Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

*ANGA LA WASHENZI II --- 81*


*Simulizi za series*



ILIPOISHIA


Hapa mhudumu akamtazama Jona machoni, wakatazamana kwa sekunde nne pasipo kufanya jambo.


“Okay!” Mhudumu akabinua mdomo. “I will do what you wish.” kisha akasogelea mvinyo na kumiminia kwenye glasi.


ENDELEA


Kabla hajautia kinywani, akasita. Akamtazama kwanza Jona na kisha Lee. Nyuso za wanaume hao tayari zilikuwa zimebeba shaka. Mambo hayakuwa sawa.


Basi mhudumu huyu akapeleka glasi kinywani, ila kabla hajafyonza, akachomoa upesi bunduki yake toka kiunoni. Alifunua sketi yake upesi kiasi kwamba hata nguo ya ndani haikuonekana. Kabla hajawanyooshea wakina Jona na kufyatua, Jona akawa amemfikia! Ila bado akafyatua. Risasi ikaruka na kutoboa mlango.


Kabla tena hajafanya jambo, Jona akawa amempokonya bunduki. Ila naye mhudumu akawa na upesi, hakumruhusu Jona amshambulie, akamng’ang’ania mkono wake, Jona akauvuta kwanguvu na kumtandika kiwiko, akadondoka chini!


Alikuwa anavuja damu puani. Kichwa kilikuwa kinamgonga sana. Hakuweza kunyanyuka tena na kupambana. Jona akamfunga kinywa na mikono kwa kutumia mkanda wake kisha akaenda upesi kwenye chumba cha Miranda kwani alihisi huenda mhudumu yule akawa ameshapitia huko kwani chumba chake kilikuwa cha mwisho kwenye utaratibu wa namba.


“Who’s it?” sauti ya Miranda iliuliza.


“It’s me, Jona!”


“Jona?” Miranda akajiuliza kwa sauti yake ya chini. Alikuwa ameketi kitandani akiwa bado hajatoa taulo mwilini mwake. Kwa ujumla alikuwa amejifunga mataulo mawili, moja kifuani na lingine kichwani, ila kuendea mlango, akajivesha taulo kiunoni kutimiza matatu.


“Umekunywa wine?” lilikuwa swali la kwanza la Jona. Aliuliza akiwa ametoa macho na akizama ndani kwa kuusukuma mlango. Alipotupa macho akaona chupa ya wine mezani. Haikuwa imefunguliwa. Hatimaye akashusha pumzi.


“Kuna nini Jona?” Miranda akauliza kwa uso wa mashaka.


“Tupo under attack,” Jona akamjibu akimtazama kwa macho ya hakika. Ila hakusema sana, akaenda kuufuata mlango atoke, ila kabla akamtazama Miranda na kumwonya, “Usinywe hiyo wine!” kisha haraka akauendea mlango kuelekea kwenye chumba cha wale makomandoo.


“Vipi, amekunywa?” Lee aliuliza. Alikuwa ni punde ametoka kwenye chumba. Ameshavalia suruali na shati jepesi.


“Hajanywa!” Jona akajibu akiwa na haraka. Akauendea mlango wa wale makomandoo akiwa anaongozana na Lee kwa nyuma. Akaukuta mlango ukiwa umefungwa. Akagonga pasipo mafanikio. Akauvamia kuuvunja.


Kutazama ndani akawaona mabwana wale wakiwa wamelala kitandani. Hawakuonekana kujielewa. Na kama wangelikuwa wazima basi wangelikuwa wamedamka punde waliposikia mlago ukigongwa, hata basi ukivunjwa.


Chupa ya wine ilikuwa tupu, haina kitu!


“Wamekunywa!” Lee akaropoka. Walitazamana na Jona, Jona upesi akawafuata wale makomandoo na kuwanusa. Walikuwa wananuka pombe!


Lakini zaidi hawakuwa wanapumua! Mapigo ya moyo yalikuwa yamezima! Kiufupi, walikuwa wamekufa.


“Tunafanyaje, Jona?” Lee akauliza.


“Sijui!” Jona akasema akiketi kwenye kitanda. Alishika kichwa chake kwa mawazo.


Ila upesi akiwa amekumbuka jambo, akamtazama Lee na kumwambia, “Tuondoke hapa upesi! Wauaji wameshajua wapi tulipo.”


“Na vipi kuhusu hii miili?” Lee akauliza.


