Bwana Jasusi usiwe mshabiki wa Chadema bila kufanya utafiti hebu soma habari hii
Silaha zatumika kampeni Bmulo
Imeandikwa na Mwandishi Wetu, Biharamulo;
Tarehe: 24th June 2009 @ 19:20
Jeshi la Polisi mkoani Kagera limeelezea wasiwasi wake kuwa huenda wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika kampeni za uchaguzi mdogo Biharamulo Magharibi wana silaha, yakiwamo magobori.
Wasiwasi huo ulitolewa juzi na Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Henry Salewi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio la dereva wa mgombea ubunge wa CCM, David Modest (3 kushambuliwa na wanaoaminika kuwa wafuasi wa Chadema.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 11 jioni katika kijiji cha Nyambale kata ya Lusahunga, baada ya dereva huyo mkazi wa Biharamulo, kusimamishwa na wananchi wa kijiji hicho, wakiomba msaada wa kumpeleka mgonjwa hospitali na badala yake wakamchoma na bisibisi mwilini na kisha kummwagia majimaji yanayodaiwa kuwa tindikali lakini yakamkosa.
Kwa mujibu wa maelezo ya dereva huyo, baada ya kufika katika kijiji hicho, alisimamishwa na wananchi kadhaa waliokuwa kando ya barabara na kumweleza kuwa wana mgonjwa mwenye hali mbaya na wanaomba msaada.
Wakati tunampandisha mgonjwa ndani ya gari, ghafla lilikuja gari la Chadema likiwa na bendera za chama hicho na kusimama mbele ya gari langu, wakashuka vijana wanne na mapanga na bisibisi mikononi na kunishambulia
wengine walinipiga kwa ubapa wa panga huku wengine wakiendelea kunichoma kwa bisibisi, alidai dereva huyo huku akionesha majeraha aliyonayo mwilini.
Alidai baada ya wananchi kuona hali hiyo, walikimbia na kumwacha peke yake akishambuliwa, lakini baada ya muda mfupi walifika askari Polisi wawili, akiwamo Mkuu wa Kituo cha Lusahunga, ndipo vijana hao walitupa mapanga na kukimbia wakidai dereva huyo ndiye aliyekuwa na mapanga.
Baadaye askari walinichukua na kunipeleka hadi kituoni na wakati narudi kuwasha gari, nilibaini sina ufunguo kumbe walininyanganya na baadaye polisi walifuatilia ufunguo wakapewa na mtoto mdogo, akidai kupewa na vijana wa Chadema ambao wakati huo walikuwa wamekimbia na kutoweka eneo la tukio, aliendelea kudai.
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Kitengo cha Uchaguzi CCM Taifa, Matson Chizii, alisema CCM imechoshwa na vitendo inavyofanyiwa na Chadema tangu kuanza kwa kampeni hizo Juni 10 mwaka huu na kuanzia sasa haikataa kimya vitendo kama hivyo vikirudiwa.
Napenda nitamke wazi kwenu ninyi waandishi wa habari, kwamba CCM sasa tumechoshwa na hivi vitendo vya upumbavu wa Chadema...mara zote wametufanyia ujinga tumekaa kimya kwa sababu hatupendi vurugu ingawa uwezo wa kufanya hivyo tunao, lakini sasa tumechoka, alisema Chizii huku akionekana kujawa jazba.
Aliongeza kuwa CCM ndiyo inayoongoza serikali ya nchi hii vikiwamo vyombo vya Dola, hivyo kufanya vurugu mbele ya wananchi ni kuonesha kwamba haina ukomavu katika siasa na kuitaka Chadema kueleza sera kwa wananchi, badala ya kuanzisha vurugu kwa wananchi wa Biharamulo ambao uchunguzi wao umebaini kuwa hawapendi vurugu.
Narudia kwamba kama vitendo vya aina hii vitaendelea, vijana wetu wa CCM wataingia vitani na matokeo yake ni kwamba damu itamwagika Biharamulo kwa sababu ya ujinga wa Chadema ambao wameshindwa kueleza sera zao kwa wananchi wa jimbo hili na kugeukia vurugu
yasipokomeshwa na kudhibitiwa, CCM itajibu na kuyakomesha, lakini tutayakomesha kwa namna gani sitasema, alisema Chizii.
Hata hivyo, aliwataka wananchi wa jimbo hilo kutulia na kusikiliza sera za vyama vinavyoshiriki katika uchaguzi huo ili wachague chama wakipendacho, huku akiwahakikishia wananchi wa jimbo hilo kutotishwa na vurugu hizo kwa maelezo, kwamba Serikali ya CCM imeandaa ulinzi madhubuti kwa ajili yao na hasa siku ya upigaji kura.
Kamanda Salewi pamoja na kuthibitisha kuwapo kwa tukio hilo, aliwaonya watu wote walioingia wilayani humo kufanya vurugu wakati huu kampeni na kusema Jeshi la Polisi limejipanga kukabiliana nao. Alilitaja gari la Chadema linalodaiwa kuhusika katika tukio hilo kuwa ni Toyota Land Cruiser namba T 437 AHN, ambalo baada ya kuhusika katika tukio hilo, dereva wake alilikimbiza hadi mjini Biharamulo na kulificha ndani ya nyumba ya kulala wageni iitwayo Robert na yeye kutoweka na kukimbilia kusikojulikana na hadi sasa anatafutwa na Polisi.
Gari tayari tumelipata jana likiwa limefichwa ndani ya nyumba ya kulala wageni iitwayo Robert na baada ya hapo tuliwaweka askari wetu katika eneo hilo kulilinda na kumkamata dereva ama mtu yeyote ambaye atakwenda kulifungua. Tunadhani kuna mapanga humo ndani na hata magobori, kwa sababu tuna taarifa kwamba baadhi ya vijana wa Chadema walioletwa hapa, wana magobori, mapanga na majambia, alisema Kamanda. Aliongeza kuwa kama hadi jana watakuwa hawajaonekana, Polisi itawaita viongozi wa Chadema na CCM na kulivunja vioo gari hilo ili kubaini kilichomo ndani.