Na Mwamba wa Kaskazini
Nimefuatilia akaunti za wasiotaka maendeleo ya Tanzania wote na kundi lao linaloumia kuona maendeleo yanayopigwa.
Wote hawa wamekuwa wakiushangilia wimbo mpya wa Msanii Roma ambaye kaimbaimba vitu vingi ambavyo hata yeye binafsi naamini ukimuuliza vingi hawezi kukwambia kwa nini kaimba. Hoja za kushikiwa.
Na waliopenyezewa fedha za ufadhili ndio walikuwa wa kwanza kuibuka kujifanya kama ndiyo wameuona kumbe wanaujua na walikuwa hata studio kuratibu mashairi. Ujinga sana huu.
Roma anaonekana kuingia katika propaganda iliyofeli-analalamikia demokrasia katika nchi ambayo hivi sasa yeye mwenyewe anazunguka nchi nzima kwa amani katika Tamasha la Fiesta akiwa na amani na kufanya muziki wake pamoja na kutukana sana viongozi majukwaani. Anataka nini zaidi?
Ni Msanii anayeimbishwa kasumba na propaganda asizozijua akiagizwa, kwa kujua au bila kujua, alilie demokrasia na uhuru wa kujieleza katika nchi ambayo yeye mwenyewe hivi karibuni kazunguka redio zaidi ya 20 kwenda kuutangaza wimbo wake alioimba na Stamina "Kijiwe Nongwa." Kote kaongea ya uongo na kweli na sasa anaendelea na bata la Fiesta. Ghafla mtu huyo huyo ataibuka kukwambia hakuna uhuru wa kujieleza!!
Namuona Roma aliyeshikiwa akili kabisa eti analilia demokrasia katika nchi ambayo hata yeye ameruhusiwa kuwa na akaunti ya Insta anaweka nyimbo zenye matusi lukuki kwa viongozi. Naona bado anaweweseka na walimteka. Asitumie hii kisiasa, aseme nani walimteka.
Haya ndiyo madhara ya vijana wanaojiona wasomi lakini wasiojielewa- wanajiita wanafalsafa kumbe ni mazuzu tu yanayotumika. Hajui siku wanaomtumia hapa yeye ni kwao, siku pakiwaka, wale watarudi kwao yeye atakwenda ukimbizini!
Unamsanii Roma anayelilia demokrasia kutoka upande mmoja, halili kubanwa demokrasia ndani ya CHADEMA ambako kuna kiongozi kawa Mfalme wa Wafalme, kuna wabunge wa upinzani wanaoburuzwa na kuchukiwa hata wanaposhukuru tu kwa majimbo yao kupata maji.
Shida yake kubwa anaumia kuona Serikali imefufua shirika la ndege sasa watanzania wanasafiri kwa bei nzuri na uhakika.
Roma na wanaomtuma wanaumia kuona tunaongeza mapato, tunazidi kuelekea kujitegemea, tunatoa elimu bure, vituo vya afya vimejengwa, hospitali za wilaya na mikoa zimemalizika na anaumia zaidi kuona ujenzi wa reli ya kisasa na mradi wa umeme Rufiji vyote kwa fedha za ndani.
Roma hana raha kuona mabarabara, flyovers, kuona walimu zaidi ya laki 1.24 wamepandishwa madaraja mwaka huu, shule zinaboreshwa. Hataki na inamuuma.
Roma anaona demokrasia ni watu kuachwa wafanye ghasia- waandamane bila mpango, wapore vitu vya watu, wazuie watu kufanyakazi n.k.
Ni ajabu sana kwamba Roma haoni chochote katika nchi yake-haoni, haoni, haoni. Ila si bure, macho anayo vizuri.
Siku mtakayojua nguvu inayowapotosha hawa vijana mtashangaa na mtabaki mnasaga meno. Lakini wajue Tanzania ni imara sana kuliko wanavyodhani.
Pole yako Roma, endelea kuimbishwa tu. Kitaeleweka.