“Inabidi tuondoke nayo. Hatuwezi kuiacha hapa!” Jona akasema akisimama.


“Hapana, Jona!” akasema Lee akitikisa kichwa. “Ni hatari sana kufanya vivyo. Hatujui maadui wapo wapi, wapo wangapi. Tutawezaje kujiokoa na huku tuna miili mitatu?”


“Sasa tutafanyaje?” akauliza Jona. Alikuwa ni kama mtu aliyechanganyikiwa. Kwa muda akili yake ilikuwa haifanyi jambo. Alikuwa anawaza mambo mengi kwa wakati mmoja.


“Tutapiga picha na kuzituma mtandaoni,” akasema Lee. “Tutaandika caption, najua picha itasambaa mtandaoni na watapata namna.”


“Seriously?” Jona akatia shaka.


“Ndio. Jona hatuna muda hapa. Lazima tufanye maamuzi ya hekima ama wote tuwe wafu!”


Kabla Jona hajasema jambo, wakasikia sauti za vishindo. Wakahisi si shwari. Haraka Lee akachomoa simu na kupiga picha miili ya wale makomandoo …


Huko nje koridoni kulikuwa na wanaume wawili na mwanamke mmoja. Watu hawa waliokuwa wanatembea sambamba walikuwa wamebebelea bunduki mikononi mwao. Nyuso zao zilikuwa za kazi na macho yao yalikuwa yanaangazia milango mitatu inayofuatana.


Milango mitatu ya vyumba vya Jona na wenziwe.


Basi punde walisimama mbele ya chumba cha wale makomandoo. Chumba hicho kilikuwa wazi tu. Hawakuona mtu. Basi wakausogelea mlango, walipofika, wale wanaume wawili, ghafla mlango ukafungwa kwanguvu na kuwakumba!


Wakaweweseka. Walimparamia mwanamke aliyekuwepo nyuma yao na huo ukawa mwanya mzuri kwa wakina Jona kushambulia. Haraka Jona na Lee wakawarukia, na kwa ustadi wao, wakawapokonya silaha na kuwalalisha chini kwa maumivu.


Haraka wakamshtua Miranda na kumwambia waende upesi kwani mambo yameharibika. Upesi Miranda akatoka na wakaelekea kaskazini mwa hoteli. Muda si mrefu, kwenye eneo la tukio, pale walipokuwa wameachwa wale watu walio hoi kwa kipigo, akawa amewasili mwanamke kamanda, Sword, akiwa ameongozana na watu wanne wengine.


“Where are they?” Mwanamke huyo akauliza. Mwanaume mmoja akanyooshea kidole chake upande wa kaskazini, basi haraka mwanamke huyo kamanda akiwa ameongozana na watu wake wakaelekea huko.


Walisaka, hawakuona mtu! Kabla hawajarudi kwa wale wenzao, wakasikia sauti ya mtu anagugumia. Kwenda kutazama, wakamkuta mlinzi akiwa amefungwa mdomo.


“They’ve escaped!” Mwanamke kamanda akaropoka. Geti la uani lilikuwa wazi. Wakina Jona walikuwa wametoroka, na ni wazi haikuwa muda mrefu. Bado geti lilikuwa linachezacheza!


Basi haraka kamanda Sword na wenzake wakakimbilia huko. Kutazama kushoto na kulia, kwa mbali mkono wao wa kuume, wakaona mtu anaishilia. Wakaanza kukimbia kuelekea huko, kufika hawakuona mtu!


“Shit!” akalaani kamanda Sword akipiga kofi paja lake. Mazingira yalikuwa tulivu mno. Ni usiku huu tena mzito. Magari machache yalikuwa yanaonekana barabarani, watu wanaotembea kwa mguu hawakuwapo.


Basi punde, mawasiliano yakaungana toka kule makaoni. Mwanaume yule aliyekuwepo kwenye mitambo akawaambia wapi alipowaona walengwa wao. Ni mtaa wa pili toka walipo. Wapo barabarani bado hawajapata usafiri!


Lakini pia akawaonya kuwa mmoja wao ameshikilia bunduki.


“Let’s go!” akaamuru kamanda. Moja kwa moja wakaenda huko walipoambiwa.



**



Asubuhi na mapema kila kituo cha habari kikarusha taarifa juu ya watu waliokutwa wakiwa wafu kwenye moja ya mtaa wa London. Watu hao walikuwa ni wale waliokuwa wanawafukuzia wakina Jona, kwa idadi watu wanne! Wawili miongoni mwao wakiwa majeruhi wapo hospitali kupokea huduma.


