Polisi wa kituo cha Wilaya ya Monduli Mkoani Arusha wanadaiwa kumpiga risasi raia aliyetambuliwa kwa jina la Yohana Nasieli kwa kile kilichoelezwa kuwa ni wivu wa mapenzi kati ya mke wa marehemu na askari polisi.
Habari kutoka kwa ndugu na majirani wa marehemu zilisema kuwa tukio hilo limetokea aprill 12 mwaka huu majira ya saa 1.35 usiku katika mtaa wa sabasaba kata ya Monduli Tarafa ya Kisongo wilayani humo.
Vyanzo vilisema kuwa siku ya tukio ya marehemu alikuwana ugomvi na mke wake, Paulina Kiliani{37} na kumlalamikia mke wake kuwa sio mwaminifu katika ndoa akimtuhumu kuwa na mahusiano na askari polisi aliyefanya mauaji {jina linahifadhiwa} kuwa ndio mvunja ndoa yake.
Vyanzo vya habari viliendelea kusema kuwa siku ya mauaji marehemu na mke wake walikuwa na ugomvi mkubwa na kufikia hatua ya kupigana na mke alimpigia simu ya kiganjani askari polisi huyo na kumwelezea kupigwa kwake na mume wake na askari huyo akiwa na mwenza wakiwa na silaha walikwenda eneo la tukio.
Habari zilisema kuwa baada ya marehemu kumwona askari yule yule anayemtuhumu kufanya mapenzi na mke wake akiwa wa kwanza kufika eneo la tukio,marehemu kwa hasira huku akiongea kwa jazba kuwa wewe ndio niliyekuwa nakutafuta ghafla aliingia ndani ya nyumba yake na kuchukua panga kwa nia ya kumtishia askari huyo akiwa na mwenzake ili aondoke eneo la tukio.
Vyanzo vilisema kuwa kabla ya marehemu kufanya tukio la kutaka kumkata Askari huyo,ghafla askari huyo alifyatua risasi na kumpiga marehemu kifuani kushoto na mguuni na kufariki dunia papo hapo.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo alithibitisha tukio hilo kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari ambapo imesema kuwa NASIELI alijeruhiwa kwa risasi upande wa kushoto wa mguu na kwenye bega la mkono wa kushoto baada ya kukaidi amri halali ya askari Polisi ya kukamatwa na kutaka kumkata askari panga alilokuwa nalo mkononi mwake.
Kamanda aliendelea kueleza katika taarifa yake kuwa marehemu alikuwa amewafungia watoto wake na mtoto wa jirani yake ndani ya nyumba kwania ya kuwadhuru na baada ya kutoa taarifa askari waliamua kwenda eneo la tukio kwa nia ya kuwaokoa watoto lakini pia kumkamata mtuhumiwa.
Taarifa ilisema baada ya kufika eneo la tukio walianza kugonga mlango uliokuwa umefungwa ili kuokoa watoto waliokuwa hatarini wakati wanaokoa watoto hao nje ya nyumba hiyo walimwona mtuhumiwa huyo akiwa amejificha akiwa ameshika panga Mkononi huku akiwa fuata askari hao kwa lengo la kuwadhuru.
Alisema baada ya hali hiyo ndipo alipoamua kumpiga risasi kwenye bega lake la kushoto hali iliyosababisha kuvuja damu nyingi na kisha kupelekwa katika hospital ya wilaya ya Monduli na mtuhumiwa huyo alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu.
Ends...