Dar es Salaam. Saa chache baada ya kutangazwa kwa bei mpya za vifurushi, Serikali imetangaza kusitisha kutumika kwa gharama hizo hadi hapo itakapotangazwa baadaye.
Uamuzi huo unaweza kuwa habari njema kwa watumiaji wa mitandao ya simu ambao, tangu kutangazwa kwa bei hizo mpya mapema leo Ijumaa ya Aprili 2, 2021, wamekuwa kwenye mjadala mzito kwani, matarajio ya wengi ilikuwa ni kushuka kwa gharama hizo.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Semu Mwakyanjala, amesema matumizi ya bei mpya ya vifurushi yamesitishwa kwa muda.
Hata hivyo, amesema uamuzi huo utahusu vifurushi vya data pekee huku vile vya ujumbe mfupi wa maneno na kupiga zitaendelea kama ilivyotangazwa mapema leo Ijumaa.
“Tumesitisha matumizi ya gharama mpya za vifurushi hadi hapo itakapotangazwa baadaye. Lakini, hili litahusu vifurushi vya data pekee na vile vya sms na kupiga vitaendelea kama kawaida,” amesema Mwakyanjala alipozungumza na Mwananchi kwa njia ya simu dakika chache zilizopita.
Kanuni ndogo za gharama na tozo za vifurushi, utangazaji wa huduma na ofa maalum zilizotungwa na TCRA, zimeanza kutumika leo ambapo, matumaini ya wengi ilikuwa ni bei za vifurushi kupungua lakini ikawa tofauti.