Mbali na hayo, pia hata ile miili ya wale makomandoo na kile kilichotokea kule hotelini kikarushwa na watu wakajua. Hata watu wa Tanzania nao wakapata habari juu ya wanajeshi wao kwenye nchi ya kigeni. Kuitikia hilo, shughuli za kufuatilia miili hiyo ikaanza mara moja.


Basi, mambo yakazidi kupamba moto. Kwakuwa kikosi nambari ‘wani’ kilikuwa kimeshashindwa kufanya kazi yake ya kuwamaliza wakina Jona, ikabidi sasa kitumwe kikosi cha pili. Cha sasa pia kilikuwa kinaongozwa na watu kumi chini ya kamanda mwanamke mwenye jina la Arrow.


Nao wakadumu kwa siku moja. Wote wakapukutika. Kikatumwa kikosi cha tatu na cha nne, nao hawakuwa wameambulia kitu. Wote wakamalizwa kana kwamba maji. Ilikuwa ni kama utani, lakini watu wakienda hakuna aneyerejea zaidi ya taarifa ya habari ya watu kukutwa kwenye mahoteli, ama barabarani!


Kabla ya kikosi cha tano hakijatumwa, Kamanda mkuu, akaona ni kheri kabla hawajafanya hilo, watulie kwanza kuona wapi wanakosea. Ni wazi sasa wakina Jona watakuwa wanafahamu wanachokifanya.


Wakapanga mipango madhubuti ya kuwa, punde wakina Jona watakapoonekana kwenye kamera basi watoe taarifa polisi kwanza. Wahakikishe watu hao wanahitajika na serikali. Na basi picha zao zitazagaa kutangazwa kwenye vyombo vya habari.


Hapo watakuwa wameihamishia kesi mikononi mwa serikali. Ila,


“Don’t you think it will be risk even for us?” akauliza mmoja. Walikuwa wanafahamu wakina Jona watakuwa ni watu wanaujua nyendo zao, vipi wakikamatwa na polisi, hawatatoa taarifa zao huko kituoni?


“No!” akasema Kamanda mkuu akitikisa kichwa. “Before doing that I will have already killed them!” Basi kikao cha dharura kikawa kimeishia hapo. Na siku hii ikaenda salama mpaka kwenye majira ya saa tano usiku.


Kamanda mkuu akatoka kwenda kwenye tafrija fupi iliyokuwa imeandaliwa na Malkia kwa ajili ya kumpongeza mmoja wa vijana wake, kwa jina Prince Henry, kwa kupata mtoto wao wa kwanza na mwanamke aitwaye Diana Lavik, mwanamke mwenye asili ya kilatini.


Tafrija ilikuwa imehudhuriwa na watu wakubwa na wazito. Ulinzi ulikuwa mkubwa. Watu walikuwa wamependeza kwa suti na magauni ya kumetameta aghali.


Basi bwana Kamanda alipoiingia, haikuchukua muda kupata kinywaji mkononi mwake. Na pia watu wawili watatu wa kupiga naye soga za hapa na pale. Ila akiwa anafanya hivyo, mara akasikia sauti ya mwanamke nyuma yake.


“Hey, gentleman.”


Sauti hii ilikuwa kavu ila tamu masikioni. Haikumchukua muda kamanda akageuka kutazama. Hamaki uso kwa uso akakutana na mwanamke mwenye rangi ya dhahabu. Nywele zilizofundwa vema na macho ya kuvutia. Kiuno kimekabwa na gauni na amepanda kwa viatu virefu nyeusi.


Mwanamke huyu alikuwa ni Glady.


“Do I know you, madam?” Kamanda akauliza.


“Yes, you do!” akajibu Glady akirembua. “Would you mind a dance?”


“Off course!”


Glady akamkwapua Kamanda na kusonga naye kando kucheza wimbo wa taratibu uliokuwa unapiga. Sikioni mwake sauti ya mbali ikamwambia, “Hakikisha unamuua.”




***



LAKINI GLADY ATASEMA YEYE NI NANI? NA ATAMUUAJE KAMANDA KWA WATU WENGI HIVI? WENZAKE WAKO WAPI?
 
Movie inaendelea kwa bahati mbaya hakuna anyejua iko hatua ya 2 au katikati, au sehemu ya3 au ya mwisho.. Tuendelee kuwemo.
 
