliwa na King Abdullah
Juhudi za kumuokoa Rizana hazikuishia hapo tu, hata Prince Charles aliingilia na kutoa ombi lake kwa King Abdullah ampe msamaha Rizana lakini bado Mfalme alikataa.
Kuna wengine walienda mbali zaidi hata kuanzisha kampeni ya kumtaka malkia katika maadhimisho yake ya "Diamond Jubilee" apaze sauti kuungana na wanaharakati wote kutaka Rizana asikatwe kichwa hadharani.
Serikali ya Saudi Arabia ilikuwa inapewa presha kutoka kila kona ya dunia. Hii iliwafanya wahahirishe utekelezaji wa adhabu ya Rizana mara kwa mara.
Lakini kama nilivyosema jana kuwa,
"Siku ya hatma, kiza hakichelewi", hatimaye ukafika mwaka 2013. Na ulipofika mwezi January siku ya tarehe 9, Rizana alipelekwa katika uwanja wa "machinjio" kukutanishwa na binadamu ambaye kukata vuchwa vya binadamu wengine ndio amefanya kuwa wito wake wa Maisha, Rizana akakabidhiwa mikononi mwa Muhammad al-Beshi, mchinjaji rasmi wa binadamu wa serikali ya Saudi Arabia.
Zoezi la kumchinja Rizana ilikuwa ni moja ya changamoto kubwa ambayo Al-Beshi kiwahi kukutana nayo katika wito wake huu "mtakatifu". Kwa sababu kama ambavyo mwenyewe al-beshi huwa anaeleza kuwa watu wanaotakiwa kuchinjwa wakifikishwa mbele yake wanakuwa wanyonge na hawana nguvu kabisa na wamekata tamaa kabisa na hivyo wanafanya kila kitu ambacho anawaeleza. Akiwaambia inamisha kichwa, wanainamisha na anawakata kichwa kwa kasi ya ajabu kama umeme.
Lakini haikuwa hivyo kwa Rizana… Rizana alikuwa anapaparika na kupiga mayowe ya kila namna akilia kwa uchungu akirudia maneno yale yale tena na tena…
"..Sijamuua yule mtoto, sijaua mtoto, sijamuua yule mtoto, hii hadhabu ni Haramuuu, haramuuuuu..!"
Kumsikia Rizana alivyokuwa analia na jinsi walivyokuwa wanahangaika kumshika ili wamchinje ilikuwa inaweza kukufanya utokwe na mchozi shavuni.
Baada ya purukushani nyingi, hatimaye ilipotimia saa 5 na dakika 40 siku hiyo ya tarehe 9, Januaru 2013… Al-Beshi alipitisha sime shingoni kwa Rizana na kutenganisha kichwa na kiwili wili cha Rizana Nafeek.
Na huu ndio ulikuwa mwisho wa maisha na Rizana juu ya uso wa dunia.
Tazama video hapo chini…
Tahadhari: Maudhui ya ukatili mkubwa
Kuchinjwa kwa Rizana kuligusa ulimwengu kwa namna ya tofauti sana.
Serikali ya Sri Lanka walilaani vikali kitendo hicho cha raia wao kuchinjwa hadharani huku wakiamiani kuwa hakuwa na hatia.
Kabla ya kuanza kwa shughuli za Bunge, wabunge wote wasimama kwa ukimya wa dakika moja kumkumbuka Rizana.
Pia katibukuu wa Umoja wa Mataifa wa kipindi hicho alilaani vikali kitendo kilichofanyika.
Taasisi ya Asian Human Rights Commission nao walitoa tamko kali kulaani kitendo hicho.
Serikali ya uingereza nao walilaani kitendo kilichofanywa na serikali ya Saudi Arabia.
Si hao tu bali pia Ufaransa na Umoja wa Ulaya walitoa matamko kulaani kitendo cha kuchinjwa na Rizana.
Serikali ya Saudi Arabia katika juhudi ya kujisafisha kwenye Jamii ya kimataifa, wakapeleka "rambi rambi" ya dola 16,000 kwa familia ya Rizana iliyoko kijiji Moothoor, nchini Sri Lanka.
Licha ya umasikini wao wa kutupwa, lakini Familia ya Rizana ilikataa kupokea rambi rambi hiyo.
Hiki ni kisa #1…. Usikose kisa #2 nitakachoweka siku chache zijazo
The Bold