Kuhusu tafasiri za Biblia, kuna fasiri nyingi sana zaidi ya lugha 2000, lakini tafasiri zinaweza zisiwe salama kulingana na mfasiri lakini maandiko[MATINI] yapo salama kabisa tokea yameandikwa na manabii na Mitume. Ndio maana Yesu alisema hata nukta wala yodi haitatanguka mpaka yote yatimie, hivyo mtu akikuambia kuwa maandiko hayapo salama yamechafuliwa mwogope kama ukoma au homa ya Ini, maana huyo ni mpinga Kristo. Bwana alisema hivi,
“…maandiko hayawezi kutanguka..[Yohana 10:35].
Kwa maana, amin, nawaambia ,Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka,yodi moja wala nukta moja ya torati haitaoondoka ,hata yote yatimie. [Mathayo 5:18].”
Na nabii Isaya kwa njia ya Roho wa Kristo alisema hivi,
“Majani yakauka, ua lanyauka; Bali neno la Mungu wetu litasimama milele. [Isaya 40:8].”
Hivyo maandiko[matini] yapo salama kabisa, ila tafasiri zinaweza zisiwe salama, kuna kalamu za waandishi zimeingiza hila kwa kuongeza na kupunguza au kwa kinywa pale wanapotafasiri au wanapofundisha kiasi cha watu kuona kama vile Biblia inajipinga. Maana kuna aina mbili za kalamu, moja ni kalamu ya wino na nyingine ni kalamu ya ulimi, hizi ni kalamu hatari sana ambazo zinaweza kupindua dunia au kuwasha moto. Tazama [Zaburi 45:1; Yer 8:8; Yakobo 3:5-9]. Hivyo inakupasa kuwa makini kwa usomaji wako wa Biblia, hivyo ndio maana watu wanaenda kusoma vyuo vya Biblia ili wapate kujua maana iliyokusudiwa kupitia matini[maandiko kwa lugha ya kale]. Lakini bado unaweza usiwe salama kwasababu kila chuo kinavutia katika eneo lake, maana vyuo karibu vyote vinamilikiwa na madhehebu fulani; Hivyo lazima kila dhehebu lifundishe Biblia kulingana na kanuni za Imani zao. Na hiyo ni hatari kubwa sana katika ufahamu wa kiroho, maana tunapaswa kusoma Biblia kibiblia, kwa maana ya kwamba yenyewe ituongeze katika maana husika iliyokusudiwa na si kwamba sisi ndiyo tuiongoze ikubaliane na misimamo au misingi ya Imani yetu. Kwahiyo sasa, ili uwe salama kabisa unapaswa kutumia njia ifuatayo,
ROHO MTAKATIFU: Hii ndiyo njia salama kabisa kwa msomaji wa Biblia, maana Roho mtakatifu ndio pumzi ya Mungu iliyovuvia manabii nao wakaandika maneno ya Mungu kupitia lugha za kibinadamu. [2 Petro 1:21]. Hivyo ili uielewe Biblia sharti uwe na ushirika wa Roho na si kuwa uwe na ushirika wa chuo cha Biblia au mchungaji wako au kasisi wako. Yesu aliahidi kutupa kinywa na hekima ambayo itatuwezesha kujua maandiko matakatifu kiasi cha wapinzani wa Biblia au wapinzani wetu kushindwa kukabiliana nasi.
AHADI YA YESU.
“kwa sababu mimi nitawapa KINYWA na HEKIMA ambayo watesi wenu wote hawataweza kushindana nayo wala kuipinga. [Luka 21:15].”
KUTIMIA KWA AHADI HII.
“Lakini baadhi ya watu wa sinagogi lililoitwa sinagogi la Mahuru, na la Wakirene, na la Waiskanderia, na la wale wa Kilikia na Asia, wakaondoka na kujadiliana na Stefano; lakini hawakuweza kushindana na hiyo HEKIMA na huyo ROHO aliyesema naye. [Matendo ya Mitume 6:9-10].”