*ANGA LA WASHENZI (MWISHO)*


*Simulizi za series*



ILIPOISHIA


“Do I know you, madam?” Kamanda akauliza.


“Yes, you do!” akajibu Glady akirembua. “Would you mind a dance?”


“Off course!”


Glady akamkwapua Kamanda na kusonga naye kando kucheza wimbo wa taratibu uliokuwa unapiga. Sikioni mwake sauti ya mbali ikamwambia, “Hakikisha unamuua.”


ENDELEA


Kamanda alimtazama Glady machoni akamwona mwanamke mrembo haswa. Mwanaume huyu hakuwa mtu wa kupenda rangi nyeusi, ila hapa kwa Glady akachina haswa. Hakuwahi kumwona mwanamke mrembo kama huyu. Kwenye mikono yake alikuwa anampatia joto fulani analolihitaji.


Na zaidi ya yote Glady alikuwa na kitu ambacho wanawake wote wa kizungu aliokuwa nao hawakubahatika kuwa nacho - shepu! Kiuno kinajulikana kipo wapi, na baada ya kiuno basi nini kinafuatia.


Hakika hapa bwana Kamanda alikuwa ameshikwa. Ugumu na ukatili wake wote ukawa ni sponji chakavu mbele ya mwanamke kubuhu. Mtambo. Bibie Glady.


Kwa kujiamini kabisa mwanamke huyo alikuwa anamtazama mwanaume huyo machoni. Lakini siyo kumtazama kama ujuavyo wewe, lah! Kumtazama kiuanamke. Kumtazama kwa macho yanayoomba huba. Macho yanayolilia mapenzi ya ndani!


Ama kwa hakika chunusi ilipata kucha ndefu. Kiuno cha Glady kilichokuwa kimeshikiliwa na mkono mpana wa Kamanda kilikuwa kinaenda kutoka na midundo ya muziki. Nyonga yake iliaga kila melodi.


“Who are you?” Kamanda akajikuta anauliza. Alishindwa kuvumilia zaidi. Hakutaka muziki ukome. Hakutaka mwanamke huyu atoke mikononi mwake. Na hii ndiyo ilikuwa sababu ya Glady kulipiwa kila kitu aje Uingereza. Hata wale waliokuwa wanatilia shaka, sasa walianza kusadiki. Kila kazi na mkono wake.


“My name is Rebentha…” akasema Glady pasipo kutumia nguvu. Lips zake zilizokuwa zimechovya ‘lipstick’ hazikuwa zikihangaika bali ulimi.


“Rebentha?” Kamanda akaguna. “Rebentha from?”


Glady akatabasamu. Kamanda akahisi amepigwa shoti, kwa muda kidogo akasahau hata alichouliza, akasema, “You are so beautiful, Rebentha!”


“Thanks,” Glady akaipokea kwa madaha na kusema, “I am from Caribbean.”


“Caribbean! Wow! I have never been there. How did you know me?”


“How long does it take to see a handsome lonely man in the party?”


Kamanda akatabasamu pasipo kutia neno.


“Honestly I don’t know you. But my eyes just fell on you. Is it wrong?”


Kabla Kamanda hajatia tena neno, Glady akatazama kushoto kwake kwa mbali na kusema alikuwapo kule akinywa kinywaji kabla hajamtia machoni mwanaume huyo aliyependeza akiwa mpweke, aongea tu na wazee hapa na pale.


“You are so confident!” akasema Kamanda.


“Doesn’t that turn you on?” Glady akauliza. Basi Kamanda akaishia kutabasamu, akamkumbatia kwanguvu mwanamke huyo na kucheza naye kwa muda kabla hajamwomba wakapumzike kidogo na kufanya maongezi zaidi.


Lakini kabla ya kwenda huko, Glady akamlaghai wacheze zaidi kwani bado ana hamu ya kufanya vivyo. Akiwa nyumbani huwa hapati huo muda na yeye kucheza ndicho kitu anapenda zaidi.


Basi Kamanda hakuona tabu. Hakutaka kumghafirisha mwanamke huyo mrembo, akampatia dakika tatu za ziada. Wakacheza na akiwa anamuuliza maswali ya hapa na pale, wapi ametokea na amekuja na nani?


Wakiwa hapo wanacheza kutafuna hizo dakika tatu za ziada, ndipo Glady akawa anapanga namna ya kufika kwenye kilele cha kazi yake. Wigi lake refu lilikuwa linamziba masikio yaliyokuwa yana ‘earphone’ za mawasiliano na pia hereni zake zenye ncha kali.


