SoC02 Amka Afrika, amka mama!

SoC02 Amka Afrika, amka mama!

Stories of Change - 2022 Competition

Jake lema

Member
Joined
Oct 24, 2018
Posts
5
Reaction score
3
Kwanini unalala bado? Kwanini unalikumbatia shuka bado? Kumekwisha kucha, jua limekwisha chomoza. Amka sasa eeh mama Afrika maana majukumu yako ni mengi. Watoto wako wanalia njaa zinawauma, wanalia majirani zao wanawaonea, kwanini usiamke uwafariji wana wako?

1663082054878.png


Mchoro: Mama Afrika akiwa kitandani amelala.

Nyumba yako unayoimiliki pamoja na wana wako kwanini mnnaishi kama wapangaji? Kwanini mnaruhusu majirani kuingia na kutawala sebule hadi vyumba vyenu? Umewazaa watoto 54 kwa mapenzi mema, kwanini usiwapatie umiliki wao? Wanalia, Je! hauyaoni machozi yao?
1663082175657.png

Picha:Mama Afrika akibaguliwa nyumbani kwake.

Eeh mama unao marafiki wengi lakini hakuna hata mmoja anayekuwazia mema, wote wanakuchekea usoni lakini moyoni wanakutemea mate. Ni lini utajifunza kidogo unachokipata kugawana na watoto wako. Je! Miaka mingi uliyonayo haijatosha kuelewa ubaya wa hao wajiitao marafiki wa kufa na kufaana? Je! Chumvi ulioila haitoshelezi kuwabaini wema ni wapi na wabaya ni wapi?

Wingi wa mali zako hakuna awezaye kuhesabu, kwanini sasa njaa haikosi nyumbani mwako? Kwanini shida hazikomi kwako? Eeh mama Afrika wanasema eti wewe ni giza tupu-Je! hii si kwasababu ya usingizi wako? Amka sasa utambe uzuri wako na ujidhihirishe ya kuwa wewe ndiye mama lao; kama ni vijiko na sahani vyote vimejaa nyumbani mwako, mapazia na mashuka mazuri yote asili yake ni kwako. Kwanini sasa majirani ndio wanakuuzia wewe badala ya wewe kuwauzia wao?
1663082330691.png


Picha: Mali za mama Afrika haziwezi kuhesabika

Tumwambie nini huyu mama yetu, tumueleze nini atuelewe na kwa namna gani ili aamke? Eeh mama watoto wako wote wana ulemavu, wote lishe zao ni mbovu, ukuaji wao haukuwa mzuri tokea utotoni mwao. Itanichukua majuma na majuma kuwaelezea watoto wako, lakini nimewachagua watano wa makabila tofauti (mashariki, magharibi, kaskazini, kusini na kati) wawawakilishe wana wako wote, ili walau upatwe na wivu wa kuamka uwafute machozi wana wako.
1663082387927.png

Picha: Watoto 54 wa mama Afrika

Tanzania
Ni mtoto muungwana kwelikweli, mtulivu na anayependa kutunza sana amani kuliiko vyote avitunzavyo. Ni heri sana kuwa na mtoto kama huyu maana ameusitiri uso wako ujulikane na majirani zako ya kwamba wewe ni amani na upendo. Lakini ninalo moja la kukueleza juu yake, anapenda maendeleo lakini kinachomtatiza ni ametanguliza sana siasa kuliko hata vipaumbele vyake. Amejaa na mipango mkakati mingi lakini uhalisia wake hakuna. Mnyonyeshe maziwa ya siasa safi na uwajibikaji pengine utainusuru hatma yake.
1663082477697.png



Nigeria
Ni mwana mkorofi kuliko wanao wote wa kabila la magharibi. Amejaliwa na sifa na ubaguzi sana hii imepelekea vita na shida zisitoke mipakani mwake. Mpatie ziwa ulilompatia mwanao Tanzania pengine atajawaa na lishe ya uungwana, amani na utulivu.
1663082538098.png


Morocco
Amekuwa rafiki na majirani zake zaidi kuliko hata ndugu zake wa tumbo moja. Kumbuka mama ilifika wakati alitaka kukukana haujamzaa kisa rangi yake haijafanana sana na ndugu zake bali imefanana zaidi na majirani zake na eti kwamba chumba chake kimepakana nao hao majirani zake. Hivyo mama mkumbushe tu ya kwamba damu ni nzito kuliko maji.
1663082583230.png


South Afrika
Chumba chake kimekarabatiwa kwa mawe na vito vizuri sana hadi kimewashawishi baadhi ya wanao kuvutiwa na kukitembelea chumba chake. Mifuko yake imetuna, lakini sio kwa utashi wake bali hao majirani zake walimuwahi na kufanya urafiki nae. Basi mfundishe ukubwa wa mifuko yake kusiyapendezeshe madirisha tu bali hadi kitanda chake.
1663082622832.png

