Tukiangalia dini za uongo na imani mbalimbali za upotovu duniani, na moyo wa kuzipenda unaowafanya wafuasi zake waziunge mkono imani hizo, inaonesha ushahidi madhubuti kuwa watu hao hawawezi kuugundua ukweli kwa sababu ya upofu wa misimamo yao juu ya imani zao.
Ufuasi wao king`ang`anizi, kwa kawaida hauegemei ufahamu wa kiakili juu ya mafundisho, bali unategemea utamaduni wenye nguvu na vishawishi vya kihisia.
Kwa kuwa walilelewa katika familia au jamii maalum, wao wanashikamana madhubuti na imani ya jamii hizo, wakiamini kuwa, wanauunga mkono ukweli.
Njia pekee inayoweza kuufikia ukweli juu ya kitu chochote kile ni kukijongelea kitu hicho kupitia mfumo maalamu na kwa kutumia akili.
Kwanza, tuupime ushahidi kisha tunauhukumu kwa akili alizotupa Mungu.
Katika ulimwengu wa maada, kimsingi ni akili ndizo zinazowapambanua wanadamu na wanyama, akili ifanyayo kazi vizuri katika silika (maumbile) yake.
Baada ya kuubainisha ukweli bila kupendelea, hapo ndipo tujibebeshe majukumu ya ukweli huo kihisia.
Ndio, kuna nafasi ya kuwa na msimamo wa kihisia, lakini msimamo wa kihisia lazima uje baada ya ufahamu wa kiakili juu ya kadhia husika, kisha ndipo mtu ajiandae kiakili na kiroho kuutetea ukweli huo kwa juhudi.