Baada ya kutazama huku na kule, akiwa anapiga mahesabu kichwani, akatengeua mguu wake wa kuume, kisigino cha kiatu kikameguka, akaangushia kichwa chake kwenye bega la Kamanda. Mara Kamanda akaguna kutoa sauti ya maumivu akiwa amekunja sura.


“I am sorry! … shit! Its my earring!” Glady akasema akitoa kichwa chake akijitahidi kusimama. Shingo ya Kamanda ilikuwa imechanjwa kidogo. Kwa mbali kulikuwa kuna kamstari kekundu. Na punde, damu ikaanza kuchuruza.


“It’s okay, never mind!” Kamanda akasema akishika eneo lenye maumivu. Kutazama vidole vyake akaona alikuwa anavuja damu, basi akamwomba mrembo muda mchache akapate kujiosha, atarejea.


“Its ok. I will be waiting,” akasema Glady akiwa na sura ya taharuki na huzuni. Mwanamke huyu aliigiza haswa. Basi Kamanda akaenda zake ‘washroom’ Glady akimtazama mwanaume huyo akiishia, kisha akaweka kidole chake sikioni na kusema,


“Nimemaliza kazi!”


Ama kweli vitamu ndivyo venye sumu.



**


Alijihakikisha kama yupo sawa. Anhaa akaridhika. Damu ilikuwa haitoki tena hata tone. Basi akajifuta kwa mara ya mwisho na kitambaa chake kilicholowana maji alafu akajitengenezea vema. Bado alikuwa amependeza na suti yake toka Italia.


Kamanda akajirekebisha nywele zake kabla ya kwenda kukutana tena na mrembo. Alipojihakikishia kuwa yuko sawia kwa kila kitu, akatoka kuuendea mlango. Ila kabla hajaufikia, akahisi kichwa chake kinagonga. Alisimama na kuskizia, akajiona bado yu vema, basi akaendelea na safari yake.


Alipofika kwenye uwanja akaangaza huku na kule, hakumwona Rebentha! Lakini punde , si Rebentha tu, hata watu wengine akawa hawaoni. Walianza kuwa maruweruwe, asione cha kueleweka! Kichwa kikamgonga sana, na damu zikaanza kummiminika toka puani kwa fujo.


Hakudumu kwa muda mrefu akiwa amesimama, akajikuta chini!


Watu wakamtazama na kumsogelea. Damu hazikukatika, zikaendelea kummiminika zaidi na zaidi kuchafua suti yake aghali. Kwa muda kidogo shughuli ikawa imesimama. Mwili wa Kamanda ukanyanyuliwa na upesi ukatiwa kwenye gari la wagonjwa lililokuwapo eneoni kuwahishwa hospitali, huku nyuma tukio hilo likiwa limeacha zogo.


Gari hilo la wagonjwa likatimka haswa, ving’ora vikitawala barabarani. Lakini kumbe waliopo humo ndani si wahudumu bali ni Jona na wenzake. Walikuwa wamevalia sare na vichwa vyao vimemezwa na kofia zenye chapa ya huduma.


Sasa watu hawa walikuwa wamempata Kamanda. Tena kwa ulaini kabisa. Gari hilo la wagonjwa baada ya kutembea kwa takribani dakika kumi na tano, likazima ving’ora na kutoka kwenye barabara kuu.


Likapotelea huko kusikojulikana.



**


Baada ya juma moja … Dar es salaam, kituo kikuu cha polisi.



Sauti ya kishindo cha miguu yenye buti ilikomea mbele ya lango la nondo za chuma, hapo akasimama Askari mnene mweusi mkononi akiwa amebebelea bunduki na kiunoni mwake amening’iza pingu.


Akatazama ndani ya chumba cha mahabusu, macho yake makubwa yakaangukia kwa mtu mmoja aliyekaa nyuma kabisa. Jona. Akampa ishara ya kichwa kumtaka asonge karibu. Jona akafanya hivyo. Akashika nondo na kumuuliza askari,


“Mmefanya nilichokiomba?”


Askari hakumsemeza jambo, akachojoa ufunguo na kufungua lango, Jona akatoka. Akaongozana naye mpaka kaunta ambapo huko alikutana na Makamu wa Raisi, ambaye kwa sasa ndiye alikuwa amekaimu kiti cha Raisi.


Akamsalimu na Makamu akamuuliza, “Ndiyo wewe Jona?”