Kinywa ndiye Roho Mtakatifu, hivyo watoto wa Mungu watapewa Roho na hekima ya Kristo kama Stefano ambayo itavunja vunja kuta za wasomi na wenye hekima wa dunia hii ambao wanaupinga ukweli wa Biblia. Na daima Mungu hufanya kazi na wanyenyekevu, huwainua kutoka katika kudharauliwa na kuwafanya kuwa vyombo vyake hodari. Mtume anasema,
“26Ndugu, kumbukeni wakati mlipoitwa: Wengi wenu hawakuwa wenye hekima hata kwa fikira za binadamu; wengi hawakuwa wenye nguvu au watu wa tabaka la juu. 27Ndiyo kusema, Mungu aliyachagua yale ambayo ulimwengu huyaona ni upumbavu, ili awaaibishe wenye hekima; na aliyachagua yale ambayo ulimwengu huyaona ni dhaifu, ili awaaibishe wenye nguvu. 28Mungu ameyachagua yale ambayo kwa fikira za dunia ni mambo yaliyo duni na yanayodharauliwa, mambo ambayo hata hayakuwako, ili kwa hayo ayafutilie mbali yale ambayo kwa fikira za binadamu ni mambo ya maana. [1 Wakorintho 1:26-28 BHN].”
KUAIBIKA KWA WENYE HEKIMA WA DUNIA.
Marabi na makuhani na mafarisayo wa dini ya Kiyahudi ambao walikuwa wasomi sana wa Torati na Elimu mbalimbali, walistajabia hotuba ya Petro na Yohana mbele ya baraza la hukumu, hotuba ambayo ilikuwa imevuviwa kiroho, na ikawachoma mioyo na kuvunja hila yao, na kitu walichokistajabia sana ni kuwa hao watu hawakuwa na elimu ya darasani wala chuoni. Baada ya kuona hali hiyo wakafanya utafiti wao na wakagundua hawa watu wanaongozwa na nguvu isiyo ya kibinadamu, imeandikwa,
“Basi walipoona ujasiri wa Petro na Yohana, na kuwajua ya kuwa ni watu wasio na elimu, wasio na maarifa, wakastaajabu, wakawatambua ya kwamba walikuwa pamoja na Yesu. [Matendo ya Mitume 4:13].”
Hivyo siri ya kuwa kama Petro au Yohana ama zaidi ni kuwa pamoja na Yesu, kumbuka Yesu aliahidi kuwa pamoja nasi mpaka ukamilifu wa dahari. [Mathayo 28:20]. Kwahiyo sisi si yatima, tunaye Yesu, na tunakuwa naye kwa njia ya Roho wake ndani yetu. [1 Yohana 3:24]. Ulimwengu hauwezi kumwona wala kumtambua Roho wa Kristo, ila sisi tutamtambua kwasababu anakaa kwetu na yupo ndani yetu. [Yohana 14:17].”
Unaweza kustajabia habari hii kuwa kuna watu leo wanachukua PHD zao kupitia nyaraka za Petro au Yohana ambao kwa kweli hao hawakuwa na shule yoyote wala kujulikana katika zama zao, walikuwa ni wavuvi tu wa Samaki. Elimu yao waliipata katika chuo cha Kristo kwa miaka mitatu tu na kujazwa Roho wa Kristo, kwa njia hiyo waliupindua ulimwengu na bado mafundisho yao yanazidi kuwaleta wengi katika hali mpya ya Kristo. Ni elimu ya ajabu, mtu mwovu[Jambazi, mzinzi, Malaya, Muongo, muuaji nk] kupitia nyaraka za Mitume anabadilika na kuwa mtu mwema; Hii si hali ya kawaida, upo uwezo nyuma ya nyaraka hizo na huo uwezo ni Roho wa Kristo.
SIRI YA KUMPATA ROHO WA KRISTO.
“Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie. [MDO 2:38,39].”
Hivyo hiyo ndiyo siri ya kumpata Roho wa Kristo. Na kama mkristo unapaswa kuwa na Roho ya Kristo, nje ya hapo huwezi kuielewa Biblia wala kufanyika mkristo mwana wa Mungu na kuwa na tabia njema, na vile vile hutakuwa katika milki ya Kristo bali yule adui wa Kristo. Mtume anasema hivi,
“Yeyote asiye na Roho wa Kristo, huyo si wake Kristo. [Warumi 8:9 BHN].
Neema ya Yesu Kristo iwe nawe.