DR Congo
Napatwa na huzuni kukueleza juu yake mama, Kwani mali ulizommegea ilikuwa ni kwaajili yake au kwaajili ya wenzake? Nasikitika kuona amekonda licha ya milki yake kubwa. Hakika mti wenye matunda ndio unaopigwa mawe. Tazama hapa na ujifunze mama hao wanaojiita marafiki zako ndio wabaya wako. Piga hodi chumbani mwake akifungua, mueleze amani na upendo viwe tunu yake.
1663082658223.png


Ushauri wangu kwa mama Afrika
Naomba uwaite watoto wako wote uwajumuishe wawe kitu kimoja kwa maana tofauti zao ni nyingi sana. Wakumbushe umoja ni nguvu utengano ni udhaifu. Waliokuposa pale mwanzo walikuwa na nia madhubuti ya kuwaunganisha wana wako, lakini sioni hilo kwa waliopo sasa maana kila mmoja ameshika lake kwa manufaa yake na sio kwa manufaa ya watoto wako.

Usiwategemee jirani zako kuja kuujenga mji wako, kwa maana wao si wajenzi wako bali wabomozi wako. Usivutiwe na vyombo vyao wala wingi wa vyakula vyao na usikurupuke kuingia makubaliano nao maana wanacheza na udhaifu wako ili wanyonye uzuri wa matiti yako. Wategemee wanao nawe utajistarehesha uzeeni mwako

Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo, ukimlea katika upumbavu basi atakua mpumbavu, ukimlea katika ushupavu basi atakua mkakamavu. Eeh mama Afrika ulidharau kuwakuza wana wako katika ujasiri ndio matunda unayoyapata leo hii-wamekuwa wazito kujitafutia na waoga kujaribu, badala yake wanasubiri kuletewa na kupikiwa na majirani zao. Hivyo basi waonye ingali bado ni mapema watumie akili zao za kuzaliwa ili wapate kula mema ya nyumba yao.

Elimu unayowapatia wana wako bado haitoshi na haikidhi kuwakomboa kifikra na kiuchumi wanao, kwa maana utegemezi na umaskini bado unawatesa ilhali wana vyeti kibao. Hebu sasa mama Afrika badili mfumo wa elimu uwapatiao. Usiwakaririshe sana maisha ya majirani zao bali andaa mfumo wa elimu ambao utaendana na hali halisi walizonazo. Ukiwafunza zaidi katika kujitegemea na kujituma kuujenga uchumi wao na wako mama ingali bado ni wadogo ili wakulie katika mlengo huo hadi ukubwani mwao.



HITIMISHO
Kwanini nimechagua Afrika?

Kwasababu mimi ni kijana niliyezaliwa barani Afrika mwenye shauku ya kuona bara langu halidharauliwi na hayo mabara mengine, na pia natamani kuona siku moja Afrika inajitegemea kifikra na kiuchumi bila ya kuwa tegemezi kwa wazungu.

Kwanini nimemfananisha Afrika na mama?
kwa sababu asili ya mama ni kuzaa, kulea, kutunza na kujitoa kwaajili ya maendeleo ya watoto wake. Katika damu na nyama Afrika inaweza kufananishwa na mama ambaye amezaa watoto 54-ambazo ndizo hizo nchi zilizomo Afrika

Kwanini nimemuambia amka Afrika?
Kwasababu licha ya uzuri na wingi wa mali zake, Afrika ndio limekuwa bara lakudharaulika na lenye uchumi mdogo zaidi kuliko mabara yote. Huo ufinyu wa maendeleo yake nimeufananisha na usingizi. Hivyo nimemuambia aamke atoke kwenye huo usingizi ili ashike usukani wa kuwa bara kubwa kiuchumi na kimaendeleo kwa maana anaweza.

Tuungane sote kwa pamoja na kwa vitendo tumsisitizie mama yetu-Amka Afrika, Amka mama.

Afrika yenye nuru ya kesho ipo katika mageuzi na jitihada zetu za leo.

#AfrikaTUNAWEZATuamkeniWAAFRIKA!!!

MUNGU IBARIKI AFRIKA.

1663083234900.png


Picha zimechukuliwa kutoka (shutterstock.com,istockphoto.com,vectorstock.com,freepick.com) na zimenakshiwa na kuongezewa ubunifu na muaandaji wa makala hii.
 
Upvote 1
Karibuni kwa maoni na ushauri, namna gani ambavyo Afrika tunaweza kujiendeleza kiuchumi bila kutegemea hao wanaojiita ni marafiki zetu kumbe kiuhalisia wamekuwa ndio chanzo kikubwa cha kutokuendelea kwetu. ili huu ujumbe uwe chachu ya maendeleo ya waafrika wa leo na wajao, kwa maana tusipoamka tutaendelea kukandamizwa na mataifa makubwa.

#AfrikaTUNAWEZATuamkeniWAAFRIKA!!!
 
Back
Top Bottom