“Ndio, mheshimiwa.”


“Hata kama usingeliomba kuonana na mimi, ningekuja kuteta nawe maana nahisi nina mengi ya kusikia toka kwako.”


Basi Jona akapatiwa nafasi ya kuteta pamoja na Makamu wa Raisi kwa faragha. Akamweleza yote toka herufi A mpaka Ze. Na kama haitoshi, akamkutanisha mheshimiwa huyo na wenzake: Miranda, Lee na Marwa. Nao kila mmoja kwa nafasi yake akaeleza yote yale ya kweli, na hata kuthibitisha wayasemayo kwa nyaraka na shahidi mbalimbali zilizokuwa mikononi.


Makamu wa Raisi akapigwa na butwaa na yale yote aliyoyasikia. Ilikuwa ni ngumu kuyakataa kwani hata matukio yaliyokuwa yanatukia ndani ya nchi pasipo na majibu ya uhakika, yaliungana mkono na maelezo na shahidi zilizotolewa.


Akaamuru wale wachimba madini, wakina Nyokaa, watiwe nguvuni upesi. Pia akatoa agizo wakina Jona waachiwe huru, lakini akamtaka Jona aonane naye faragha baada ya majuma mawili. Zaidi akawapatia kiasi fulani cha fedha kama motisha kwa kupigania nchi yao kwa dhati.


Siku hiyo Jona na wenzake wakafanya tafrija nyumbani kwa kujipongeza. Wakamwalika pia Glady na Miriam ambaye hakusita kuja upesi. Tafrija ikafana sana na kila mtu akafurahia isipokuwa kwa Sheng ambaye alikuwa mlemavu wa kudumu kwa kupooza.


Yeye alikuwa kwenye ‘wheelchair’ akitokwa na machozi. Hakuwa anaweza kusogeza mwili wake hata kidole. Alikuwa ni wa kufanyiwa kila kitu, na kwakuwa hakukuwa na mtu mwenye muda huo, wote walishakubaliana kuwa mwanaume huyo atatumwa kwenda kwao China kukutana na familia yake.


Kwa mujibu wa daktari hakuwa anaweza kudumu hai zaidi ya miezi miwili tangu sasa.


“Samahani sana, Sheng,” alisema Lee. “Sitaweza kuwa nawe tena kwa sasa maana nimepata familia mpya. Nasikitika maana utakuwa mpweke sana, na mikono yako iliyozoea kuua haiwezi tena kufanya kazi hiyo.


Ila nina furaha pia maana kwa sasa hatimaye utakuwa huru kuwa na familia yako. Hautakuwa na haja ya kujificha tena maana wote wameshamalizana wenyewe kwa wenyewe. Pengine kwa muda kidogo tutaiona dunia ikiwa tofauti.


Kwaheri Sheng.”



Lee aliposema hayo, akambusu Sheng kwenye paji la uso na kurudi tafrijani alipokutana na Glady na kukumbatiana kwa huba. Ila muda si mrefu, Jona akamwita na kumtaka faragha.


“Kuna lolote?” akauliza.


“Ndio, lipo,” Jona akajibu na kisha akatazama kushoto na kulia kuhakikisha kama wapo wenyewe. Akamnong’oneza jambo Lee, Lee akatabasamu. Ghafla, Lee akamshika mkono Jona na kumvutia tafrijani kisha akapaza sauti,


“Naomba tuskizane tafadhali!” muziki ukazimwa. Watu wote wakawatazama. “Jona hapa ana kitu cha kuwaambia…”


“Mimi?” Jona akatahamaki.


“Oooh basi nitakusaidia kusema …” Lee akapayuka. “Jona wants to marry Miranda!”


Watu wakalipuka kwa shangwe, ila Miranda akaziba mdomo wake akiwa ametoa macho kwa kutoamini. “Serious?” akauliza akitahamaki. Basi Jona akamtazama na kujikaza akimwambia, “Yes, serious!”


Mara Miriam akadondoka chini na kuzirai.



***



NASHUKURU SANA KWA KUWA NAMI MPAKA MWISHO. KWA WALE WATAKAOHITAJI KUWA PAMOJA KWENYE SIMULIZI YETU MPYA YA MWEZI WA TANO, ROHO YAKE INADAI, TUTUMIANE UJUMBE WHATSAPP KWA NAMBA 0685 758 123.


NAWAPENDA! MAMBO MAZURI HAYAKOMI KUJA.
 
Back
Top Bottom