JanguKamaJangu
JF-Expert Member
- Feb 7, 2022
- 2,780
- 6,607
Nyumba hii ambayo ni mali ya Mary Victor Mahundi, mwandishi wa habari wa Gazeti la Raia Mwema la Dar es Salaam imepigwa mnada kwa Tsh. Milioni 30 ili kufidia deni la benki la Tsh. Milioni 5.2 ambalo alikuwa akidaiwa mume wa mwanahabari huyo.
Inaelezwa kuwa nyumba hiyo iliyopo Tabata, Kata ya Kinyerezi, Mtaa wa Kichangani ilipigwa mnada siku chache zilizopita na tayari mwandishi huyo na familia yake wametakiwa kutoka ndani ya nyumba ndani ya siku 14, leo Desemba 5, 2022 ikiwa ni siku ya 9 kati ya siku alizopewa kuhama.
Mary amesema taarifa hiyo ni ya ukweli na kudai kuwa alikuwa akifahamu juu ya deni hilo la mumewe lakini hakuwa anajua kilichokuwa kikiendelea hadi kufikia hatua ya nyumba hiyo kupigwa mnada.
“Nilikuwa Dodoma katika shughuli zangu za uandishi wa habari, nikapokea simu kutoka Serikali ya Mtaa kunijulisha kuwa nyumba yangu inapigwa mnada.
“Niliporejea nikapata nakala ya barua ya taratibu za nyumba kupigwa mnada moja ikiwa imetumwa katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya na benki wamefuata taratibu nyingine zote inavyotakiwa, lakini hilo deni ni la mume wangu ambaye kwa sasa hatupo naye pamoja.
“Nimewasiliana na Mkuu wa Wilaya kumueleza hali ninayopitia kwa kuwa hii nyumba si ya mume wangu peke yake ni mali ya familia, yeye (mume) kwa sasa hayupo nasi anaishi sehemu nyingine, inamaanisha kuwa tutatakiwa kuondoka ndani ya siku hizo 14, na kuwa watatuletea mabaunsa na kututoa kwa nguvu. Mkuu wa Wilaya ameniambia anashughulikia suala langu.
“Wakati huohuo, napambana kutafuta msaada wa kisheria ili kuweka zuio kabla ya hakimu na Majaji kwenda likizo ya kufunga mwaka, kwa kuwa sikushirikishwa katika huo mchakato wao wa mnada,” anasema Mary.
Nyaraka za benki zinaonesha kuwa deni lililosalia ni Tsh. 4,759,368 (Milioni 4.7), asilimia 10 ya deni ni Tsh. 475,936, hivyo jumla deni ni Tsh. 5,235,304.
Mary ameongeza kuwa: "Naomba kama kuna yeyote ambaye anaweza kunipa msaada wa kisheria anisaidie katika hilo kwa kuwa hapa nawazi nitaishi vipi na wanangu, kwanu hata huyo mume bado nina kesi naye kwa kuwa alibadili nyaraka na kuofanya nyumba ionekane ya kwake peke yake wakati hii nyumba ni ya familia, nina watoto, nitaenda wapi mimi na watoto wangu!